MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Maoni ya Mhariri Pongezi JWTZ, lakini rekebisha mambo haya
BOOKMARK THIS PAGE
Pongezi JWTZ, lakini rekebisha mambo haya  Send to a friend
Thursday, 02 September 2010 21:54

Maadhimisho ya kutimiza miaka 46 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), yalimalizika juzi kwa Serikali kuahidi kwamba itaendelea kuliimarisha jeshi hilo katika kila idara. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, alitoa hotuba katika kilele cha maadhimisho hayo na kuwahakikishia Watanzania kwamba nchi yetu na mipaka yake viko salama.
     
Tunapenda kulipongeza jeshi letu kwa kutimiza miaka 46 na kwa kuonyesha utii na uaminifu mkubwa kwa serikali zetu na watu wake tangu lilipoasisiwa  mwaka 1964. Miaka 46 siyo mingi sana katika maisha ya binadamu, lakini kwa upande wa maisha ya jeshi, miaka hiyo ni mingi mno kutokana na misukosuko inayozikabili nchi nyingi duniani kila kukicha. Jeshi letu hilo muda wote limekuwa imara na limehakikisha kwamba ulinzi wa mipaka yetu daima unapewa kipaumbele.

Ndiyo maana tunasema jeshi hilo linastahili pongezi za dhati, kwani tumeona majeshi katika nchi kadhaa, zikiwemo za bara hili la Afrika, zikiweka kando wajibu wake wa kulinda mipaka ya nchi zao, na badala yake zinabadilisha mamlaka za nchi kwa kutumia mitutu ya bunduki. Kama alivyosema Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, wakati wa maadhimisho hayo, jeshi hilo linaendelea kutimiza majukumu yake kwa moyo, uzalendo na uadilifu mkubwa, pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi.

Ni jambo la kutia moyo pia kwamba jeshi hilo sasa limepanua wigo wake katika kulinda mipaka yetu kwa kufanya operesheni dhidi ya madawa ya kulevya, ugaidi, uharamia na usafirishaji haramu wa binadamu. Jenerali Mwamunyange alisema kwamba pamoja na eneo la bahari kuwa salama, imechukuliwa tahadhari kubwa kwa kuwa vyanzo vya maovu hayo havijadhibitiwa katika nchi za wenzetu.

 Pamoja na uzito wa majukumu hayo yanayoendelea  kulikabili jeshi letu, bado tumekuwa tukishuhudia likijiweka karibu na wananchi wakati wa maafa na katika nyanja za elimu, matibabu na nyingine nyingi, tofauti na mataifa mengine mengi ambayo majeshi yake hujitenga na wananchi mithili ya majeshi ya kukodiwa. Tunadhani kwamba waasisi wa nchi yetu walikuwa sawa kabisa kusema jeshi letu hilo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

 Lakini pamoja na pongezi zetu nyingi kwa jeshi letu hilo, tunadhani kwamba yapo mambo ambayo linapaswa kuyarekebisha  iwapo linataka kupata ufanisi wa kiwango cha juu na kuendelea kupendwa kama jeshi la wananchi. Moja ya mambo ya kutilia mkazo ni suala la mahusiano na wananchi, kwani baadhi ya askari wamekuwa wakiwanyanyasa raia kwa kuwapa vipigo pasipo kuchukuliwa hatua.

Katika baadhi ya sehemu, wananchi wamezibiwa njia au kufutiwa vituo vya mabasi vilivyo kwenye barabara za umma kwa madai kwamba zinapita katika sehemu za jeshi. Moja ya mifano hai ni njia panda ya kwenda Kawe, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam, ambapo wananchi waendao Kawe wanapata mateso makubwa kwa kutembea mwendo mrefu -- hasa wanawake wakati wa usiku -- kwa sababu mabasi hayaruhusiwi kupandisha au kuteremsha abiria sehemu hiyo.

Kwa upande wa ufanisi, jeshi letu sasa lijikite zaidi katika kuajiri na kutoa mafunzo kwa vijana wasomi katika nyanja zote kwa sababu karne tuliyomo hivi sasa ya sayansi na tekinolojia inazo changamoto zisizohitaji majibu rahisi. Kwa mfano, tumeshangazwa na kitendo cha jeshi letu hivi majuzi kutangaza ajira za madereva na kusema kwamba wanahitajika hata wenye elimu ya darasa la saba, wakati wenye elimu ya sekondari na vyuo vikuu wamejaa mitaani maelfu kwa maelfu bila ajira. Lazima tukubali kwamba elimu ya msingi kwa sasa siyo tu haina nafasi katika jeshi letu, bali pia katika mfumo mzima wa serikali za mitaa na Serikali Kuu.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner