|
KWA mara nyingine tena, Jumamosi iliyopita nilipata bahati ya kuhudhuria pambano la ndondi lililokuwa linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ndondi nchini kote, kati ya Francis Cheka wa Morogoro na Karama Nyilawila wa Dar es Salaam.
Pambano hilo lilifanyika katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ikiwa kama ni uwanja wa nyumbani wa kujidai wa Cheka. Kama ilivyo ada katika mapambano ya ndondi, pambano hilo lilikuwa limejenga mvuto mkubwa kwa mashabiki na kwa vyombo vya habari nchini kote. Hasa kwa nyakati hizi ambazo bondia Cheka anapopigana na mabondia maarufu wa jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya pambano hilo, Nyilawila alikubali kuuvua ubingwa wa dunia wa ngumi za kulipwa uzito wa kati wa WBF, ili acheze pambano la kirafiki dhidi ya Cheka kwa vile aliahidiwa fedha taslim Sh7milioni. Pamoja na mbwembwe nyingi ambazo Nyilawila alizitoa katika vyombo vya habari kabla ya pambano hilo, bado pambano hili lilikuwa kama mapambano mengi yaliyopoteza ladha na utamu kwa mashabiki.
Mashabiki waliojazana Uwanja wa Jamhuri walitarajia kushuhudia ngumi kali zikirushwa na mabondia wote wawili hasa kufuatia tambo na mbwembwe za kila aina walizozitoa kuelekea pambano hilo.
Lakini kinyume na matarajio hayo, mashabiki waliendelea kuwa watumwa wa kushuhudia ngumi zilizokosa ladha, utamu na ushindani toka kwa mabondia hao waliooneka kama walikuwa kwenye mzaha.
Wanamasumbwi hao walikuwa wakizichapa kama vile pambano lao halikuwa na kiingilio kutoka kwa mashabiki ambao baadhi walisafiri kutoka Dar es Salaam na Pwani. Waliligeuza kama sehemu ya kujifurahisha. Haikupedeza hata kidogo.Bondia Nyilawila alitumia raundi zote 10 za pambano hilo kuhakikisha anaizima staili ya upiganaji stadi ya Cheka kwa kumkumbatia kila wakati kama 'wakumbatianavyo' watu ambao hawajatiana machoni muda mrefu.
Hakuna ushindi kwamba, Nyilawila aliamua kufanya hivyo ili kuhakikisha anamaliza raundi zote za pambano hilo bila ya kujiruhusu kutupa ngumi zake kwa ufasaha au kumruhusu Cheka kutupa makonde yake. Mwisho, pambano liliisha kwa ushindi wa pointi kwa Cheka huku Nyilawila akionekana kufurahia zaidi kwa kumaliza raundi zote 10 licha ya kupigwa.
Wakati Nyilawila akiwa na taswira ya furaha kumaliza na kudundwa kwa pointi, hali ilikuwa tofauti kwa mashabiki ambao baadhi yao walisikika wakimlalamika kutumia mbinu chafu kuzima utamu wa masumbwi.
Na sasa imekuwa kama fasheni kwa mabondia wengi nchini ambao wanajiona wako katika kiwango cha kupigana na Cheka. Wengi wanaongea maneno mengi ya kujigamba kabla ya pambano lakini wakati wa pambano lenyewe huwa hawana jipya na wanazuia uhondo wa mechi yenyewe kwa kumdhibiti Cheka kwa kumkumbatia ili asiweze kurusha makonde yake.
Ingawa kwa wataalamu wa ngumi wanaweza kuichukulia mbinu hii kama njia pekee ya kupunguza makali ya adui mkali, lakini ukweli unabakia pale pale kuwa huu ni wizi wa viingilio na utapeli kwa mapromota wanaoandaa mechi hizi. Kabla ya Nyilawila kuonyesha tabia hii Jumamosi iliyopita, tayari bondia Mada Maugo alipigana na Cheka katika pambano lao la mwisho ukumbi wa PTA akitumia staili hii inayokera.
Bondia pekee ambaye alipambana nyakati kadhaa na Cheka bila ya kutumia mbinu hii ya uwoga ni mkali wa ngumi, Rashid Matumla ambaye licha ya kuonekana kupitwa na wakati ulingoni lakini bado alipambana na Cheka mara kadhaa bila ya uoga. Ingawa alipigwa kwa pointi lakini alionyesha ukomavu wa hali ya juu na kuwapa ladha ya ndondi mashabiki wake. Kitu kingine kinachokera ni tabia ya mabondia hawa kulalamikia matokeo pindi wanapopigwa kwa ajili ya kujenga utata usio wa lazima ili wapate nafasi ya kuchuma fedha za pambano la marudiano.
Mapema wiki hii, bondia Maugo kwa mara nyingine alisaini mkataba wa kupigana pambano la marudiano na Cheka katika ukumbi wa PTA Sabasaba April 28 mwaka huu.
Lakini kuna uwezekano mkubwa pambano hilo likawa halina jipya kama Maugo atarudi ulingoni akiwa na mbinu zile zile za kumdhibiti Cheka kutorusha ngumi zake kwa kuamua kukumbatia mara kwa mara.Hii ilitokea katika pambano lao la kwanza lililopigwa ukumbi wa PTA ambao Cheka licha ya kushinda aliondoka ukumbini akilia kwa malalamiko kuwa Maugo alikuwa anatumia mbinu chafu ya kumkumbatia kwa muda wote kiasi cha kushindwa kurusha ngumi zake wala kupigana kifundi.
Ni wazi kwamba Cheka yuko juu kwa sasa, lakini bado mabondia waliopo wangeweza kupambana naye kwa ustadi kama wangekuwa na nidhamu ya mazoezi na bidii ya hali ya juu kama ambavyo Cheka amekuwa akisifiwa na mashabiki. Kwa kufanya hivi, ngumi zitarudisha hadhi yake na kuturudisha tena katika zama za akina Stanley Mabesi, Iraq Hudu, Charles Libondo, Koba Kimanga na wengineo.
Wakati umefika kwa wahusika kukomesha utapeli huu wa wazi wazi kutoka kwa wapinzani wa Cheka. Wanaharibu ndondi na pia wanadhulumu fedha za maelfu ya mashabiki ambao huwa wanavutika katika mapambano yao.
Kwa mfano, katika pambano la Jumamosi iliyopita kati ya Cheka na Nyilawila, kulikuwepo na mabasi matatu yaliyosafirisha watu kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa ajili ya kuhudhuria pambano hilo. Lakini hakuna walichoambulia zaidi ya mbinu mbovu za Nyilawila.
Ndondi ni tofauti na soka. Katika soka kama mchezaji mmoja au wawili wanatumia mbinu mbovu wenzao wengine wanaweza kuwaburudisha watazamaji, lakini katika ndondi kama bondia mmoja anaharibu mchezo ni vigumu kwa mwingine kufanya vizuri.
Wahusika wa mchezo wa ndondi ambao wanaandaa mapambano haya tayari wamesikia malalamiko haya kwa muda mrefu na pengine sasa ni wakati wa kuchukua hatua.
|