
| Wasanii kuweni makini katika kampeni za kisiasa | Send to a friend |
| Saturday, 28 August 2010 10:38 |
Festo PoleaSH UGHULI za kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani zimeanza na wanasiasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama vya siasa nchini wameanza kazi. Wengi wao wamekuwa wakijinadi kwa wapigakura wao wenyewe na wengine kwa kutumia wasanii wa fani mbalimbali kwa lengo la kutoa burudani kwa watu wanaohudhuria mikutano yao ya siasa. Katika mbwembe hizo wasanii hao wa fani mbalimbali zikiwemo maigizo, muziki na uchekeshaji wakitumika kama kichocheo katika kutoa burudani kwa mashabiki ili kutowachosha na maneno yao ya muda mrefu wakijinadi kuomba kura. Wasanii hao kwa wakati huu wa uchaguzi hutumika pia kama sumaku ya kuvuta watu wengi wakubwa kwa wasogo ili kuhudhuria mikutano hiyo na kusikiliza maneno na ahadi za wanasiasa. Mikutano hiyo ya kampeni inapofanyika bila kuwa na wasanii wa aina yoyote imekuwa ikipwaya na kukosa watu au wakijitokeza wanakuwa wachache. Hivyo, kuwepo kwa wasanii katika mikutano hiyo husaidia kuongeza idadi ya watu wanaohudhuria hata kama si wanachama wa chama husika wala wapigakura kwa maana ya umri mdogo, lakini viwanja vimekuwa vikioenekana kufurika watu ambao husikiliza hotuba na maneno ya kisiasa na baadaye burudani au burudani. Baadhi ya wasanii wanaeleza kuwa kabla ya kuanza kwa kampeni walishapata hofa nyingi za kurekodi nyimbo zinazowahusu wanasiasa au wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi huku wengine wakidai kupata ahadi za mialiko mingi. Wengine wamediriki kueleza kuwa wameshapata kianzio cha fedha kwa ajili ya kazi hizo na hivyo walishaanza mazoezi ya maigizo na uimbaji. Hayo yote ni heri kwao, nawaombea wapate hizo kazi na wafanye kazi kwa moyo mmoja hata kama si wanachama hai wa vyama wanavyovifanyia kampeni ilimradi lengo lao liwe ni kujipatia kipato nalo litakamilika kwa kutumia vizuri taaluma zao na kisha kupata pesa za kujikimu kimaisha. Lakini, sijui kama wasanii wamekwishajiuliza kwa nini wakati huu wa kampeni ndiyo wanaonekana kuwa na umuhimu na wanasiasa wote wanawafahamu tena kwa majina halisi? Ni swali ambalo wasanii wetu hawana budi kujiuliza wanapokubali kuwafanyia kampeni wanasiasa . Ninajua baada ya kukamilika kwa uchaguzi na kupata viongozi baadhi yao watakimbilia katika vyombo vya habari na kulalamika kuwa wamedhulumiwa, wametumikishwa bure au hata kuibiwa. Ni kwa sababu hiyo katika kampeni kuna watu wanaojiita mameneja wa kampeni, hao ndio wanaokuwa na posho zikiwamo za wasanii, naamini hao ndio watu wanaoweza kuwatumia vibaya wasanii wetu. Ninawashauri wasanii wetu wahakikishe wamefikia makubaliano ya kikazi kwa kuwekeana mikataba na kukubaliana kwa muda wote wa kampeni wanapofanya kazi ziwe kwa maslahi ya pande zote mbili na wenye kuwasaidia kujiendeleza katika fani na kupata haki zao bila kusumbuliwa. Nakumbuka kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005, wapo wasanii waliotumika na baada ya kumalizika kwa uchaguzi walikimbilia kwenye vyombo vya habari na kulalamika kuwa wamedhulumiwa, wametengwa na malalamiko mengine mengi. Ninawashauri wasanii waamke, wasirudie makosa na yale yaliyotokea mwaka 2005 yasiyotee tena. Ninawaomba watumie majukwaa ya siasa kuwanadi wagombea nao waeleze matatizo yao ili wananchi waweze kuyafahamu na wagombea nao wasaidie kuyatatua kwani muda huu ndiyo malalamiko yanaposikilizwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Ni wazi kuwa kusubiri watetewe bila kujitetea wenyewe na kutambua matatizo yao kamwe hawatofanikiwa na watabaki kulalamika miaka nenda rudi. Mini ni mdau wa fani ya sanaa, ninajua kuwa kuna matatizo mengi yakiwemo ya kukosa soko la uhakika la kuuzia kazi za sanaa ambako utakuta albamu ya msanii wa bongo fleva ambaye ndiye anatumika zaidi katika kampenzi anapata faida ya Sh 200. Labda, wewe kama msanii unayesubiri meneja wako kwenda kuipeleka albamu yako sokoni ndiyo uwe makini na wakati huu wa kampeni ambazo zinaweza kuwamaliza na kuwaondoa katika fani. Hivyo, kwa tathmini yangu ndogo kwa baadhi ya wasanii wa muziki tena wenye majina na hata kwenye filamu ni wakati wa kujiangalia wakati huu wa kampeni ili msije kujuta baadaye. Vinginevyo, kwa wasanii ambao ni wagombea, ninawatakia kila la heri mfanikiwe, lakini kumbuka kampeni hizi zinaweza kuwa kaburi lenu na kuwaondoa katika ajira kama hamtakuwa makini. Festo Polea ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kwa simu namba 0755-625042, email: This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it |
| Last Updated on Saturday, 28 August 2010 12:36 |



Festo Polea









