Hili la barabara za mwendokasi tuwasikilize viongozi wetu

Hivi ni kweli Watanzania ni wagumu kuelewa kiasi hiki? Kwa nini tunapokatazwa tusifanye kitu fulani hatusikii au tunataka hadi malaika ashuke ndiye aseme jambo hili haliruhusiwi?

Ni vigumu kuelewa hata agizo linalotolewa na Rais wa nchi? Mbona agizo lake linapuuzwa bila sababu za msingi na baadhi ya watu. Nimelazimika kulizungumzia tena baada ya kuona baadhi ya viongozi wa kitaifa na wale wa taasisi husika wakirudia mara kwa mara lakini wananchi hasa wakazi wa Dar es Salaam wanalipuuzia.

Hapa nazungumzia matumizi barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT), zilizojengwa katika barabara za Kawawa na Morogoro. Baadhi ya watu wenye vyombo vya moto wanazitumia licha ya kupigwa marufuku na Serikali.

Wa kwanza kupiga marufuku alikuwa ni Rais Magufuli ambaye kwa nyakati tofauti aliwahi kuwataka askari wa usalama barabarani kung’oa magurudumu ya magari, bajaji na pikipiki yanayopita kwenye barabara za mwendokasi.

Mwaka 2017, Rais Magufuli alisema, “ukiona kuna gari au bajaji na pikipiki inatumia barabara ya mwendokasi yashikeni, myapeleke kwenye kituo cha polisi na myatoe magurudumu, baada ya hapo watajifunza lazima wakati mwingine mtumie nguvu, katekelezeni hivyo hakuna atakayewasumbua mimi ndiyo amiri jeshi mkuu.”

Kama hiyo haitoshi, Machi mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Lwakatare aliungana Rais Magufuli kupiga marufuku magari mbalimbali yakiwamo ya wagonjwa akisema hadi yapewe ruhusa na polisi wa usalama barabarani.

Lwakatare alitoa agizo hilo baada ya kuona changamoto kwa watu wenye vyombo hivyo vya moto kuendelea kutumia barabara hiyo maalumu kinyume cha sheria. Marufuku hiyo ya mtendaji mkuu wa Dart ni kama vile iliwaingia watu sikioni upande wa kushoto na kutokea kulia kwa kuwa hawakusikia badala yake waliendelea kuzitumia barabara hizo na kusababisha changamoto kadhaa ikiwamo ajali.

Hata hivyo, bado viongozi wa Serikali hawajachoka safari hii amejitosa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo ambaye amevitaka vyombo vingine viache kutumia barabara za mwendokasi.

Jafo, ambaye ni mbunge wa Kisarawe (Pwani), amesema kumekuwa na ajali nyingi zinazojitokeza na kusababisha mabasi ya mwendokasi kupekekwa gereji mara kwa mara kwa ajili ya matengenezo. Ni kweli alichokisema Jafo kwa sababu hivi karibuni magari takribani 40 ya mwendokasi yalipelekwa gereji kwa ajili ya matengenezo hali hii ilisababisha uhaba mkubwa wa mabasi kwa watumiaji wa usafiri huo.

Uhaba huo ulichangia abiria wa maeneo mbalimbali hasa kituo kikuu cha Kimara kutumia muda mwingi vituoni kusubiri mabasi yaliyoelezwa kuwa machache.

Sisemi ajali za magari ya kawaida yanayopita katika barabara ya mwendokasi ndiyo yamechangia mabasi ya mwendokasi kupelekwa gereji la hasha, bali jambo hilo linaweza kuwa sababu ya mabasi ya kuharibika.

Tumeshuhudia miaka iliyopita hasa mwaka jana ajali mbalimbali zikitokea katika barabara hizo zikihusisha mabasi ya mwendokasi na magari ya kawaida yanayotumia barabara hiyo kinyume cha sheria.

Watanzania hasa wakazi wa Dar es Salaam, ifike mahali tuheshimu na kuyatii maagizo yanayotolewa na viongozi wa juu wa Serikali kuhusu matumizi ya jambo fulani ikiwamo barabara za mwendokasi.

Ni aibu kwetu, kwa sababu kiongozi wa Taifa anatoa agizo lakini linapuuzwa na baadhi ya wananchi na mwisho jambo hilo linaleta madhara kama ilivyotokea kwa dereva bodaboda na abiria wake walivyopoteza maisha baada ya chombo hicho kugongwa na basi la mwendokasi kwenye barabara hiyo.

Ukiona viongozi wanarudiarudia jambo mara kwa mara ujue bado kuna watu hawatii agizo hilo na ndio maana sasa ni jambo la kawaida kuona magari ya Serikali yakitumia barabara hizo.

Siyo hayo tu, bali hata yale yanayomilikiwa na vyombo vya dola ambayo baadhi ya wananchi wanasema yamekuwa mstari wa mbele kutumia barabara hizo badala kupita zile njia za kawaida.

Rais Magufuli alishakabidhi rungu hili kwa polisi wa kikosi cha usalama barabarani kuyakamata magari yanayokiuka taratibu kwa kupita kwenye barabara hizo. Ni vyema sasa hatua zichukuliwe.

Bakari Kiango ni mwandishi wa Mwananchi, 0719-999988