MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Uchambuzi na Maoni Twiga Stars inahitaji sapoti yetu wote
BOOKMARK THIS PAGE
Twiga Stars inahitaji sapoti yetu wote  Send to a friend
Friday, 06 January 2012 19:45

Jessca Nangawe
TIMU ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), iko kwenye maandalizi ya mbio za kusaka tiketi tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake (AWC).

Shukrani kwa Jeshi la kujenga Taifa, JKT kwa msaada wa kufadhili kambi ya timu hiyo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kudai haina pesa za kuihudumia timu hiyo.

Ikiwa chini ya Kocha Boniface Mkwasa Stars ina inaendelea kujifua kwa nguvu ili iweze kufanya vizuri katika mechi za awali kufuzu michuano hiyo.

TFF ilisema kiasi cha Sh. 50milioni zilihitajika kama sehemu ya maandalizi ya timu hiyo, ikiwa ni pamoja na usafiri na posho za wachezaji na viongozi.

Twiga Stars itaondoka Januari 11 tayari kwa mechi ya kwanza mjini Windhoek, Namibia Januari 14 kabla ya kucheza mechi ya marudiano Januari 29 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kikosi hicho kinaundwa na nyota wanaocheza soka nyumbani toka timu za Uzuri Queens, Sayari, Mndela na nyingine zinazoshiriki ligi mbalimbali za TFF.

Kwa kifupi maandalizi ya timu hiyo si mazuri ukilinganisha na ukubwa wa mashindano wanayokwenda kushiriki na hili linawatia shaka mashabiki wa soka nchini.

Naamini kukosekana kwa maandalizi mazuri inaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa timu hii kusonga mbele. Sisemi haya kwa lengo la kuwavunja moyo wachezaji, lakini ni changamoto iliyowazi na kila mdau wa soka anafahamu.

Timu zetu zote zinazoshiriki mashindano ya kimataifa zimekuwa na tatizo la kukosa maandalizi mazuri na ndio maana hazifiki mbali kwenye michuano ya kimataifa.

Twiga inaweza kufanya vizuri kama wachezaji watajituma na kucheza kwa bidii pamoja na maandalizi ya muda mfupi waliyopata kabla ya mashindano hayo kuanza.

Ikumbukwe kwamba, Twiga ndiyo pekee iliyoweza kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, na iliweza kufanya hivyo katika mazingira magumu ya kukosa maandalizi mazuri.

Ni Twiga ambayo mwaka juzi ilicheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Afrika Kusini na Julai mwaka jana ilikuwa kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) nchini Zimbabwe na kushika nafasi ya tatu.

Aidha, Septemba mwaka jana ilishiriki michezo ya Afrika (All African Games- AAG) ambako nako haikufanya vibaya.

Katika mazingira magumu kama haya ya maandalizi, bado timu hiyo iliweza kufanya vizuri kwenye michuano hiyo iliyoshirikisha timu ambazo zilikuwa na maandalizi mazuri.

Kama Twiga Stars ingekuwa inapewa maandalizi mazuri kama timu ya wanaume, Taifa Stars, nina hakika ingeweza kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya kimataifa.

Katika kipindi hiki ambacho TFF inakabiliwa na ukata mkubwa, ni vyema Watanzania wakafungua macho na kuipa sapoti Twiga ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano yaliyo mbele.

Naamini kuna wadau wengi wana uwezo wa kuichangia timu kwa hali na mali ili iweze kufanya vizuri. Timu iliyoandaliwa vizuri ndiyo yenye nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano.

Pamoja na TFF kukabiliwa na 'njaa', lakini bado hawana sababu ya kukata tamaa katika maandalizi ya timu hiyo ambayo hakika inaweza kufanya vizuri tofauti na mawazo ya watu wengi.

Misaada na ufadhili kwa timu hiyo ni kama deni kwa wachezaji, ambao hawatapenda kuona watu waliochangia kufanikisha wao kushiriki michuano hiyo wanawangusha kwa kufanya vibaya kwenye mashindano.

Huu si wakati tena wakunyosheana vidole na kumtafuta wa kulaumiwa kutokana ukosefu wa fedha za maandalizi kwa timu hiyo, bali wadau watumie fursa hiyo kuhakikisha timu inatapa mahitaji yote ya msingi kuwawezesha kushiriki.

Tunafahamu hali ya maisha ilivyo ngumu wakati huu, lakini pamoja na hali hiyo bado tuna jukumu la kuhakikisha maisha yanakwenda mbele na siyo kurudi nyuma.

TFF ina mamlaka ya kusimamia soka na ina jukumu la kuziandaa timu za taifa, hata hivyo ukweli ni kwamba mzigo huu haupaswi kuwa wa kwao pekee bali wadau wote wapenda michezo.

Ikumbukwe, timu za Taifa zinapofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, heshima siyo ya TFF pekee bali Watanzania wote hivyo kwa hali hiyo ni tunapaswa kuiunga mkono.

Tumeshuhudia mara kadhaa timu ya Taifa ya wanaume ikihudumiwa kwa gharama nyingi lakini bado imeshindwa kufanya vizuri kwenye mashindano kulinganisha na Twiga.

Naunga na TFF katika kuwashawishi wadau mbalimbali wa michezo nchini kujitokeza kuisaidia Twiga ili safari ya kusaka tiketi ya kucheza fainali hizo iwe yenye mafanikio.

Naamini muda bado tunao na vizuri tukachukua fursa hiyo kujiona kama tuna jukumu la kuchangia maendeleo ya michezo nchini na kwa kuanzia tuitupie macho Twiga Stars katika safari yao.

Ningependa kumaliza kwa kuwapongeza wadau wote ambao wameonyesha muitiko wa kuisaidia timu hiyo katika safari ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Jessca Nangawe
This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner