Furaha hii kilimo cha korosho isaidie uzalishaji

Thursday November 1 2018

 

By HUSSEIN ISSA

Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, napenda kumpongeza Rais John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kutenga muda wenu na kukutana na wanunuzi na wakulima wa zao la korosho pamoja na kutoa msimamo wa Serikali kuhusu bei ya zao hilo.

Kwa hakika uamuzi huo umeweza kumaliza mvutano wa bei ya zao hilo kati ya wanunuzi na wakulima ambao ulikuwa unaendelea kwa muda mrefu.

Rais kwa kuguswa na mvutano huo, aliamua kuingilia kwa kuvamia mkutano wa majadiliano uliokuwa ukiendelea kati ya wanunuzi na Waziri Mkuu, Majaliwa.

Furaha inaendelea zaidi baada ya Rais kutoa msimamo wa Serikali kwa kuwataka wakulima kukataa bei zilizotolewa na wanunuzi katika minada iliyofanyika hivi karibuni ambapo kampuni za ununuzi wa korosho zilitangaza kununua korosho kwa bei ya kati ya Sh 2,717 na 1,900 kwa kilo ikiwa imeshuka kutoka zaidi ya Sh3,600 ya msimu uliopita.

Huu ndio msimamo ambao wakulima walitaka kuusikia kutoka serikalini na naamini kwamba wameufurahia hasa walipoambiwa kwamba endapo wanunuzi hao hawatakuwa tayari kununua korosho kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo, Serikali ipo tayari kuzinunua kwa bei yenye maslahi kwao na kutafuta masoko yenye bei nzuri nje ya nchi.

Tena, Rais alienda mbali zaidi kwa kuwahakikishia wakulima kwamba yuko tayari hata kutumia majeshi kununua korosho na kutafuta masoko ya uhakika ili iuzwe kwa bei nzuri.

Kicheko kingine kwa wakulima hao ni pale Rais Magufuli alipokubali kuondolewa kwa utozaji ushuru wa mara ya pili wa halmashauri uliokuwa ukifanywa baada ya korosho kufikishwa Mtwara.

Pia alipunguza ushuru wa Bodi ya Korosho kutoka Sh17 hadi 10 kwa kilo na ameruhusu wafanyabiashara kununua magunia yao wenyewe kwa ajili ya korosho badala ya kuuziwa na vyama vya ushirika kwa bei kubwa.

Ni kama vile ilifanyika ‘dua maalumu’ kabla ya kufika kwenye mkutano huo kwani Rais kukubali maombi ya wanunuzi kutaka kusafirisha korosho kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam ambapo kilo moja inasafirishwa kwa Sh47 kwa kutumia meli ambazo zimeleta mizigo mingine, ikilinganishwa na ile ya Mtwara ambako kilo moja inasafirishwa kwa Sh203 kwa kutumia meli zinazokodiwa kwa ajili ya korosho pekee.

Hata hivyo, kwa upande mwingine ni vyema wabunge wa kusini wakakumbukwa kwa sababu wamekuwa wakisimama mara kwa mara bungeni kuzungumzia changamoto za bei ya zao hilo linalowarudisha nyuma wakulima, iwapo halipangiliwi vizuri.

Hakika muungano wa wabunge hao ni wa kuigwa na wengine kwa sababu wameweka itikadi zao za vyama pembeni ili kuipigania korosho kwa kujali jasho la wakulima wao.

Pia wabanguaji wadogo wanayo nafasi kubwa na muhimu katika kufanikisha dhamira ya ubanguaji korosho na kuwaongezea kipato. Vilevile upo uwezekano mkubwa wa kuanzisha vikundi, kuviwezesha visimame na viwe endelevu. Rais ameonyesha nia na wataalamu hawana budi kumuunga mkono.

Tunachohitaji ni mahusiano yenye afya yatakayowezesha utendaji wa pamoja katika kuleta ustawi wa tasnia ya korosho nchini.

Changamoto kubwa tuitarajie kutoka kwa wabanguaji wakubwa duniani. Kwao, ubanguaji wa korosho ni chanzo cha uhakika cha ajira kwa raia wao.

Pia ni chanzo kikubwa cha mapato ya ndani na muhimu cha fedha za kigeni. Korosho zetu ndizo bora zaidi duniani, na wao miaka nenda - miaka rudi ndiyo wanunuzi wa korosho zetu ghafi. Hawatakaa kimya, tujiandae.