MwanzoContactsEmail
Home Uchambuzi Kolamu Yaelekea CCM ya Kikwete imesahau ilitokoka, iliko na kule iendako!
BOOKMARK THIS PAGE
Yaelekea CCM ya Kikwete imesahau ilitokoka, iliko na kule iendako!  Send to a friend
Monday, 28 November 2011 11:35

(Rais Kikwete)
WIKI chache zilizopita niliandika kupitia katika safu hii uchambuzi wenye kubeba kichwa cha habari, CCM; mtoto umleavyo ndivyo akuavyo!

Nilieleza kwa ufupi katika uchambuzi huo kwamba  siku chache zilizokuwa zimepita jamii yetu ilikuwa imeshuhudia mambo mengi ya ajabu yakijitokeza, kutendekea na kisha kupita na kusahaulika.

Nikaeleza kuwa miongoni mwake ni kauli kadhaa za ajabu  zikiwamo zile kali na nzito ambazo zote zimekuwa zikitolewa na vijana ndani ya chama tawala, CCM.

Nikaongeza kuwa kauli hizo ambazo zimezua mijadala mingi katika jamii yetu  zinaonyesha kitu kimoja kikubwa kwamba chama hiki kikongwe ambacho kwa muda mrefu wa uhai wake kikiwa madarakani kimejivunia idadi kubwa ya wanachama wake watii na waadilifu, sasa kimedhoofu na kuanza kupoteza mwelekeo.

 Huko nyuma niliwahi pia kueleza katika safu hii kuwa zama zile, yaani wakati wa uhai wa Tanganyika African National Union (TANU) ya kina Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rashid Mfaume Kawawa na  timu yao nzima, umoja wa vijana au wakati  ule Tanu Youth League au TYL  ulikuwa ndio nguzo na hazina kubwa ya chama.

Ndani ya TYL ni mahali ambako vijana wote waadilifu waliandaliwa vizuri ili kuwa viongozi wa siku za baadaye na wazalendo wa kweli wa nchi hii.

Nikaeleza kwamba zamani zile ilikuwa nadra  mno kuona vijana waliohitimu kutoka TYL wakigeukana, kubadilika kuwa mzigo au wabeba lawama na badala yake walikuwa msaada mkubwa kwa chama na serikali yake.

Nikaeleza pia kuwa ukisikia kijana ameteuliwa kwenda Ihemi, chuo maalum cha mafunzo na itikadi kwa vijana kwa ajili ya mafunzo yanayohusu itikadi ya TANU na hatimaye CCM ya miaka ya mwanzo, hakika ulitambua kwamba kijana yule kweli alikuwa akiandaliwa kuwa kiongozi mzuri wa siku zijazo.

Haikuwa ajabu kuona wahitimu wale kutoka Ihemi wakielekea katikamasomo zaidi kwenye  vyuo vingine vya itikadi vya makada  wa chama hicho kama vile, Hombolo kule Dodoma, Murutunguru cha Ukerewe au hata Kivukoni, Dar es Salaam, ambavyo kwa leo havipo tena.

Wengi wengi walipelekwa kwa mafunzo ya juu ya itikadi au propaganda kule Ulaya Mashariki au hata Urusi, ambako hakuna shaka walinolewa zaidi na kutokea kuwa makada hodari mno ambao baadaye walibadilishwa na kuwa viongozi imara wa Tanzania ya miaka ya kwanza ya uhuru.

Hadi leo ipo mifano ya vijana wengi wazuri na ambao walipitia hatua zote hizo za uongozi na ambao ama wengine bado  wapo serikalini katika  idara au taasisi za umma ambako kote wanachapa kazi vizuri.

Tena wengine  kati yao ni waadilifu, watu makini, ingawa inawezekana kama wasemavyo waswahili katika msafara wa mamba, kenge wamo pia, baadhi yao wamepotoka au kupotoshwa!

Lakini, uamuzi wa  CCM kuacha taratibu za kusaili watu wote wanaoomba uanachama na kuanza kuwa na wanachama wa haraka au papo kwa papo, ni kasoro nyingine kubwa ambayo imekizorotesha mno chama hiki na hata watendaji wake.

Kwa hiyo, kelele zote ambazo zinasikika kwa sasa nchini mwetu, mashambulizi au makombora yote ambayo yanaelekezwa kwa chama chenyewe au viongozi wengi, wengine wao wakichafuana wao wenyewe tena ndani ya chama hiki ni ushahidi wa kuondoka kwa misingi ya kuanzishwa kwa chama hiki.

Madai ya  mmomonyoko wa maadili yote ambayo yalijengwa na kuaminiwa katika jamii ya Tanzania ni moja ya magonjwa sugu ambayo yanakisumbua chama hiki.

Matokeo yake, ndiyo  maana tunashuhudia kambi mbalimbali zinazopingana wazi wazi ndani ya chama hiki, zimepanda mbegu au chachu ya chuki ambayo kwa bahati mbaya imeota na   imeanza kusambaa, imestawi mno hata ndani ya vyama vingine  ambavyo vimeiona au kuichukulia CCM kama mfano wa kuigwa au dira.

Sote ni mashuhuda wa vikao vikuu vya CCM ambavyo vimefanyika na kumalizika kule Dodoma wiki jana ambako wengi katika Tanzania walidhani kuwa ungepitishwa uamuzi mzito na yenye lengo la kukisafisha chama.

Matarajio ya wengi yalikuwa ni kwa uongozi wa CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete kuanza kuwachukulia hatua zikiwamo za kinidhamu viongozi  wote au wanachama wale ambao wamekuwa wakidaiwa kuwa wamechafuka na hawana sifa ya kuendelea kuwa viongozi ndani ya chama hiki.

Badala yake, tumesikia mengi yakiwamo kama kauli nzito kama ile iliyoibuliwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli.

Lowassa, kada wa CCM ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hiki amekaririwa na vyombo vya habari karibu vyote siku ya Ijumaa akiwalaumu viongozi wenzake kwa kumchafua.

Sidhani kama Lowassa alikuwa akitania alipoamua kueleza kile kilichoko moyoni mwake mbele ya kadamnasi ile ya wajumbe kwamba amechafuliwa kwa miezi saba, akimtaka mwenyekiti wake (Rais Kikwete) achukue hatua dhidi ya wabaya wake.

Siyo kama kujaribu kujilinda, kwani tumeambiwa kuwa hata Frederick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kikao kile, akaeleza mshangao wake kwa chama chake, hasa kwa kushindwa kuwachukulia hatua wale wanaotumia vibaya jina la chama kuwachafua wenzao.

Ndipo hapo nikarejea katika kauli yangu kwamba sasa CCM imekuwa nyumba au familia ya kambale ambayo kila mmoja ana sharubu!

Ni kama familia ambayo imekosa usimamizi thabiti wa baba kwa watoto na mke wakena matokeo yake, kila mmoja anafanya atakalo kwa muda apendao!

Ninajiuliza, hivi kamati ya maadili ya chama hiki ambayo imebebeshwa mzigo kuhusu madai haya ya kina Lowassa na Sumaye, inayo meno ya kung’ata kipande cha nyama na kukitupa au ni kibogoyo, pengine kama kilivyo chama chenyewe?

Ninajiuliza, CCM ambayo inaonekana kuwa dhaifu na ambayo inalaumiwa na wengi, haioni kasoro zote ambazo zinawafanya watu mbalimbali wakiwamo wapenzi na mashabiki wake wapoteze imani ya chama kiasi hiki?
Kama hivyo ndivyo, ni lini CCM hii ya Kikwete itafanya uamuzi mgumu na ambao utabakia kuwa simulizi katika jamii ya Tanzania kwa miaka mingi ijayo?

Je, kamati ya maadili ambayo inaonekana kutwisha msalaba na mzigo ambao viongozi wa CCM hawaugusi ina ubavu wa  hata kupendekeza kwamba wakosaji wang’olewe kutoka viti vyao?

Kwa hiyo, ni nini kifanyike ili kukinusuru chama hiki katika hatari ya kusambaratika katika miaka michache ijayo?
Hili ni swali gumu na zito ambalo uongozi wa kitaifa wa chama hiki chini ya  mwenyekiti Kikwete , Wilson Mukama akiwa katibu mkuu na bila shaka Pius Msekwa kama makamu mwenyekiti bara na Amani Abeid Karume, kule visiwani wazinduke sasa.

Lakini, kikubwa zaidi, Mukama ambaye ndiye mtendaji wake mkuu wanatakiwa kukaa chini na kufanya tafakuri ya kina na kupata suluhu.

Mbali ya tafakuri hii nzito, viongozi hao ambao miezi michache iliyopita wameibua dhana ya ‘kujivua gamba’waitumie kupitisha uamuzi mzito ambao hata kama unaumiza na ambao ni mchungu kama shubiri ufanyike kwani wengi wanaikumbuka dawa ya klorokwini ambayo ilikuwa chungu mno lakini mgonjwa hakuwa na budi kuimeza ili kupona malaria, hivyo uamuzi mgumu ndio utainusuru CCM katika hatari ya kuanguka.

Kwa ushauri wako, Kikwete kama waswahili wasemavyo, ‘ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke’ na hilo ndilo linalotakiwa kufanyika katika CCM ya mwaka 2011 na michache ijayo tunapelekea mwaka 2015, ambako upepo na nyufa za kuwania urais zinazidi kujitokeza na kuwa dalili mbaya kwa chama hiki kama anavyokiri Mukama!


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner