
| Hili la Basena ni uzembe wa TFF, Uhamiaji na Simba | Send to a friend |
| Monday, 09 January 2012 10:34 |
|
HIVI karibuni, Shirikisho la Kandanda nchini (TFF) kupitia kamati yake ya Sheria, Maadili na Hadhi ya wachezaji ilitoa maamuzi ya mgogoro wa malipo kati ya aliyekuwa kocha wa Simba, Moses Basena na uongozi wa klabu hiyo. Katika maamuzi hayo, TFF ilisema kuwa Basena alifanya kazi nchini kinyume cha sheria kutokana na kutokuwa na kibali cha kufanyia kazi kutoka Idara ya Uhamiaji nchini pamoja na kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo. Mbali ya kauli hiyo, TFF ilitangaza kujitoa rasmi katika sakata hilo na kurudisha mgogoro huo kwa klabu ya Simba ili ione itafanya nini katika malipo ya fidia kwa kocha huyo ambaye alikaa nchini si chini ya miezi nane kati ya miaka miwili ya mkataba wake. Wakati TFF inatoa maamuzi hayo, uongozi wa Simba kupitia msemaji wake ulitangaza kuwa suala la Basena wamelifunga rasmi na kumfanya kocha huyo kutangaza kutafuta haki yake katika shirikisho la Kandanda Afrika (CAF) na dunia, Fifa. Suala la Basena linatakiwa kuchukuliwa kwa umakini zaidi vinginevyo linaweza kuliweka soka letu katika aibu kubwa katika medani ya kimataifa mbali ya hapa nyumbani. Umakini wake unatakiwa hasa kwa TFF na Simba kuhakikisha kuwa kocha huyo analipwa stahiki zake kwani suala la yeye kufanya kazi nchini halina ubishi kwa wadau wa soka na hata Shirikisho la Kandanda Afrika, CAF. Ikumbukwe kuwa Basena ameiongoza Simba katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara hatua ya mzunguko wa kwanza na mechi za kufuzu za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo (DRC). Kimsingi kocha huyo alikuwa halali kukaa katika benchi la ufundi la timu hiyo akiwa kocha mkuu chini ya usimamizi wa TFF na CAF katika mechi za Ligi na kimataifa. Kauli ya TFF imetoa maswali mengi sana kuhusiana na uhalali wa kocha huyo na hapo ndipo wadau wengi wa soka wanatia mashaka. Moja ya swali kubwa ni kwa nini TFF ilimpa mwanya Basena kuongoza Simba katika mechi za Kimataifa na za Ligi Kuu huku wakijua kuwa hana kibali cha kufanyia kazi. Mbali ya swali hilo, Idara ya Uhamiaji ilikuwa wapi kwa kipindi si chini ya miezi nane kutomchukulia hatua za kufanyakazi kinyume cha sheria hapa nchini. Hoja nyingine ambayo inawabana TFF na Idara ya Uhamiaji ni suala kocha mkuu wa Yanga, Kostadin Papic aliambiwa haruhusiwi kukaa katika benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma kutokana na kukosa kibalicha cha kufanyia kazi. Kocha huyo alilazimika kukaa kwenye jukwaa la watazamaji, kwa Basena ilikuwa vipi? Ukilichunguza kwa umakini suala hilo, lawama zinabaki kwa TFF, Uhamiaji na Simba kwa kutokuwa makini katika utendaji wao wa kazi. TFF inalaumiwa kwa kutotimizika majukumu yake kwa Basena kwa mujibu wa sheria kwa makocha wanaofundisha ligi kuu ya Tanzania Bara. Kila timu inatakiwa kuwasilisha vyeti vya makocha wake kwa Idara ya Ufundi ya TFF kwa ajili ya kukaguliwa kama anafaa kukaa katika bechi la ufundi la timu hiyo kwa mujibu wa sifa zilizowekwa. Kocha anayetakiwa kuifundisha timu ya Ligi Kuu anatakiwa kuwa na cheti pevu (advance Certificate) kwa mujibu wa Sheria za TFF. Naweza kusema kuwa TFF ilimpendelea Basena kwa kumwacha kufundisha katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara bila kuwasilisha cheti chake. Kuna uzembe uliofanyika mpaka kocha huyo kuongoza Simba kwa muda mrefu na baada ya kuingia katika matatizo, aliamua kuwasilisha vyeti vyake. Inatakiwa kwa TFF kuweka msisitizo kwa sheria hiyo na kuepuka ya Basena kwani inatia aibu soka letu na Idara ya Uhamiaji ambayo inatakiwa kutoa kibali kwa kocha baada ya kupata barua ya TFF. Kwa upande wa Simba, nayo inaingia katika lawama hizi kutokana na kukiuka sheria za ajira na kulitia aibu Taifa na hasa Idara ya Uhamiaji. Inaonekana Simba ilimuamini sana Basena kwa kumsainisha mkataba bila kuona vyeti vyake na kuchukulia maelezo ya CV kama ndicho kigezo chao. Simba pamoja na kuongozwa na wasomi, walishindwa kujua kuwa CV mara nyingi huwa inaambatana na vyeti husika vya muombaji wa kazi. Je kuamini CV kuwa kocha ana digree ya fani hiyo huku akiwa na Diploma ni sahihi? Uongozi wa Simba chini ya Mbunge, Alhaji Ismail Aden Rage na wasomi wengine kama akina Geofrey Nyange Kaburu na Katibu Mkuu, Evodius Mtawala wanatakiwa kuwa makini sana katika kazi zao. Walichokifanya kwa kocha wao mkuu wa sasa, Circkovic Milovan ndiyo walitakiwa kukifanya wakati wa kumuajiri Basena. Uhamiaji wao wanaingia katika lawama kutokana na kumwacha Basena kufanya kazi nchini kinyume cha sheria ikiwa wao ndiyo waliopewa mamlaka kisheria kuwakamata raia wote wa kigeni wanaoishi hapa nchini bila ya kufuata sheria. Uhamiaji ilimuacha Basena kwa kipindi chote hicho mbali ya kujulikana wazi wazi kuwa anafanyakazi wapi na kupatikana kirahisi, lakini walikuwa kimya. Je ni watu wangapi ambao hawajulikani kama Basena wanaishi nchini ikiwa kwa Basena aliishi kwa ëkutanuaí bila woga? Wanatakiwa kuwa makini katika utendaji wao wa kazi. Kwa suala la Basena hawawezi kukwepa lawama kutokana na uzoefu wao katika masuala ya kandanda na elimu zao kwa ujumla. Ni jukumu la TFF na Simba kuhakikisha kuwa suala la Basena linashugulikiwa haraka zaidi kabla ya kocha huyo kuwasilisha hoja zake CAF na Fifa na kutuumbua. |














