Jifunze tabia za waliofanikiwa ili na wewe ufanikiwe

Kuna kitu kimoja kikubwa kipo nyuma ya mabadiliko muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyafanya. Hata wewe ukihitaji kufanya mabadiliko basi utapaswa kuwa nacho. Na kitu hiki si kingine, bali ni tabia.

Tunaweza kutoa maana ya tabia kama mwenendo au matendo yanayojirudia kwa muda mrefu. Tabia hizi ni matendo ambayo huamua mafanikio yako.

Kwa kawaida mwenendo na matendo ya mafanikio huwa vigumu kuyajenga. Kuthibitisha hili, mshauri nasaha na mwandishi maarufu wa vitabu raia wa Canada, Robin Sharma aliwahi kusema tabia za watu waliofanikiwa ni ngumu kuzianzisha mwanzoni, ngumu zaidi katikati ila rahisi sana mwishoni.

Japo unahitaji kuwa na tabia za watu waliofanikiwa ili ufanikiwe, lakini usidhani tabia hizi ni rahisi kuwa nazo ingawa ukishazianzisha zinakuwa sehemu ya pili ya maisha yako. Yaani hutahitaji nguvu kuzikamilisha.

Chukulia mfano wa tabia yako ya kupiga mswaki. Tabia hii imeshakuwa sehemu ya maisha yako kiasi kwamba ukiamka asubuhi huhitaji kujiuliza juu ya suala hilo. Unapiga bila kukumbushwa.

Kabla sijaingia ndani zaidi kuzungumzia tabia hizi, tambua kuwa unahitaji siku 21 kuzijenga. Huu ndio muda ambao umethibitishwa kitalaamu na wanasaikolojia.

Zipo tabia muhimu zitakazokupeleka kwenye mafanikio uyatakayo. Kwanza ni kuamka mapema. Miaka mingi iliyopita aliyekuwa Rais wa Marekani, Benjamin Franklin aliwahi kusema kuwa kulala mapema na kuamka mapema kunamfanya mtu awe mwenye afya, tajiri na busara.

Tabia hii ya kuamka mapema ni ya kitajiri ambayo watu waliofanikiwa wamekuwa wakiishi kwa karne nyingi sasa. Na wewe ukitaka kwenda hatua kubwa maishani jifunze kuamka mapema kwani kuna faida nyingi za kufanya hivyo.

Faida tatu za awali za kuamka mapema ni kuwa na afya njema, utajiri na busara. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukiamka mapema utapata muda wa kufanya mazoezi hivyo kujiendeleza kimwili, utapata muda wa kuongeza maarifa kwa kusoma vitabu suala litakaloisaidia akili yako kuimarika na utapata muda wa kuwa peke yako, wasaa wa kujiendeleza kiroho.

Kuamka asubuhi pia kutakufanya ukamilishe shughuli zako mapema zaidi kuliko wengine maana utaanza majukumu ukiwa na muda wa kutosha. Upo usemi kuwa ndege wa asubuhi ndiye hupata chambo bora sana katika kusisitiza kuamka mapema.

Tabia nyingine muhimu kuwa nayo ni kusoma vitabu vingi kadri uwezavyo. Upo msemo kuwa ukitaka kumficha kitu Mwafrika basi kiandike kwenye kitabu. Aliyesema usemi huu alikuwa anajua kabisa kwamba kwenye vitabu kuna maarifa ya kutosha, hivyo wachache wanaoweza kukaa chini kwa nidhamu na kukisoma ndio wenye uwezo wa kuyapata na kunufaika nayo.

Sasa umefika wakati wako wa kuanza kusoma vitabu. Usikubali kufichwa kitu kitabuni kwa sababu ya uzembe wa kutopenda kujisomea.

Tenga muda na hakikisha unasoma vitabu kila siku. Kwa mwezi kiwango chako cha chini cha kusoma vitabu iwe walau kimoja.

Na kwa siku usisome chini ya kurasa kumi za kitabu. Kusoma kuna faida nyingi sana. Ikiwa ni pamoja na kukupa mawazo mapya, kuongeza uwezo wako wa kufikiri, kukukutanisha na watu na kukupeleka kwenye mazingira mapya na uliyoyazoea.

Tabia ya tatu inayoshikilia mafanikio yako ni uwezo wa kujiongoza. Kama mara nyingi huwa unasubiri ukumbushwe au usukumwe ndipo ufanyekazi ulizonazo, basi mafanikio yapo mbali nawe. Wanaofanikiwa hujisimamia na kufanya kila kitu kwa ratiba zao.

Huu ni wakati wako pia kuongeza juhudi na kujikumbusha mwenyewe kukamilisha majukumu yako bila kukumbushwa na yeyote. Jisimamie kwani watu wote waliofanikiwa wanajua wao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kutimiza wajibu wao.

Kuwa mtu wa matendo zaidi ya maneno. Matendo huongea zaidi ya maneno.

Dunia hii ina waongeaji wengi wasiotekeleza wayasemayo, jitofautishe nao. Ukiwa mtu wa matendo, tofauti na wengi walivyo, utafanikiwa.

Unaweza kukuta watu wanapiga hesabu inayopatikana kwenye biashara kwa maneno mwaka hadi mwaka.

Wewe ukipiga hesabu hizi kwa kufanya na kuleta matokeo wanayojadili ndio itakuwa tofauti yako na mafanikio yako yatadhihirika.

Mwaka 2019 ndio kwanza umeanza. Unao muda wa kutosha kubadili tabia zako ili kuyakaribisha mafanikio yako. Ukibadili tabia zako, utajihakikishia kupata uyatakayo kwa wakati.

Mwandishi ni mdau wa maendeleo. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa namba 0755-848 391