
| Serikali imlipe fidia mbunge aliyevuliwa nguo gerezani | Send to a friend |
| Thursday, 02 February 2012 21:48 |
MBUNGE wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), juzi alipiga moyo konde na kupata ujasiri wa kula mfupa uliowashinda wananchi wengi, pale alipolieleza Bunge linaloendelea na kikao chake mjini Dodoma jinsi alivyodhalilishwa gerezani kwa kuvuliwa nguo zote na kubaki uchi wa mnyama kabla ya kurushwa kichura.Huku wabunge wakiwa wamepigwa butwaa pengine kwa kutoamini kuwapo kwa uvunjaji wa haki za binadamu kwa kiwango cha kutisha kama hicho katika magereza yetu nchini, mbunge huyo alikomalia hoja yake na kusisitiza kwamba atakuwa mtu wa kwanza kutoa ushahidi popote kuhusu vitendo vya unyanyasaji alivyosema vinafanywa na askari magereza dhidi ya wafungwa, hasa wanawake. Itakumbukwa kwamba mbunge huyo na wenzake 11 walikamatwa wilayani Urambo, mkoani Tabora katikati ya mwaka uliopita baada ya kudaiwa kufanya mkutano wa hadhara bila kibali na hatimaye kupelekwa mahakamani, lakini walikosa dhamana na kusota rumande kwa wiki mbili. Mbunge huyo alitoa kauli hiyo baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki kulieleza Bunge kwamba hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kuwapo kwa mateso na udhalilishaji wa wanawake katika magereza yetu nchini, ingawa alitoa pole na kumuomba radhi kama kweli alifanyiwa vitendo hivyo. Mbunge Sakaya alitoa dukuduku lake hilo wakati akiuliza swali la nyongeza kutokana na swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Mhonga Ruhwanya (Chadema), ambaye alisema askari magereza wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwadhalilisha wafungwa wanawake na kutaka kujua Serikali inawachukulia hatua gani askari magereza wanaofanya udhalilishaji huo. Sakaya aliitaka Serikali kuachana na ‘porojo’ na kusema ushahidi wa namna wanawake wanavyovuliwa nguo anao yeye mwenyewe. Hata hivyo, baada ya ushuhuda wa mbunge huyo, Balozi Kagasheki alitoa maelezo yanayoweza kutafsiriwa kwamba Serikali imekuwa ikijua kuwapo kwa vitendo hivyo pale aliposema Jeshi la Magereza limekuwa likifanya upekuzi kwa ajili ya kujiridhisha kama vitu vya hatari na haramu haviingizwi magerezani. Lazima tukubali kwamba hizi ni tuhuma nzito kwa kigezo chochote kile na swali linalojitokeza hapa ni kwa nini Serikali siyo tu imeshindwa kumlipa mbunge huyo fidia kwa udhalilishaji huo, bali pia imeshindwa kuchunguza tuhuma hizo kwa lengo la kufanya mabadiliko ya kisera na kimuundo katika magereza yetu, ingawa kumekuwapo ushahidi usiotiliwa shaka kwamba vitendo vya udhalilishaji alivyovieleza mbunge huyo vimekuwa jambo la kawaida katika magereza yetu. Wafungwa wengi wanaotoka magerezani wamekuwa wakisimulia jinsi walivyokuwa wakiachwa uchi wa mnyama na kupekuliwa mwili mzima kabla ya kurushwa kichura eti kwa lengo la kuhakikisha hawaingizi gerezani sigara, simu za mkononi na madawa ya kulevya. Mhariri wa gazeti moja la Kiingereza nchini ambaye alitoka gerezani yapata miaka minne iliyopita, aliandika makala ya kusononesha na kueleza jinsi yeye na wenzake wa kiume walivyokuwa wakifanyiwa unyama huo. Tatizo hapa ni Serikali ambayo bado inaendesha magereza kwa kutumia mifumo ya kizamani badala ya mifumo na tekinolojia ya kisasa. Pamoja na kutumia njia za kikatili na za kinyama kuzuia vitu hivyo kuingizwa magerezani, haijiulizi kwa nini bado vitu hivyo vinaendelea kuingizwa. Serikali imeshindwa kugundua kwamba baadhi ya askari magereza ndiyo tatizo kwa sababu, mbali na kufanya biashara hiyo, hupewa rushwa na ndugu wa wafungwa na mahabusu ili wapenyeze vitu hivyo magerezani. Sisi tunadhani kwamba pengine uongozi wa magereza yetu umeona kwamba jawabu pekee la tatizo hilo ni kuendesha unyama huo ambao umechangia kuyafanya magereza kuwa jehanam na mahali pa mateso kwa wafungwa. Matokeo yake ni kwamba badala ya kurekebisha tabia za wafungwa, magereza yamewajengea usugu, chuki na hali ya kukata tamaa ya maisha. Hali hiyo tunadhani imechochewa na walinzi wa amani, ambao ni mahakimu, majaji na mawakili ambao wameshindwa kuyatembelea magereza hayo ili kuhakikisha haki za wafungwa zinalindwa. |



MBUNGE wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), juzi alipiga moyo konde na kupata ujasiri wa kula mfupa uliowashinda wananchi wengi, pale alipolieleza Bunge linaloendelea na kikao chake mjini Dodoma jinsi alivyodhalilishwa gerezani kwa kuvuliwa nguo zote na kubaki uchi wa mnyama kabla ya kurushwa kichura.











Comments