MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Maoni ya Mhariri Wananchi wanachezewa shere suala la posho za wabunge?
BOOKMARK THIS PAGE
Wananchi wanachezewa shere suala la posho za wabunge?  Send to a friend
Thursday, 02 February 2012 08:10

SUALA la posho za wabunge sasa linaonekana kuchukua sura ya sarakasi au mchezo wa kuigiza, kwani siku moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza kwamba Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameidhinisha ongezeko la posho za vikao kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku, Ikulu juzi ilitoa taarifa iliyokanusha kauli hiyo, ikisema Rais hajatoa kibali cha kuongeza posho hizo.
   
Muda mfupi kabla ya Ikulu kutoa taarifa hiyo ambayo bila shaka ilimfadhaisha sana Waziri Mkuu Pinda, Spika wa Bunge Anne Makinda alikuwa ameitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma ambako Bunge linaendelea na mkutano wake wa sita na kurudia kauli yake aliyoitoa mwaka jana  kwamba posho hizo zilianza kulipwa mwaka jana na Rais alikuwa tayari ameidhinisha ongezeko hilo la posho.
   
Wakati Spika Makinda akisema hivyo, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais iliyoko Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema maelekezo ya Rais kuhusu suala hilo la posho yako wazi kabisa na hakuna mahali popote ambapo alibariki posho hizo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais anakubali kwamba ipo haja ya kuangalia upya posho hizo za wabunge, lakini ilisisitiza kwamba Rais aliwataka wabunge kutumia kikao cha sasa cha Bunge kulizungumzia upya suala hilo kwa kutumia hekima na busara.
   
Tafsiri sahihi ya taarifa hiyo ya Ikulu ni kwamba Rais hakuwahi kuidhinisha rasmi ongezeko la posho hizo kama sheria inavyotaka, vinginevyo waraka uliotiwa saini na Rais wa kuidhinisha ongezeko hilo ungekuwa umetolewa hadharani kama ushahidi. Inawezekana kwamba pengine shinikizo la  wabunge kuhusu nyongeza hiyo liliwachanganya Waziri Mkuu na Spika wa Bunge kiasi cha kudhani kwamba Rais aliidhinisha nyongeza hiyo aliposema awali kwamba ulikuwapo umuhimu wa kuangalia upya posho hizo za wabunge. Hata hivyo, viongozi hao wangetegemewa kujiuliza kwa nini Rais aliwataka watumie hekima na busara katika kushughulikia suala hilo.
   
Mkanganyiko huo yabidi utukumbushe yaliyotokea huko nyuma wakati Spika Makinda alipotangaza mwaka jana kwamba tayari posho hizo mpya zilikuwa zimeanza kulipwa kwa wabunge lakini kauli hiyo ikapingwa vikali na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah aliyesema posho hizo zilikuwa hazijalipwa kwa sababu zilikuwa hazijaidhinishwa na Rais kama sheria inavyoelekeza. Mgongano wa misimamo hiyo ya Spika na Katibu wa Bunge ambaye ndiye mkuu wa Sekretarieti ya Bunge  hakika uliwashtua wananchi na kuonyesha pasipo shaka kwamba hapo palikuwa na tatizo.
   
Wananchi wengi walihoji kulikoni viongozi hao wawili wa Bunge watofautiane katika mambo ya msingi kama kanuni za fedha na maelekezo ya sheria iliyoanzisha chombo hicho? Kama sheria na kanuni zinasema mamlaka ya kuongeza posho za wabunge ni ya Rais na kwamba atafanya hivyo kwa maandishi, inawezekanaje Spika na Katibu watofautiane kiasi cha Spika kuamuru Idara ya Uhasibu ilipe posho hizo pasipo kumshirikisha mkuu huyo wa Sekretarieti ya Bunge? Hapa kuna maswali mengi magumu ambayo lazima yapewe majibu.
   
Lakini kwa upande mwingine, Ikulu nayo pengine inapaswa kubeba lawama kwa kuwachanganya wananchi, kwani ilikataa kabisa kutoa ufafanuzi wakati sakata hilo lilipoibuka mwaka jana. Tunadhani haikuwa sahihi kwa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu iliposema mwaka jana kwamba suala hilo aulizwe Spika wa Bunge wakati kilichokuwa kinatakiwa ni ufafanuzi kama Rais alikuwa ameridhia rasmi ongezeko la posho au la.
   
Ni bahati mbaya kwamba suala hilo limefikia hatua hii ya aibu bila sababu za msingi. Baya zaidi ni pale suala hilo linapoibuliwa tena wakati huu ambapo madaktari wako katika mgomo wakidai nyongeza ya mishahara na posho, huku Serikali ikisema haiwezi kutekeleza madai yao kwa sababu haina fedha. Kama habari iliyochapishwa katika gazeti hili leo, wananchi wameonyesha kukerwa na mkanganyiko huo. Ni matumaini yetu kwamba Waziri Mkuu Pinda na Spika Makinda watawajibika kwa kuwaeleza wananchi ukweli, tena ukweli mtupu.
   
   

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #1 2012-02-09 11:04
Laki mbili tu(ksh 10000)?jamani kenya ni zaidi kwani wambuge hulipwa ksh 1000000(Tsh 18000000) kwa mwezi,marupurup u kando!kwa hivyo acheni wale wanone ili wawaundie sheria za kuwauwa.ama?
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner