UCHAMBUZI: Kwa nini bei ya taulo za kike haishuki licha ya kuondolewa VAT?

Juni 14 mwaka jana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitangaza kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike (sodo) zinazoagizwa nje ya nchi.

Serikali haikujali kiasi kikubwa cha fedha iliyokuwa inapata kutokana na bidhaa hizo ambako Sh3 bilioni zilikusanywa mwaka 2016/17 na Sh2.5 bilioni kwa mwaka wa fedha 2017/18 kabla ya kodi hizo kuondolewa Juni, 2018, kutokana na umuhimu wake iliondoa kodi hiyo.

Tangazo hilo lilipokewa kwa shangwe na watu mbalimbali wakiwamo wabunge wanawake ambao walipiga vigelegele kuonyesha furaha yao.

Dk Mpango alitangaza mapendekezo ya msamaha huo wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2018/19.

Wakati akitangaza msamaha huo, aliweka wazi kuwa anaondoa kodi hiyo kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa bei nafuu ili kulinda afya ya mama na mtoto wa kike hasa walio vijijini na shuleni.

Maombi na dhamira ya kuondolewa kwa kodi hiyo vilianza chinichini lakini Januari 22, Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza alipeleka hoja binafsi bungeni kuomba ipitishwe sheria ya kugawa bure taulo hizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo, hoja hiyo ilikataliwa kutokana na kifungu kinacholikataza Bunge kujihusisha na kubadilisha kodi isipokuwa kupunguza.

Aprili wakati wa Bunge la Bajeti, Peneza aliuliza tena swali kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka kujua kama Serikali inaweza kuondoa kodi kwenye taulo hizo za kike.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema Serikali ina utaratibu wake wa kuondoa kodi kwenye bidhaa zinazoleta tija.

Lakini katika kuonyesha kuwa jambo hilo linahitaji kupatiwa ufumbuzi alizitaka wizara ya Fedha na Tamisemi kuona namna watakavyokaa kwa pamoja na kujua jinsi ya kupunguza bei kwenye bidhaa hizo.

Pamoja na juhudi zote hizo, bidhaa hiyo bado haijapungua bei licha ya kuondolewa VAT.

Bidhaa hiyo bado ina bei kubwa kwani kwa mijini inapatikana kuanzia Sh2,500 hadi Sh4,000 huku baadhi ya mikoa ikiwa ni Sh3,000 hadi Sh5,000.

Kwa maana hiyo, hata baada ya kuondolewa VAT bado zipo juu na kuna baadhi ya maeneo hazipatikani.

Jambo linalotakiwa ni mamlaka husika ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujipanga kufuatilia ili kuhakikisha zinapatikana kwa gharama nafuu kama lengo la kuondolewa VAT lilivyokusudiwa. Tofauti na hapo, itakuwa kazi bure na wanafunzi na wanawake wasiokuwa na uwezo wataendelea kuteseka kwa kukosa bidhaa hiyo muhimu kwa sababu inavyoonekana anayenufaika kwa kuondolewa kwa kodi hiyo ni anayeagiza kwani zinapofika kwa mtumiaji ambaye ni mlengwa bei iko juu kama zamani.

Hayo hayakuwa malengo ya Serikali, bilioni hizo zilizosamehewa kodi zilitakiwa zikamnufaishe mwanamke mlengwa na sio kinyume chake.

ushauri wangu ni kwamba wadau husika wakutane na waagizaji ili wajue wanakwama wapi kupunguza bei ya bidhaa hiyo, kwa sababu watumiaji bado wanaipata kwa bei ya juu.

Bidhaa hiyo si tu inatumiwa na wanawake kujihifadhi na kupata ujasiri, bali pia ni muhimu kwa mustakabali wao ikiwamo wa elimu kwa wasichana.

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unicef), linasema karibu wasichana 850,000 hushindwa kuhudhuria masomo yao kwa wiki sita ndani ya mwaka hapa nchini, huku kina mama wengi wakishindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa sababu ya kukosa bidhaa hiyo ya kujihifadhi.

Hapo unaona athari ya moja kwa moja ambayo huwapata wasichana na wanawake wanapokuwa kwenye hedhi na wakakosa bidhaa bora ya kujihifadhi.

Serikali imetimiza wajibu wake kwa kuondoa kodi hiyo, lakini hiyo haitoshi, ishirikiane na mamlaka nyingine kuangalia hili na watimize wajibu wao kwa nafasi zao.

Hawa ni pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), vyama vinavyohusika na afya salama ya hedhi kwa ustawi wa wanawake kwa ujumla.

Wapo wasichana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na kukosa vifaa salama vya kujihifadhi wanapokuwa na hedhi na kulazimika kuacha shule.

Hata wabunge wanawake walipiga vigelegele baada ya Dk Mpango kutangaza kuondoa kodi hiyo, sababu ya furaha hiyo ni kwa kuwa walitambua namna mwanamke anapokuwa kwenye hedhi anavyohitaji bidhaa salama kwa ajili ya kujisitiri.

Mamlaka zisimamie suala la kupunguza bei ya bidhaa hiyo. Wahurumieni wasichana wanaokosa masomo, wahurumieni kina mama wanaoshindwa kutimiza majukumu yao ya kila siku.

Wadau mbalimbali hili nalo linahitaji kupaziwa sauti ili lifikie kikomo.