Changamoto zilizojitokeza Ligi ya Kikapu zifanyiwe kazi

Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam ulikuwa ‘bize’ kwa takribani wiki moja wakati timu za mpira wa kikapu zilipochuana kuwania ubingwa wa Taifa (NBL).

Ligi ya Taifa ilishirikisha timu 14 na kushuhudia JKT ikitwaa ubingwa kwa kuifunga Savio katika mchezo wa fainali.

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Kikapu Dar es Salaam (RBA), Savio waliduwazwa baada ya kufungwa pointi 62-51 dhidi ya JKT. Nahodha wa JKT, Baraka Athumani alitwaa tuzo ya mchezaji bora.

Hata hivyo, JKT ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Afrika (BAL) itakayoanza Novemba 17 nchini Kigali, Rwanda haikutwaa ubingwa kwa urahisi.

Savio moja timu kongwe katika mashindano hayo, ilitoa upinzani dhidi ya mabingwa hao kabla ya kupoteza mchezo huo.

JKT ilicheza fainali baada ya kuichapa Oilers pointi 68-45 kama ilivyo kwa Savio ambayo ilikiangusha kigogo Pazi kwa pointi 69-45.

Awali katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu Oilers iliilaza Pazi kwa pointi 79-42.

Jambo la kuvutia timu za Rukwa Stars na Deep Sea Queens ya Tanga zilikuwa timu pekee kutoka nje ya Dar es Salaam zilizofuzu robo na nusu fainali.

Pamoja na timu hizo kuonyesha ushindani, mashindano ya mwaka huu yalikuwa na changamoto ambazo zilitia doa.

Kitendo cha umeme kukatika mara kwa mara kilitia dosari kwani baadhi ya mechi zililazimika kusimama muda mrefu kusubiri kununuliwa mafuta ya jenereta.

Dosari nyingine ilikuwa ni baadhi ya mechi kusimama wakati mvua ikinyesha kupisha wasimamizi wa uwanja kuondoa maji yaliyopenya kutokea juu ya bati.

Pia baadhi ya maeneo hayakuwa safi hasa nje ya jengo ambapo baadhi ya mashabiki walitupa taka ovyo na kufanya eneo hilo kutokuwa salama kwa afya.

Itakumbukwa michuano hiyo inajumuisha idadi kubwa ya wachezaji wa kikapu hodari wanaotamba katika timu zao za mikoa.

Wakati matarajio ya wengi ilikuwa ni kuona michuano hiyo ikifanyika kwa kiwango bora, hali ilikuwa tofauti.

Ligi hiyo ina umuhimu mkubwa kwani mpira wa kikapu uliitangaza Tanzania kimataifa kutokana na ubora wa wachezaji waliotamba.

Katika miaka ya 1990 hadi 2002 mchezo wa kikapu ulikuwa sehemu ya maisha ya vijana wengi hususani Dar es Salaam uliokuwa umesheheni wachezaji nyota.

Nimeitaja Dar es Salaam kwa sababu ndiyo ilikuwa kitovu cha mpira wa kikapu ingawa ipo baadhi ya mikoa ilifanya vyema katika mchezo huo.

Bila shaka wengi wanakumbuka enzi za Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD) kilichokuwa chini ya Mwenyekiti Simon Msofe na Katibu Mkuu Mbamba Uswege.

Vigogo hawa watabaki katika kumbukumbu ya familia ya mpira wa kikapu kwa mchango mkubwa waliotoa katika uongozi wao.

Mbamba alikuwa mhimili wa mpira wa kikapu na wengi wanakumbuka Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam ilivyokuwa na ushindani wa aina yake kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Shamrashamra zilizopambwa na wasanii nyota wa Bongo Fleva zilinogesha ligi hiyo huku idadi kubwa ya mashabiki wakimiminika uwanjani hapo.

Udhamini mnono wa baadhi ya kampuni kubwa ulichagiza ukuaji wa mpira wa kikapu na uliwaibua wachezaji hodari kutoka kila pembe ya Dar es Salaam.

Vijana wengi kutoka maeneo ya Upanga, Chang’ombe na sehemu nyingine za Dar es Salaam walifanya mpira wa kikapu kuwa sehemu ya maisha yao.

Fundi Abdallah Ramadhani ‘Dulla’ alitamba Pazi akiwa mchezaji bora wa aina yake kutokea nchini.

‘Dulla’ jina lililokuwa maarufu enzi zake, alikuwa MVP wa ukweli katika mpira wa kikapu na vijana wengi wa wakati huo wanakumbuka vitu vyake uwanjani.

Mbali na Dulla wapo baadhi ya wachezaji waliotamba na klabu tofauti akiwemo aliyekuwa nahodha wa muda mrefu wa JKT na timu ya Taifa Franklin Simkoko. Pia walikuwepo mastaa wengine Frank Bategeki, Michael Mwita, Ally Dibo, Adam Jegame, Michael Casmir, Juma Kisoky, Frank Kusiga, Haleluya Kavalambi na wengine wengi tu waliotamba.

Kwa mantiki hiyo ili tuwapate kina Dulla wapya ni vyema Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kuboresha mashindano mbalimbali kuanzia ngazi ya mikoa ili kupata timu bora. Kwa upande mwingine Serikali ifanye kitu kwa Uwanja wa Ndani wa Taifa kwani umekuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu.