Thursday, July 10, 2014

Serikali itegue kitendawili cha mabomu ArushaIGP Ernest Mangu.PICHA|MAKTABA

IGP Ernest Mangu.PICHA|MAKTABA 

Tunasikitishwa na kuongezeka kwa matukio ya milipuko ya mabomu katika Jiji la Arusha, ambapo katika kipindi kifupi tu kisichozidi miezi 18 yametokea matukio saba ambayo yamesababisha vifo. Matukio hayo ambayo pia yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali yamejenga hofu kubwa kwa wakazi wa jiji hilo, hali inayotishia kudidimiza uchumi wa nchi yetu kutokana na jiji hilo kuwa kitovu cha shughuli za kitalii zinazochangia pato la taifa kwa kiasi kikubwa.

Pengine yafaa tujikumbushe angalao kwa kifupi tu mlolongo wa matukio hayo ambayo yameacha maswali mengi kuliko majibu. Mlipuko wa kwanza ulitokea Oktoba 2012 wakati bomu lililorushwa lilimjeruhi usoni Katibu wa Bakwata mkoani Arusha, Sheikh Hussein Jongo. Bomu la pili lilirushwa Mei 2013 katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti wakati wa ibada ya misa ya kubariki kanisa hilo na kusababisha vifo vya watu wanne, huku wengine 70 wakijeruhiwa.

Ibada hiyo ilikuwa ikiongozwa na mwakilishi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Montecillo, pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Arusha, Josephat Lebulu.

Bomu la tatu lililoua watu wanne na kujeruhi wengine 50 lilirushwa Juni 15 mwaka 2013 wakati wa mkutano wa Chadema wa kampeni za udiwani uliofanyika katika Viwanja vya Soweto, huku bomu la nne likirushwa Februari 24 mwaka huu katika Mgahawa wa Mercury.

Matukio hayo yalifuatiwa na bomu la tano lililorushwa katika Baa ya Night Park, Aprili 13 mwaka huu na kujeruhi watu 17, huku bomu la sita likirushwa Alhamisi iliyopita nyumbani kwa kiongozi wa Answar Muslim Youth Centre Kanda ya Kaskazini, Sheikh Sudi Ally Sudi. Bomu la saba lililorushwa siku nne zilizopita katika Mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine lilijeruhi vibaya watu wanane.

Tumeorodhesha matukio hayo yote siyo tu kuonyesha ukubwa wa tatizo, bali pia kujenga hoja kwamba pengine kuna siri iliyofichika nyuma ya milipuko hiyo. Inatuwia vigumu kuelewa jinsi taswira nzuri ya Jiji la Arusha, inavyoweza kuachwa kuchafuka kwa kiwango hicho. Kama tulivyodokeza hapo juu, hali hiyo imeacha maswali mengi kuliko majibu kutokana na Serikali kushindwa kutegua kitendawili kuhusu watu wanaohusika na milipuko hiyo.

Kwa maneno mengine, vyombo vya ulinzi na usalama vimeshindwa kutafuta mbinu za kuwakamata wahusika, ingawa Jeshi la Polisi limekuwa likitoa kauli zisizotekelezeka. Haiingii akilini kuona vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinashindwa kuwakamata wahalifu hao katika jiji hilo lenye eneo dogo sana kuliko majiji mengi duniani. Kushindwa huko pengine kunaipa nguvu dhana inayojengwa na baadhi ya wananchi kwamba milipuko hiyo siyo tu ni hujuma, bali pia ni mkakati uliosukwa na mtandao mahususi unaolenga kudhoofisha sekta ya utalii hapa nchini.

Vinginevyo juhudi za kudhibiti uhalifu huo zingeonekana, ikiwa ni pamoja na kufunga kamera za usalama, watendaji wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuacha ofisi zao na kupiga kambi jijini humo na kuongoza operesheni maalumu. Uhalifu huu haukubaliki na hauwezi kumalizwa na porojo za kisiasa. Serikali lazima itambue kwamba isipochukua hatua stahiki sasa watalii watatukimbia na matokeo yake sote tunayajua. Ni wajibu wake pia kulinda usalama wa raia na mali zao.

-->