
| Kutoka London:Fasdo kituo kinachosaidia vijana wa Tandika, Bongo | Send to a friend |
| Friday, 07 October 2011 14:48 |
|
SIKU chache zilizopita nilimhoji Lilian Nabora dada wa Kitanzania anayesomea utawala na maendeleo Chuo cha Utafiti wa Maendeleo Ulaya, Ubelgiji. Bi Nabora mwenye miaka 43 pia ni mzazi wa watoto watatu. Wakati haendi darasani Lilian hufanya kazi Ubalozi wa Botswana, mjini Brussels. Mbali na kusoma, kuajiriwa na kulea, Bi Nabora anajishughulisha na kituo cha kuendeleza vijana, Fasdo, pale Tandika, Dar es Salaam. Kiasilia, wanawake wameumbwa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Wazungu hutumia neno “multi-tasking” kuelezea kadhia hii. Na ndani ya dunia yetu leo yenye mawasiliano ya haraka ni muhimu sana kuwa mtu uliye tayari kwa vyovyote kitaaluma. Pamoja na kuzaa wanawake wetu hulea na kutunza nyumba. Hivyo si wengi wanaopata fursa ya kusoma sana na kuwa wataalamu waliobobea. Yapo mamilioni ya kina mama nchini wanaofanya mazito lakini hawatajwi (na bahati mbaya hawatakaa wakuuzwe ndani ya vyombo va habari). Ni mashujaa wasiosikika wala kutukuka; rafiki yao mkuu Mungu Mwenyezi anayefahamu siri ya tunda na ua jema. Kwa hiyo si kweli Lilian Nabora ni bora kuliko wenzake; bali ni mfano tu wa namna ambavyo wanawake wetu Tanzania walivyo shupavu, wachapa kazi na wanaostahili sifa pale inapobidi. Je, sisi Watanzania tuna desturi ya kumsifia mtu anayefanya vizuri au wepesi kuropoka mabaya pale anapokosea? Bi Nabora alikulia Temeke akenda zake kusoma Majuu. Anasema akiwa likizoni mwaka 2008 aligutushwa na hali ya vijana wa pale. Hawakuwa na kazi wala elimu; na hakuna aliyewasaidia ndani ya kitongoji kile kilichosakamwa na umaskini na UKIMWI. Aliona njia ya kuwaendeleza vijana ni kutumia michezo, muziki na sanaa za maonyesho. Mwaka 2009 Fasdo ilisajiliwa. Ingawa mwasisi na anayesukuma Fasdo ni Lilian Nabora, uongozi wa kituo unahusisha pia, viongozi mbalimbali, madereva na wataalamu kwenye bodi ya utawala; wake kwa waume, wageni na Watanzania. Kati ya wageni wahusika ni Brendon Church, mkurugenzi wa MediaAid.Org mwenye ujuzi wa kutangaza habari mtandaoni aliyetengeneza tovuti yao. Brendon anasema anaipenda sana Tanzania na kuonyesha penzi hilo hujihusisha na maendeleo ya watoto yatima. Wengine ni Anita Maira mwenye shahada ya utawala wa maendeleo ya jamii; pia mama wa watoto wawili. Anita hufanya kazi Benki ya Wanawake Tanzania inayosaidia biashara ndogo ndogo. Wanaye pia mwanasheria Kamana Stanley Kamana, vile vile mmoja wa waasisi wa Fasdo aliye ofisi ya Wizara ya Masuala ya Katiba na Sheria. Bwana Kamana hujitolea kutoa masomo ya sheria kila Jumamosi. Kifedha Dada Lilian hujitolea akisaidiana na Mzungu, James Lace. Kirefu cha Fasdo ni “ Faru Arts and Sports Development Organisation” na lengo lake ni kuendeleza vijana kimichezo, kitaaluma na kiafya. Je tunaweza kujifunza nini kutokana na vituo kama Fasdo? Kihistoria, ugunduzi na mabadiliko yameletwa na bidii ya watu binafsi. Mambo mbalimbali yaliyosaidia maendeleo yetu wanadamu yametokana na juhudi za mtu mmoja aliyehusisha wenzake, akasaidiwa na jamii au kukinzana nayo hadi badiliko lilipotokea. Simu iligunduliwa na Mwingereza, Alexander Bell; gari la kwanza lilijengwa na Mbelgiji , Ferdinand Verbiest karne ya 17. Verbiest aliyezungumza lugha tano alikuwa na vipaji vingi akasafiri nchi mbalimbali ikiwemo China alikojenga uswahiba na Mfalme Kangxi. Kabla ya kupanga chombo kinachosemekana kuwa kilikuja kuwa gari karne ya 19 mtaalamu Verbiest alifundisha hesabu, falsafa na muziki ndani ya ukumbi wa Mfalme huyo wa Kichina. Aghalabu, basi, watu binafsi wanaojituma, wenye nidhamu bila kumngojea mchawi au malaika ndiyo wanaohitajika Tanzania. Hatujakumbwa na zahma la mauaji ya kivita vya wenyewe kwa wenyewe mathalan Wasomali wanaoghafilishwa na magaidi wa Al Shabab. Ingawa Tanzania ina amani bado tunayo matatizo mazito yasiyotakiwa kuwepo yaani umaskini, maradhi na ukosefu wa elimu. Juzi nilikuwa napiga soga na rafiki mmoja katika simu. Nilipomweleza kuwa natazamia kuja Tanzania juma hili akasema “kaa macho utakapokuwa mjini.” Je, akimaanisha vibaka? Akasema ndiyo lakini kuna zaidi. Nikamweleza huwa nahisi woga mjini London kuliko Tanzania. Hapa Uingereza unaweza kupigwa kisu kwa kumkodolea mtu usiyemjua macho barabarani. “Kwa kutazamana tu?” Akaniuliza. Wakati ‘naishi Marekani ya Kusini, miaka mingi iliyopita, wasiwasi ulikuwa kupigwa risasi. Siku moja usiku nilimpa lifti mmoja wa wanamuziki tuliokuwa bendi moja kitongoji cha Tijuca Kaskazini ya Rio De Janeiro. Wakati narudi kwa kuwa safari ndefu, niliegesha gari kando ya barabara kujisaidia. Kumaliza tu nikashtukizia kasheshe. “Mikono Juu!” Nimezingirwa na magari matatu ya polisi; washachemka; taa machoni, vimulimuli vyekundu na vyeupe vinanimulika. “Piga magoti!” Askari zaidi ya sita sasa wamenizunguka. Mitutu yao ya bunduki imeelekezwa rohoni kwangu; nanusa mauti, naisikia harufu ya damu. “Nimefanya kosa gani mabwana?” Nikauliza kwa Kireno. “Kelele! Tunakujua wee muuza dawa za kulevya. Nani wengine katika gari lako?” Kawaida katika hali kama hii unatakiwa ujieleze haraka na kwa ufasaha. Ukikosea, ukisita au tuseme ukileta ujeuri au kujibu ujinga; mwisho wako. Nikasema upesi mi mwanamuziki, nikawaambia wafungue gari watakuta magitaa mawili. Mmoja kanisogelea... “Wee unatoka wapi?” Maana kutokana na lafudhi yangu haikuelekea nilikuwa mwenyeji. Nikawaambia, Tanzania. “Wapi hiyo? Australia? Tasmania? Mbona hatujawahi kumwona Mwaustralia mwenye sura yako. Usitudanganye wewe jambazi tunakujua!” “Tanzania. Nchi ya mlima Kilimanjaro, kisiwa cha Zanzibar...” Kutaja Zanzibar ikawa kama nimewapa almasi. Miaka michache awali mwanamuziki mashuhuri wa Kibrazili, Gilberto Gil alitunga wimbo uliosifia visiwa vya Zanzibar na Pemba. Baadhi ya wale maaskari waliufahamu wimbo huo. “Tupigie basi wimbo wa Kizanzibari!” Ikawa mkombozi wangu; nikaruhusiwa kunyanyuka pale, bunduki zimeshushwa, usiku ule wa manane, kati kati ya sehemu iliyofanana na Buguruni sasa nabwabwaja : “Malaika Nakupenda Malaika...” Wabrazili kwa muziki utawaweza? -Barua pepe: This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it -Tovuti: www.freddymacha.com |














