MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Uchambuzi na Maoni Ni halali kwa Mererani, kilipo kitovu cha Tanzanite kuwa hivi?
BOOKMARK THIS PAGE
Ni halali kwa Mererani, kilipo kitovu cha Tanzanite kuwa hivi?  Send to a friend
Thursday, 22 December 2011 15:16

 Na Florence Majani
Siku nilipofika katika mji wa Mererani,  mkoani Arusha, nilishangazwa na mandhari niliyoikuta hapo. Uchakavu wa majengo, miundombinu duni na hata wakazi wake nao hawakuonekana kufurahia maisha.


Kila unayekutana naye basi atakuomba fedha kidogo angalau akapate mlo, wengine wanapanga mikakati ya kuukimbia mji huu na baadhi wameshaondoka. Nilipohoji, kulikoni niliambiwa kuwa, hali ya maisha Mererani ni mbaya mno na inazidi kuwa mbaya.


 Zamani ungelikuta wakazi wa hapa wakiwa katika shamrashamra. Aidha katika kumbi za starehe, wakikimbiza pikipiki zao, wakinunua magari na kujenga nyumba ya kifahari. Lakini sasa hivi wamebaki wakitazamana tu! Rasilimali ya kwao wenyewe  imewatumbukia nyongo.


 Lakini Mererani ndipo kilipo kitovu cha madini ya Tanzanite. Kito cha thamani ambacho hakipatikani kwingine kokote zaidi ya hapa. Iweje leo hii, Mererani iwe kama ilivyo.  Iweje watu wake wawe maskini wa kutupwa?
Nikahoji, madini yanayochimbwa hapa yanamnufaisha nani? Jibu nililolipata ni kuwa, “wawekezaji wametuvamia” wamechukua moja ya mgodi mkubwa unaotoa madini kwa wingi na wanavuna tani kwa tani za Tanzanite na kuzipeleka  nchi za nje.


 Kilio cha wakazi wa hapa ni kuwa, kwa sasa hawayapati madini kama awali. Ispokuwa wakiwa wameajiriwa katika kampuni ya uchimbaji inayomilikiwa na wawekezaji. Lakini hata ukiajiriwa hapo, upatacho ni kidogo mno na hakikunufaishi.


 Inasemekana kuwa, sheria ya uwekezaji Tanzania, ndiyo inayozidi kutudidimiza kwani,katika kila shilingi 100, muwekezaji anapata sh 97 na nchi inapata sh 3. Kweli kwa mwendo huu tutaondokana na umaskini?
Inakadiriwa kuwa madini ya Tanzanite  huingiza mapato yanayofikia dola za Kimarekani milioni  20 kwa mwaka hapa nchini,  lakini katika soko la dunia takwimu zinaonyesha kuwa mauzo ya Tanzanite ni dola milioni 500 za Kimarekani; kiasi ambacho ni kikubwa mno ukilinganisha mauzo ya ndani.


Na je, sheria inasemaje kuhusu kuwaajiri wazawa?Inasemekana kuwa, katika kampuni ya  Tanzanite One iliyopo kitalu C,inayomilikiwa nakampuni ya Afrika Kusini, wazungu ndiyo asilimia 70 ya wafanyakazi wakati wazawa ni wachache mno.
 Si hivyo tu bali madini hayo yote husafirishwa na kwenda kuuzwa nje ya nchi huku Tanzania tukibaki kuwa wamiliki wa mashimo tu.
Wawekezaji wetu wamekuwa si wabia wa maendeleo tena, bali ni waporaji , wakichota tani kwa tani za Tanzanite na kuwaacha wazawa wakiogelea katika kina cha umaskini.
 Mererani ya leo si ile ya jana, leo hii waliokuwa na mali, wakifanya biashara, wakijenga nyumba za kifahari wamebaki na majina yao tu, kwani hivi sasa mdudu mnyonyaji kawaingilia.
 Mdudu huyu anayekuja kwa jina la mwekezaji anazidi kuwatia hofu wakazi hawa na watanzania wengine wachimbaji kwa ujumla kwani ana mkataba wa muda mrefu hapa nchini.
 Anazoa madini yote na kuyapaleka nchi za nje. Na  linalotia uchungu zaidi ni kuwa, kampuni ya Tanzanite One imepewa eneo ambalo linatoa madini  kwa wingi mno kuliko maeneo mengine yenye madini.  Hivyo inakomba na kuhakikisha imeyamaliza madini hayo na kuondoka ikituachia mashimo.
 Wakati huo huo nchi za Kenya na Thailand ndizo zinazoongoza katika uuzaji wa madini duniani lakini sisi ambao tunazalisha tunashika mkia?
Sera  ya uwekezaji inasema kuwa, wawekezaji  hawana budi kuyaboresha mazingira wanayofanyia kazi, kuhakikisha miundombinu inakuwa imara, maji, huduma za afya na hata elimu ikiwezekana. Lakini kwa Mererani hali haipo hivyo. Ni zaidi  ya umaskini.
Kiwango cha elimu bado kingali kinashuka, huduma za afya zipo mbali, ukulima nao bado ni dhaifu na hata ufugaji  si ule wa kuleta tija.
Wachimbaji wadogo wadogo  wanaukimbia mji wao. Wanaona ni bora wakatafute namna nyingine ya maisha kuliko kujilisha upepo ndani ya mji huu, ambao baraka yake imegeuka kuwa laana.
Machungu ya wakazi wa Mererani ni sawa na yale ya watanzania wengine, yale ya kumiliki mali na utajiri  lakini mmiliki ukashindwa kuufaidi utajiri huo. Inauma mno.
Ni sawa na kumiliki nyumba, kisha nyumba hiyo ukaipangisha, lakini mpangaji akakulipa kodi kidogo mno ambayo haiwezi kukufanya ujenge nyumba nyingine.
Ilitegemewa kuwa, Mererani kwa kuwa ndipo kitovu cha madini hayo, basi ungekuwa ni mji wenye hadhi yake. Mji wenye hoteli za kifahari, miundombinu bora, mji usiokuwa na wasiwasi wa kupata maji wala umeme.
Lakini kwa nini taifa limefikia hapa? Ilitegemewa kuwa  tunapozidi kukomaa basi tungetafuta mbinu za kujitegemea zaidi na kuimarisha uchumi wetu. Lakini sivyo ilivyo.
 Badala yake, mikataba mibovu inayotiwa saini na viongozi wetu inayowapa kipaumbele wawekezaji inamfanya maskini azidi kuteketezwa na umaskini wake.
 Ni sawa  na mchimba kisima ambaye baada ya kumaliza kuchimba anakosa wa kumshika mkono na kumtoa nje, je ataweza kupata manufaa ya uchimbaji huo?
 Kwa nini viongozi wetu wanashindwa kuchukua hatua zitakazoipa ahueni Mererani? Kwa nini wazawa waachwe wataabike namna hii ilhali wageni wakijizolea madini katika ndege  na kuyapeka kwao?
Hali hii si ya hapa Mererani pekee, bali hata kule Geita, Bulyankulu, Mahenge na Mwadui. Kote kumesheheni wawekezaji wanaokula bila kusaza.
Wakazi wa Mererani wanahitaji elimu, miundombinu, vituo vya afya kutokana na madini haya ambayo yamebarikiwa kuwepo,walipo.
Ni wizi wa kimachomacho kwa wakazi wa hapa kutonufaika na rasilimali yao.
 Serikali ilitupie macho swala hili tena na tena. Ninaamini ipo nafasi maalum kuzimu kwa  viongozi wanaothamini wageni  na matumbo yao, huku wakimuacha mtanzania akigumia maumivu ya uchungu.
 Mungu ibariki Tanzania, wabariki viongozi waadilifu pekee. Ila wale viongozi wala rushwa …
0715 773366


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #2 2011-12-23 20:15
NI vigumu kuamini hali hii:
Hata sisi baadhi ya wananchi tunaijua mererani au kuzaliwa au kutemblea mji huo mdogo duniani maarufu sana!! kwa kuzalisha hicho kito maarufu duniani, hata miundo mbinu tu inatosha kuwa ushahidi, zamani mji ulikuwa maarufu kwa jina kama Zaire maana wanachi walikuwa wana jiweza.
Sasa wizara husika ilitambue hilo maana ni aibu tupu, vipi kito hicho kipatikane pale dunia nzima na wao wachukue zaidi kivipi?
Quote
 
 
+1 #1 2011-12-22 19:41
Viongozi wasio wabinfsi.Hawatakubari hata wawekezaji kwanye maeneo ya mali ya sili.Nyelele kwani hakujua kuna Madini au Mbuga za wanyama.sasa hivi tulio wakarisha wanachukua mali na uhai wa vijana wetu wasio na elimu wanao jitafutia kwa ugumu.Vijana wetu hutafuta maeneo kuanza kuchimba kimasikini waanza kuata tu selikali inatafuta mwekezaji na vijana kufukuzwa kwa lisasi.Haitokei tena kupata kiongozi kama Nyerere.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner