Kauli za kudhibiti mafuriko Dar zisiwe za kisiasa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema Serikali imefanikiwa kupata dola 100 milioni za Kimarekani (sawa na takriban Sh220 bilioni za Kitanzania) kwa ajili ya kumaliza tatizo sugu la mafuriko katika bonde la Mto Msimbazi.

Makonda alitoa kauli hiyo juzi baada ya kufanya ziara ya kukagua athari za mvua zilizonyesha mfululizo kwa zaidi ya wiki.

Alisema wataalamu wa maafa wa ofisi yake wamepiga picha eneo linalozungukwa na Mto Msimbazi kupata taswira halisi itakayowezesha kupata mkakati wa kuikabili changamoto ya mafuriko katika makazi.

Hatupingani na mkakati wa Makonda kwa kuwa tatizo la mafuriko jijini Dar es Salaam limesababisha vifo pamoja na watu kupoteza mali zao.

Itakumbukwa Aprili 2014 jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na mafuriko na watu zaidi ya 13 walipoteza maisha.

Mbali na watu kupoteza maisha, mvua hiyo iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo pia ilisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja ikiwamo kukata mawasiliano.

Tunajua kuwa huu si mkakati wa kwanza kuelezwa na viongozi wa juu serikalini kuhusu mpango wa kudhibiti mafuriko.

Mwaka jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliliambia Bunge kwamba tatizo la mafuriko la jiji la Dar es Salaam linatokana na ramani ya mipango miji kutofanyiwa marekebisho kwa muda mrefu.

Lukuvi alisema kiutaratibu ramani za mipango miji hupitiwa kila baada ya miaka sita, lakini ramani ya Jiji la Dar es Salaam haijapitiwa tangu utawala wa awamu ya kwanza.

Alilihakikishia Bunge kwamba katika kudhibiti mafuriko hayo Serikali imechora ramani ya mipango miji mpya kwa Jiji la Dar es Salaam na kwamba ilikuwa inapitiwa.

Tunachosema suala la mafuriko mkoani Dar es Salaam limekuwa sugu na mikakati yote iliyozungumzwa na viongozi haijafanyiwa kazi na haifahamiki itatekelezwa lini.

Mkoa wa Dar es Salaam inaponyesha mvua inakuwa ni adha kwa wakazi wake huku wananchi wa maeneo ya mabondeni wakiathirika zaidi baada ya nyumba zao kujaa maji.

Imezoeleka kuwaona viongozi wa Serikali wakiibuka na kuzungumzia kwa ustadi kuhusu namna bora ya kudhibiti mafuriko pale yanapotokea, lakini mvua zinapoisha na wao huishia.

Kwa mtindo huo tatizo la mafuriko linaonekana kuchukuliwa kisiasa zaidi kuliko kutafuta namna bora ya kuwanusuru wakazi wa Dar es Salaam.

Tunaamini mpango wa Makonda utatekelezwa kwa dhati na pengine anaweza kuweka historia kama atatekeleza kwa ufanisi mkakati wake.

Kuna methali inasema usipoziba ufa utajenga ukuta, ni wazi mafuriko haya yamekuwa yakileta hasara kwa wananchi na Serikali yenyewe kwa kuwa imeshindikana kuyadhibiti.

Hivyo, kuepuka hasara hizi za mara kwa mara ni vema mkakati uliotangazwa na Makonda ukafanyika kwa ufanisi na kwa haraka, kwa kuwa fedha zipo.

Hatuoni sababu ya wakazi wa Dar es Salaam kuendelea kuteseka na mafuriko, pia hatuoni sababu kwa Serikali kutumia fedha nyingi mara kwa mara kurekebisha miundombinu inayoharibiwa na mafuriko yanayoweza kuzuilika. Tunamuomba Makonda atengeneze zawadi atakayoendelea kukumbukwa na wakazi wa Dar es Salaam ambao kwa miaka kadhaa wamekuwa wakiteseka na mafuriko yanayotokana na maji ya mvua.

imani ya wakazi wa Dar es Salaam ni kwamba mkakati huu hautakuwa siasa tena, maadam fedha zimepatikana kazi ianze mapema.