
| Kudhalilika kwa mwanamke kunatokana na mienendo yake | Send to a friend |
| Friday, 13 January 2012 10:19 |
|
Na Florence Majani Lakini, pia wengi wao walikiri kuwa baadhi ya wanawake wenyewe wamekuwa wakichangia katika kudhalilishwa kwao. Imebainika kuwa, wanawake hali kadhalika ni miongoni mwa wale wanaotumia lugha chafu mno, wakitumia viungo vyao wenyewe kama silaha unapotokea ugomvi. Kwa mfano, msomaji Aggrey Nguni wa Morogoro anabainisha kuwa wanawake mjini hapo ndio vinara wa kutukana tusi lile… linalotaja kiungo cha mzazi mwanamke. Jambo hili ni la kweli, kwani siku mbili zilizopita nilimshuhudia msichana mmoja akimrushia utingo matusi yale yale yanayotaja viungo vyake mwenyewe baada ya kutokea kutokuelewana baina yao kuhusu nauli. Kwa muda mrefu sasa wanawake wamekuwa wakililia haki na usawa. Lakini, je, wamekuwa wakiishi katika mazingira yanayostahili watu kuwapa haki hizo na usawa? Au, hawazifahamu ni haki gani wanazozililia na wajibu upi wanaopaswa kutenda katika vita hii? Usawa huu si katika nafasi za viti maalum bungeni, katika siasa na katika elimu pekee bali ni pamoja na kuhakikisha mwanamke anakuwa chombo cha thamani katika jamii badala ya kugeuka tusi. Na ili mwanamke awe chombo cha thamani yeye mwenyewe anatakiwa ajithamini kwanza. Ajithamini kwa kutenda maadili yanayokubalika katika jamii. Anapoutaka usawa, basi asimame katika nafasi ambayo hali halisi ya matendo yake itatoa taswira ya ‘yeye ni nani’ . Ili hata utakapopaza sauti yako, watu wataisikia na kuifanyia kazi. Kwa mfano, unapovaa mavazi yasiyo na heshima mbele ya jamii, yanayoacha sehemu kubwa ya mwili wako mtupu, unategemea utaheshimika kweli? Ni nani atakuheshimu iwapo wewe mwenyewe hujiheshimu? Kila mtu atakuona una upungufu fulani na hata inapotokea nafasi katika ofisi yako, watu wataona hustahili nafasi hiyo kwa sababu mavazi yako yanakupa tafsiri mbaya. Mfano mwingine ni katika bendi zetu za muziki siku hizi, wanaume wanenguaji watavaa mavazi ya kawaida, lakini wanawake watajibana na kuacha robo tatu ya mwili nje. Ni lipi linalowanyima nafasi ya kunengua iwapo watavaa mavazi ya kawaida yasiyowaacha watupu? Thamani ya mtu huanzia kwake (mtu) mwenyewe, mazungumzo yako, upeo wako, matendo yako, na hata mavazi yako. Mwanamke mwenyewe unapoibuka na kutukana matusi hadharani ukiainisha kiungo chako mwenyewe, unategemea nini hasa? Unategemea jinsia ya kiume itabadilisha tusi hilo na kuweka kiungo cha kiume? La hasha, hawatabadilisha bali itaendelea kuwa hivyo hivyo. Wanawake wenzangu tutaendelea kudhalilika kwa kuwa, hatuko mstari wa mbele kukemea na badala yake tunaongeza mafuta ya taa katika moto uwakao kutokana na baadhi ya matendo yetu. Napenda kusema kuwa, siwaungi mkono vijana na wengine wanaowashika sehemu nyeti wasichana katika maeneo kama ya masokoni, iwe Buguruni, Ilala, Tandale, Manzese na kadhalika,lakini ni nadra sana kumkuta mwanamke aliyevaa kiheshima -akipigiwa mbinja au kudhalilishwa kwa kushikwashikwa na vijana hawa. Inasikitisha kuona mwanamke mwenyewe anatoa lugha chafu akihusisha kiungo nyeti cha mwili wake. Jamii itashindwa kumwelewa mtu huyu iwapo ana akili timamu au ana upungufu fulani. Ni sawa na wale wazazi wanaowatukana watoto wao, ‘mbwa wewe” na wanasahau ya kuwa, kama mtoto ni mbwa, basi hata mzazi ataitwa ‘mama mbwa au baba mbwa’ Iweje mtu achochee mwili wake uwe sehemu ya matukano? Hii ni aibu na kujipalia makaa ya moto vichwani mwetu. Lakini, tabia hii si kwa wanawake wa mitaani tu, hata baadhi ya waimbaji wetu, ambao walipaswa kuwa kioo cha jamii, mashairi yao yanamchora mwanamke kama mtu mwenye hulka ya kugombania wanaume. Anayezipa baraka ndoa za mitala na kuzipapatikia. Baadhi ya nyimbo zetu zikiwamo za taarabu naonyesha dhahiri kuwa tunaridhia kuolewa katika mafungu tena kwa kupigana vikumbo. Kwa mfano siku za hivi karibuni kimezuka kikundi cha ‘kanga moko moko’, wanawake wanafanya matendo ya aibu na kuishusha thamani yao kwa kiasi kikubwa. Wanacheza katika mtindo ambao unachochea vitendo vya ngono na ni fedheha kubwa kwao wenyewe. Heshima inaanza na wewe. Pasipo wanawake kujithamini na kujiheshimu hakuna atakayekuheshimu, hata watoto wako nyumbani ukiwa na mienendo ya ajabu ajabu basi nao watapunguza uaminifu kwako. Kuna wakati fulani mke wa Rais Kikwete, Mama Salma aliwahi kutoa rai hii na kuwaasa wanawake kujithamini. Mila zinazomdhalilisha na kumdunisha mwanamke, kama vile, tohara, watoto wa kike kutopelekwa shule, ni mbaya na hatuna budi kuzipiga vita kali. Lakini ukiangalia kwa undani, utawakuta wanawake wamejisahau na kufanya matendo mengine yanayoshusha utu wao. Laiti kama wanawake wangejua thamani waliyo nayo na wakaitumia vyema basi taifa hili lingeimarika zaidi kupitia wao. Baadhi ya wanawake waliosimama imara kama Helen Sirleaf Johnson, Rais wa Liberia, Dk Asha Rose Migiro aliyeko Umoja wa Mataifa kutoka hapa Tanzania, Wangari Maathai (hayati) , mshindi wa tuzo ya Nobel kutoka Kenya, walitambua lulu walizonazo. Walijithamini, wakajiheshimu na wakaitumia elimu yao kuwajibika vyema katika jamii. Walitumia nguvu walizojaliwa na Mungu na wakayaleta mapinduzi ya jinsia, uchumi na siasa Afrika. Hakuna wakulibadilisha hili zaidi ya wanawake wenyewe, endapo watabadilisha mienendo yao. |















Comments