
| Michuano ya Afrika imetufunza umuhimu wa wachezaji vijana | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 09:30 |
|
Timu zilizoingia hatua hiyo ni Ghana, Mali, Zambia, Gabon, Guinea ya Ikweta, Sudan, Tunisia na Ivory Coast, ambapo leo Zambia itacheza na Sudan, Ivory Coast itacheza na Guinea ya Ikweta. Kesho ni Gabon dhidi ya Mali na Ghana ikicheza na Tunisia. Kabla hatua hii ya robo fainali ambayo imebaki na timu nane, timu 16 za mataifa bora Afrika, zilishiriki kuanzia Februari 12 mwaka huu. Zilizoaga mashindano ni Morocco, Botswana, Guinea, Senegal, Angola, Burkina Faso, Niger na Libya. Kwa kawaida, timu inayoshika nafasi ya kwanza katika kila kundi katika mashindano ya kuwania kufuzu ndiyo, hupata tiketi ya kucheza fainali hizo zenye utaratibu wa kufanyika kila baada ya miaka miwili. Lakini kwa mwaka huu kuna mabadiliko, ambayo tutashuhudia tena fanaili za hizo kubwa na pekee kwa aina yake barani Afrika, zikifanyika tena mwakani tofauti na utaratibu wa awali wa kila baada ya miaka miwili. Tanzania imepangwa kuanza kuwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali hizo za Afrika 2013 kwa kucheza na Msumbiji Februari 29, Maputo. Ni dhahiri zimebaki wiki tatu kabla ya mechi hiyo. Kubwa tunaloliona mbele yetu siyo tu kushauri timu iingie mapema kambi kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo, bali aina ya wachezaji watakaochaguliwa kuunda kikosi cha Taifa Stars. Kwa wale wanaofuatilia kwa karibu michuano ya mwaka huu nchini Gabon na Guinea ya Ikweta, watasimama juu ya ukweli wenye ushuhuda wa tosha kwamba safari hii timu nyingi zimewakilishwa na wachezaji vijana. Kusudio letu si kuingilia majukumu ya kocha wa Stars, Jan Poulsen ila tunaamini ataweka mkazo wa uteuzi wa wachezaji vijana zaidi, ambao kimsingi ndio wanaoguswa na kasi ya mabadiliko ya soka la sasa. Ni imani yetu pia kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linafuatilia kwa karibu fainali za mwaka huu kushuhudia aina ya wachezaji wanaoshiriki. Basi ni vyema fursa hiyo ikatumika vizuri na viongozi wa TFF na benchi zima la ufundi Stars kukaa pamoja na kujadili aina ya wachezaji wanaopaswa kutuwakilisha. Si kwa maana ya kuingilia majukumu ya Kocha Poulsen ile kwa lengo la kumshauri kutokana na mifano mbalimbali inayoendelea kuonekana kwenye fainali za mwaka huu. Hatutarajii kuona TFF wakimuingilia Poulsena katika uteuzi wa kikosi chake ila tunaamini watampa ushauri huo wa uteuzi wa wachezaji wengi vijana ili kuunda kikosi chenye kasi mpya. Tunategemea kuona mabadiliko mengi katika uteuzi hasa ukizingatia kuwa Poulsen amekuwa Tanzania tangu Agosti mwaka jana, hivyo tunaamini analielewa soka letu na aina ya wachezaji tulionao.
Ni kwa kuangalia mifano itokananayo na michuano hiyo, ndipo tunapotegemea pia kuwa Kocha Poulsen atakuwa ameshajifunza mengi ambayo yatamsaidia kurahisisha kazi yake. Hatuna sababu ya kujidanganya hata kidogo, ukweli uko wazi ili tuweze kurejea tena kwenye fainali hizo baada ya miaka 32, ni lazima kuwapa vijana nafasi. Huu si wakati tena wa kuchagua wachezaji kwa kigezo cha majina, umaarufu au Usimba na Uyanga kama ambavyo imezoeleka na kuonekana kuwa ni utamaduni katika uteuzi wa Stars. Sababu za kufanya vibaya kwenye michuano ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za mwaka huu, ambazo tunaziangalia kwenye televishen, zilishawekwa mezani kwa ajili ya marekebisho. Tunaamini TFF na benchi la Ufundi la Stars limeshafanya marekebisho hayo na tunatarajia kuona mabadiliko makubwa katika safari ya kusaka tiketi za fainali hizo. |



FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinaendelea kushika kasi nchini Gabon na Guinea ya Ikweta, ambapo sasa zimefikia hatua ya robo fainali.










