
| Tumeendekeza siasa,kusahau uchumi hakika tutakwama | Send to a friend |
| Wednesday, 11 January 2012 09:15 |
|
Mhariri Ipo mifano mingi ya jinsi ambavyo siasa ndizo zinazojadiliwa zaidi kupitia mijadala, mihadhara (siyo ya kidini), makongamano na kadhalika au wakati mwingine wasomi waliobobea kuacha taaluma zao zikiwamo udaktari, ualimu na kuzama katika siasa. Kwa bahati mbaya, siasa imeachiwa kutawala mambo mengi yakiwamo uchumi, kiasi kwamba ni ndara kusikia wataalam wa uchumi wakiwa wameandaa kongamano la kitaifa la kuangalia namna ya kuisaidia nchi yetu kuondonana na matatizo kama ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, sababu za kuzidi kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali ambazo nyingine ni muhimu katika maisha ya kila siku. Binafsi, sipingani na hao wanaopigania kupatikana kwa katiba mpya, ila najiuliza, vipi uchumi wetu ambao unadumaa na kupooza kila uchao, mbona hakuna mahali ambao wataalam wake na wadau wengine wanakutana na kuangalia nini kifanyike, kuweka mikakati ya kusogea mbele? Hata wakati mwingine unasikia makongamano kama ya kujadili hali ya siasa katika Tanzania na kisha yanapitishwa maazimio, lakini sikumbuki tunaazimia nini katika uchumi, biashara au afya! Kama mwanajamii katika Tanzania, ninaamini kuwa hata Wizara ya Fedha na Uchumi, wataalam wake wanatakiwa kushirikiana na wengine kama wa Kilimo, Ushirika, Biashara na kuangalia jinsi ambavyo tutapiga hatua na kuiondoa nchi yetu katika janga hilo la umaskini wa kupindukia. |














