
| Sekta ya viwanda na kilimo zifungishwe ndoa ya kudumu | Send to a friend |
| Thursday, 02 September 2010 09:43 |
Na Florence MajaniWATU wazima watakuwa wanazikumbuka kauli nyingi ambazo zilikuwa zikielezea na kusisitiza umuhimu wa kilimo: Kauli kama Mvua za kwanza ni za kupandia (1974/75); Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa; Kilimo ni uhai; Kilimo cha kufa na kupona; Siasa ni kilimo na sasa ni Kilimo Kwanza. Lakini pamoja na kauli zote hizi, bado kilimo cha Tanzania hakijakidhi matarajio. Tunalima mazao chekwa ya biashara lakini kila unapopita njiani na madukani, bidhaa zilizozagaa ni za kutoka China, Uganda, Kenya na nchi nyinginezo. Kama kilimo ni uti wa mgongo wa taifa na kama asilimia 80 ya Watanzania ni wa kulima na kama serikali inaamini katika Kilimo Kwanza, sioni kwa nini ukulima uwe kazi ya maskini. Kwa nini hii asilimia 80 wengi wao bado ni maskini? Tatizo nililoligundua ni kuwa sekta za viwanda na kilimo zimepeana mipaka. Ni kama ofisi mbili zilizo na majukumu tofauti ilhali zinapaswa ziwe kama mume na mke wanaotegemeana kwa kila hali. Tukiwa tumeingia katika Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushindani wa masoko ya bidhaa utakuwa mkubwa. Ushindani huu utakuwa ni aibu kwetu kama hatutaweza kufanya juhudi za dhati ili kuwa juu katika uzalishaji wa bidhaa bora kama au kushinda za wenzetu wa nchi wanachama. Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 22.6 tu ya bidhaa za ndani zinazouzwa nje ya nchi. Kwa mwendo tulionao sasa ambao sekta ya viwanda inazidi kushuka kila kukicha, tutashindwa kupiga hatua kiuchumi. Viwanda na kilimo ni sekta mbili ambazo kwa hakika zinahitaji kufungishwa ndoa ili zitumikiane, zisaidiane na zitegemeane. Hii ni kwa sababu, sekta moja inapopewa kipaumbele zaidi, nyingine hudorora na kufa kwa sekta moja ni uchuri kwa nyingine. Mkakati wa Kilimo Kwanza umedhamiria kukiboresha kilimo na kukifanya kuwa cha kisasa yaani kutumia teknolojia ya hali ya juu. Kilimo hicho kitakuwa kinatumia zana kama matrekta, mashine za kuvuna na pembejeo za kilimo za kisasa. Kwa mujibu wa mipango hiyo, viwanda vyetu vina teknolojia ya kuzalisha zana kama hizo? Au tunavyo viwanda vya kuchakata mazao ili kuzalisha bidhaa za kilimo kuliko kuuza mazao ghafi au kushindwa kuyatunza kwa muda mrefu? Inawezekana kabisa kwamba mkakati wa Kilimo Kwanza una maana na nia nzuri, lakini ni vigumu kufanikiwa kama hatutavijengea uwezo viwanda. Tunapoipa kipaumbele sekta ya kilimo na kuiacha ya viwanda ni dhahiri nayo itakufa. Ili kilimo kistawi ni lazima kiwe na zana bora na za kisasa za kilimo. Zana hizo ni kama mbolea, vifaa bora vya kulimia, dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao na mashine bora za kuvunia, kupalilia na kuchakata mazao. Viwanda hupokea malighafi za kilimo kuzalisha bidhaa, kwa hiyo bila bidhaa kiwanda hakina kazi ya kufanya. Uwiano kati ya sekta hizi mbili utatengenezwa kwa kuhakikisha kinakuwepo kiunganishi kikuu ambacho kitaziwezesha kufanya kazi kama ubongo na mwili wa binadamu vinavyofanya kazi kwa pamoja na kumuwezesha binadamu kupumua. Kwanza kabisa, wakulima wanapaswa kuzalisha kwa wingi mazao ya vyakula ili kuwapatia chakula rasilimali watu. Haitakuwa na maana kama wakulima watajikita katika mazao ya biashara pekee kama pamba, katani, tumbaku na sufi wakati wafanyakazi na wakulima hao hao wanakosa chakula. Ni lazima rasilimali watu ipate nguvu ili itumike vyema katika uzalishaji. Inapopata chakula cha kutosha na kushiba kazi zitafanyika kwa ufanisi zaidi. Mara nyingi mazingira ya nguvu kazi yasipotengenezwa, ufanisi huwa mdogo katika utendaji. Jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa katika kuweka sawa mshikamano kati ya viwanda na kilimo ni kuhakikisha kuwa viwanda vyetu vinazalisha zana bora na za kisasa zaidi za kilimo. Wakulima hawataweza kuzalisha kwa wingi kama wanatumia jembe la mkono, tena bila mbolea wala dawa za kuua wadudu. Kilimo Kwanza hakitakuwa na manufaa kwa uchumi ikiwa hakitamsaidia mkulima mdogo kwa kumuwezesha kupata vifaa bora na vya kisasa. Kauli hii itakuwa ni wimbo usio na vina wala mizani kwa asilimia 80 ya wakulima ambao ndiyo tunaowategemea kwa uzalishaji kutoka katika sekta hiyo. Kilimo Kwanza kimuwezeshe mkulima kwa kumpa mbolea ya ruzuku na zana bora za kisasa ili aweze kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya taifa lake na kwa ajili ya mauzo kwa soko la nje. Mkulima ataweza kuzalisha kwa kiasi kikubwa iwapo viwanda vitazalisha zana bora na za kisasa kwa za kilimo. Ufike wakati tutumie jembe la mkono kwa kupenda, au kwa ajili ya bustani za maua za nyumbani lakini siyo kwa mashamba ya mazao ya biashara. Nchi nyingi maskini ikiwemo Tanzania zipo katika kundi la kuzalisha isichotumia na kutumia isichozalisha. Hii ni kwa sababu, malighafi zetu nyingi hasa za biashara, zinasafirishwa na kwenda kutengenezwa katika viwanda vya nje na baadaye tunauziwa wenyewe. Kilimo Kwanza kitafanikiwa vipi ikiwa viwanda bado vina uzalishaji mbovu ambao hautuwezeshi kufanya biashara zenye faida kimataifa? Ina maana tutegemee kununua mashine za kilimo kutoka nje wakati tungeweza kutengeneza zana hizo katika viwanda vyetu? Sekta ya kilimo na viwanda ziende sambamba katika utendaji wake, tusiweke nguvu katika kilimo pekee huku tukiwa hatuna viwanda vyenye teknolojia ya hali ya juu. Serikali haina budi kutia nguvu katika uwekezaji wa viwanda vya kilimo kama kweli imedhamiria kuwakomboa wakulima. 0715 773366 |
| Last Updated on Thursday, 02 September 2010 10:00 |



Na Florence Majani









