
| Urafiki wa wabunge na na DK Magufuli utufumbue macho | Send to a friend |
| Monday, 09 January 2012 10:52 |
|
Nimejiuliza ni wapi ulikotoka urafiki huu wa ghafla mno ambao unaweza kuuita wa shaka baina ya wabunge wa majimbo saba na wenzao kadhaa wa viti maalum, kutoka vyama vyote umetoka wapi hasa na mbona hatukuwahi kuusikia au hata kuuona kwa macho? Nikaenda mbali, mbona hatukuwahi kuwasikia wawakilishi wetu hao wakikutana iwe kule Dodoma au kwingine wakati wowote kabla na wakati wa vikao vya Bunge ili kuweka mikakati thaibiti ya mambo ya msingi ya kujadili na ambayo yanawahusu wakazi wote zaidi ya milioni tatu wanaoishi Dar es Salaam? Ninajiuliza, hivi tatizo kubwa linaloisumbua Dar es Salaam yetu ya leo ni ongezeko tu la bei ya kivuko cha Kigamboni ambayo imewaweka vitani wabunge hao na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli? Kama nilivyoeleza awali, hakuna jibu la moja kwa moja la maswali haya na mengine ambayo yanafuatia mzozo na mgogoro usio na lazima ambao unaelekea kukuzwa kwa upande mmoja na umoja huu wa wabunge kwa upande mmoja na chama tawala, CCM kwa upande wa pili. Kama ilivyo, naamini Dk Magufuli ni binadamu. Yeye, bado ni mwakilishi tu wa wapigakura wa Jimbo la Chato (kule katika mkoa usiokuwapo Geita), ambaye wapigakura wake walimwamini kwa kumpa kura nyingine kwa uchapakazi wake, hata kama anao udhaifu wake binafsi kama binadamu mwingine na ndiyo maana hata Rais Jakaya Kimwete akamwanini! Lakini, kama ambavyo nimekuwa nikieleza mara kwa mara kwamba ningekuwa mbunge, basi ningetangaza maslahi binafsi baina yangu na Dk Magufuli, ambaye si bahati mbaya, bali ni kwamba tulisoma wote elimu ya sekondari miaka ile ya ’70 kule Biharamulo, Mkoani Kagera, hivyo ninamfahamu kwa kiasi cha kutosha. Ninafafahamu jinsi asivyopenda mzaha, kuuma maneno, kwani anapohisi kuna jambo, yeye atalisimamia kwa dhati, kulisema hadharani na hata kutaka litendeke na hivyo ndivyo alivyotaka katika hili la kivuko cha Kigamboni, ambako hakuficha hisia zake kwa kueleza kwa miaka 14 nauli imebakia kuwa Sh100 wakati vivuko katika maeneo mengine nchiin bei zipo juu. Siamini kuwa umoja huu wa wabunge wa Dar es Salaam chini ya Abbas Mtemvu, Mbunge wa Temeke haukumwelewa vizuri Dk Magufuli, hasa kwa dhamira hii ya kutaka wakazi wa eneo hili ambalo tumeambiwa kuwa litageuzwa jiji la kisasa, hawawezi kulipa Sh200 kwa ajili ya kuvuka kwenda na kurudi kuroka katikati ya jiji na maeneo mengine. Naamini kilichoko katika nyoyo za Mtemvu na timu yake ambayo inaundwa pia na Dk Faustine Ndugulile, kijana msomi mzuri ambaye sina shaka anabeba jukumu zaidi la kuwapigania wapigakura wake (Kgamboni) wapate maendeleo, si pekee wananchi kuvuka kwa Sh200, bali namna ya kuondokana na umaskini mkubwa. Ni umaskini huo uliowageuza wengi wa wazawa wa Kigamboni kuwa watumwa kwani wameuza ardhi na maeneo yao kwa wageni, wawekezaji wa ndani na nje, kisha wao wakakimbia kwenda kuishi maeneo ya mbali! Jikumbushe kidogo zile zama za giza ambako baadhi ya wanafunzi wakiwamo wa Shule ya Msingi Bunge ya jijini Dar es Salaam walivyotumbukia baharini na kufa wakati wakivuka, huku mwalimu wao, Elmus Rwakarehe (Mungu amlaze pema peponi) alivyojitosa kuwaokoa, naye akafa. Nilidhani kuwa Dk Ndugulile ,mwakilishi wa wapigakura wa kule angekuwa akishiniliza Serikali au hata kuulizia iko wapi ile tuzo ya Rwakarehe, ni wapi ilikofia baada ya mwalimu kijana yule kupoteza maisha yake na kisha Serikali kuamua kuanzisha tuzo ya ushujaa kwa heshima yake, ambayo haipo tena katika kumbukumbu au msamiati wao Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Hapa suala la msingi kwa umoja huo lingekuwa kuhoji zinapokwenda fedha zote zinazokusanywa kivukoni pale tangu zikiwa Sh50 hatimaye Sh100, ambazo kwa sasa Dk Magufuli anapendekeza zipande na kufikia Sh200, ambazo bado naamini wakazi wengi wa Kigamboni wanazidumu. Kigamboni ya sasa, tusijidanganye inao matajiri ambao Sh200 kwao si tatizo hata kidogo, ingawa inawezekana kuwa pia wapo maskini ambao hawawezi kuimudu hiyo Sh400, kwa maana ya 200 asubuhi na nyingine 200 jioni, ingawa naamini ni wachache mno! Nimesema kuwa Dk Magufuli kama binadamu yeyote bila shaka anazo kasoro zake nyingi tu, anaweza kuwa aliteleza ulimi wake kwa kauli ya kutaka wananchi wapige mbizi kwenda na kutoka Kigamboni kama hawawezi kulipa Sh200 za nauli. Lakini, mbona nauli kubwa zinawaumiza wakazi kama wa Bunju, Boko, Mbezi, Kibamba, Bonyokwa, Malambamawili na kwingi kwingineko hapa Dar es Salaam? Je, wabunge wetu kwa umoja hawana habari kwamba wakazi hao ambao pia ni wapigakura wao hawazioni tena nauli kubwa kama tatizo kwani kwao kulipa Sh500 au zaidi tena kwa safari moja, mfano ya kutoka Mbezi hadi Mwenge au Kariakoo, Posta au Tegeta- Ubungo, Bunju hadi Kariakoo kwa Sh800 si jambo la ajabu, ambalo nilidhani kuwa umoja huu wa wabunge ungekuwa ukizungumzia? Ninawaonea huruma wakazi wa wote mabondeni ambao wamehamishiwa kule Mabwepande, ingawa pia ninawapa mkono wa heri kwa kuyakimbia maafa yakiwamo mafuriko, lakini nauli ya kutoka huko Kariakoo si chini ya Sh1,300 kwa safari moja, je, wabunge hao chini ya Mtemvu wataandamana? Niliamini kuwa umoja huo ungekwenda hadi Sumatra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini) na kuwalilia wakazi wa maeneo karibu yote ambao kwenda na kurudi kazini au kwenye biashara zao ndogo au kubwa ni vita, yaani ya kugombea magari asubuhi na jioni, kushindana na misururu mirefu ya magari kwa zaidi ya saa mbili! Nilidhani wawakilishi wetu wangetumia umoja wao kukataa bajeti ya wizara kadhaa za serikali ambazo idara zake zina upungufu na ni chanzo cha mateso kwa wakazi wa Dar es Salaam. Kwa mfano, kama wakazi wengine wa maeneo kama Kimara, Mbezi, Kibamba au hata Goba na kwingi kwingineko hapa Dar es Salaam hawana maji ya kunywa, kuoga, wengine wana matatizo kama ya uharibifu wa mazingira kama ambavyo tumeiona Dar es Salaam yetu kwa muda mrefu inanuka, je, hili si jukumu ambalo umoja huu ungeweza kulishikia bango au haliwahusu? Je, wawakilishi wetu hawaoni tatizo sugu la ongezeko la watu ambalo haliendi sambamba na upatikanaji wa huduma zilizopo, hili nalo haliwahusu wabunge wa Dar es Salaam? Hawaoni tatizo kiasi kwamba wakienda Dodoma wawasilishe hoja binafsi wakiibana Serikali iamke na kuacha kulewa sifa ambazo hazina msingi huku uchumi binafsi wa mtu mmoja, kaya hadi taifa ukizidi kudumaa? Tanzania imedumaa kiuchumi, tunaambiwa kuwa utafika wakati hata mishahara ya watumishi wa sekta ya umma haiwezi kulipwa kwa kuwa Serikali imechacha (haina fedha), hakika sikubaliani nao (wabunge)! Nilisema chama tawala, CCM pia kinao mkono katika hili kwani tumemsikia mwenyekiti wake wa mkoa huo, John Guninita akiingia kichwa kichwa katika mzozo huu akidai kuwa Dk Magufuli amekuwa akiendesha mambo kwa ubabe, udikteta wa hali ya juu. Hapa, ndipo ninaposema kuwa CCM, hasa kwa ngazi ya taifa ilitakiwa kumzuia mtu kama Guninita kuzidi kuuchochea mzozo huu baina ya wabunge wa Dar es Salaam na Dk Magufuli kwani chama hakina budi kujua kuwa moto ambao umewashwa si rahisi kuzimika. Vinginevyo, chama hiki kikongwe cha Rais Kikwete na timu yake nzima ambacho kwa macho ya wengi kinaonekana dhaifu mno, kilichozaa Serikali goigoi na legevu, kitakuwa kinajichimbia kaburi! |



NIMEKUWA kwa karibu wiki nzima nikijiuliza ma swali kadhaa, lakini hadi leo sijapata majibu ambayo yanasadifu , kiasi cha kuniondolea shaka.











Comments
pili jinsi bei zilivyopandishw a, sio hiyo mia mbili tu, bali angalia GUTA lililo beba nyanya n.k. limepandishwa kutoka Sh. 300 hadi.... kiasi ambacho kimesababisha bei ya bidhaa MUHIMU katika maeneo yote ya Kigamboni kupanda kwa zaidi ya asilimia 150;
Kwa hiyo maelezo yako ya Kumsifu kitimate wako John Pombe Magufuli kwa kuzunguka kwenye hiyo mia mbili ni upotofu kwa kiasi fulani.
Kuna wanaoweza kupiga mbizi, na wanapiga lakini hawawezi wanajikakamua, hawana la kufanya
Yeyote anayelinganisha kupanda kwa nauli ya kivuko cha kigamboni na vivuko vingine au nauli ya kwenda sehemu nyingine,au ushuru wa kuingia ubungo bus terminal nk kitaalam anakosea sana! Hata ikiongezeka Tsh5/= kwenye nauli si tija kwa mwananchi. Gharama za maisha zinapaswa kushuka ili kuleta unafuu na maendeleo kwa mwananchi wa kawaida.