Kwa nini tujali kodi kuliko madhara ya kamari?

Thursday March 14 2019

 

By MOHAMMED ISSA

Machi 4, kuna vyombo vya habari viliandika kuhusu michezo ya kubahatisha kuiingizia Serikali mabilioni ya fedha.

Sambamba na kuingiza fedha Hazina, michezo hiyo ya kubahatisha au kwa jina lingine kamari, ikatajwa kuwa inaajiri watu wapatao 20,000.

Kama haitoshi tukaelezwa kuwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imejipanga kupanua sekta hiyo na kuleta ufanisi katika kukusanya mapato kwa kuweka mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Ukiangalia hoja zilizowasilishwa katika kuitetea kamari iendelee nchini ni kwamba Mosi inaliingiza Taifa kodi na pili, kamari inaajiri watu wapatao 20,000.

Kwa sekta ya kamari kuajiri watu 20,000 nchini panakusudiwa kupingana na hoja kwamba inaleta uvivu na inauza nguvu kazi ya Taifa maana kama inaleta uvivu mbona sekta hiyo imeajiri watu wote hao?

Kwa kutaja mabilioni yanayopatikana ni kama vile tunaambiwa mtapigaje marufuku kitu kinachoiingizia Serikali mapato makubwa kiasi hiki? Mkipiga marufuku kamari Taifa litapoteza mapato hayo na ajira hizo.

Kwa hoja hizi wahusika wanakusudia kuishawishi Serikali ione kwamba kupiga marufuku kamari kutakuwa na madhara makubwa kwa Taifa.

Hatuamini kwamba watu wa bodi hawajui madhara ya kamari kiafya, kijamii na kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na hata kielimu pia.

Ndiyo maana tunauliza hivi tumefikia kujali kodi kuliko madhara ya kamari?

Kama ni hoja ya kuiingizia Serikali pesa, mbona tumepiga marufuku mirungi, bangi, gongo na dawa za kulevya? Kwani vingeruhusiwa visingeliingizia Taifa mabilioni au hata matrilioni ya pesa?

Kupiga kampeni kuhamasisha kitu au bidhaa fulani itumike kwa kuangalia faida zake kiuchumi, si vyema bali kuangalia madhara yake.

Ni kwa kuzingatia kanuni hii ndiyo maana mataifa mbalimbali duniani kote yanapambana na biashara ya dawa za kulevya ambayo ingeachwa iwe huru ingeyaingizia matrilioni ya dola za Marekani.

Hakuna nchi duniani iliyohalalisha biashara ya dawa za kulevya hata iwe masikini namna gani, kwa sababu madhara yake ni makubwa kuliko manufaa yanayopatikana kwa mapato.

Ni kwa kutumia kanuni hii ya “madhara yake ni makubwa kuliko manufaa” ndiyo maana Serikali zote duniani zimeharamisha vitu mbalimbali pamoja na kwamba vina manufaa kwa jamii.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Makosa ya Jinai (UNODC), biashara ya dawa za kulevya duniani mwaka 2003 ilikuwa na thamani ya Sh690 trilioni.

Takwimu hizo zinatosha kupata picha kuwa biashara hiyo inaingiza pesa nyingi, lakini pamoja na hayo haijawahi kuhalalishwa kwa kigezo cha kuingiza kwake mapato makubwa.

Kama hivyo ndivyo kwa nini hatuhalalishi biashara ya dawa ya kulevya nchini kwa kigezo cha mapato kama tulivyofanya kwa kamari?

Bila shaka tumezingatia kwa busara zetu kuwa pamoja na uwezekano mkubwa wa kuingiza pesa nyingi na kuajiri Watanzania wengi kwa biashara hiyo, tumeona ina madhara makubwa kuliko manufaa.

Sambamba na hilo, biashara ya mirungi Kenya huliingiza Taifa hilo Dola 400,000 za Marekani kwa siku (sawa na Sh 858 milioni).

Kwa hiyo kwa mwezi itakuwa Sh25.7 bilioni sawa na Sh308.4 bilioni kwa mwaka.

Kama ni kuangalia kamari inaingiza Sh78 bilioni kwa mwaka, mbona hatuiigi Kenya tukahalalisha biashara ya mirungi ambayo ingetuingizia pesa nyingi na kuajiri watu wengi zaidi kuliko kamari?

Bila shaka kwa kuharamisha biashara ya mirungi nchini tumezingatia madhara ya mirungi, ni zaidi kuliko manufaa yanayotokana na mapato yake.

Mbali na madhara ya kamari kiuchumi ambapo mcheza kamari hufilisika hadi kufikia kuuza mali zake, imebainika pia kuwa na madhara kiafya.

Moja ya madhara hayo ni ugonjwa uitwao ADHD (Attention Deficit Hyperactivity Disorder) yaani mtu kukosa umakini na utulivu katika mambo anayoyafanya.

Madhara mengine ni pamoja na kufikwa na ugonjwa wa sonona (depression), kukosa usingizi (insomnia), hasira zisizo na sababu na hisia za kutaka kujiua.

Kamari hutishia maendeleo ya vijana kielimu kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Tabia zinazozalika kwa wanafunzi kucheza kamari ni pamoja na utoro au kuacha kabisa masomo.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kijamii.