
| Gharama za maisha zinawagusa wabunge peke yao? | Send to a friend |
| Wednesday, 18 January 2012 09:39 |
|
Kutokana na kutapatapa kwa watendaji hao wawili, Katibu wa bunge, Thomas Kashililah aliyekana kuwepo ongezeko la posho za Wabunge na baadaye Spika wa bunge Anne Makinda alithibitisha kupanda kwa posho kutoka 70,000 hadi 200,000. Kutofautiana huku kwa kauli ya Katibu wa bunge ni ishara kuwa kitendo hiki cha kuongezewa posho kimefanyika kienyeji na hakikupata Baraka kutoka kwa ofisi zinazohusika. Lakini kitu kingine kinachoshangaza ni utetezi wa spika Makinda juu ya sababu za kuongezeka kwa posho hizo linatokana na kupanda kwa gharama za maisha katika mji wa Dodoma. Sababu hiyo haina mashiko kwa sababu, sio kweli kuwa maisha yamepanda Mkoa wa Dodoma peke yake? Na kama ni hivyo, Je vipi kwa wafanyakazi wa idara zingine wanaoishi mkoa huo, je? serikali inawasaidiaje kukabiliana na gharama za maisha? Kupanda kwa gharama za misha ni kwa Watanzania wote na wala si kwa wabunge tu. Nyongeza ya posho za wabunge inaashiria nini kwa idara za serikali kama walimu, askari na wahudumu wa afya ambao wanafanya kazi ngumu na katika mazingira magumu na ya hatari ambao hawajafikiriwa katika kupanda kwa gharama za maisha? Watanzania sasa hivi tunalia na kupanda kwa bei za vyakula kila kukicha lakini hakuna lolote linalofanyika ili kupunguza hali hii. Hali hii inaweza kutafsiriwa kuwa serikali kutowajali wafanyakazi katika idara zingine ambao hata mishahara yao ni midogo ukilinganisha na gharama za maisha kwa sasa. Kwa hali ya sasa kuna matatizo mengi ya kijamii yanayohitaji utatuzi na si kuwaangalia wabunge tu. |














