Serikali iharakishe uanzishwaji wa bima ya takaful

Wananchi mbalimbali wamekuwa wakihoji hatima ya uundwaji wa kanuni zitakazoruhusu uanzishwaji wa bima ya Takaful hapa nchini.

Wananchi hao wamekuwa wakitaka kujua sababu za kuchelewa kukamilika kwa mchakato huo ambao umechukua muda mrefu, bila kuleta matokeo chanya, jambo ambalo limewaacha wananchi hao gizani wakiwa hawajui nini kinaendelea.

Katika vipindi tofauti, Serikali, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) mekuwa ikitoa ahadi mbalimbali kuhusu uwezekano wa kukamilika kwa kanuni hizo mapema.

Katika moja ya ahadi hizo ni ile ya mwaka 2015 ambapo aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Tira, Israel Kamuzora, alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema kuwa mchakato wa uundwaji wa kanuni hizo upo katika ‘hatua za mwisho.’

Tira ilifanya utafiti mwaka 2012 juu ya Takaful chini ya ushauri wa Benki ya Dunia na wataalamu kutoka Malaysia na wale wa Kituo cha Masuala ya Huduma za Kifedha za Kiislamu na Ushauri hapa nchini (CIFCA) na kutoa mapendekezo serikalini.

Lakini pia Tira ilipendekeza zitungwe kanuni za kuruhusu aina hiyo ya bima.

Takaful ni aina ya bima ambayo huendeshwa kwa misingi ya kusadiana kufidia majanga yanayowakumba wahusika wanaokata bima hiyo. Mtu anapokata bima anakuwa amejiunga na Takaful na iwapo hatopata janga katika mali aliyoiwekea bima, fedha zake ukifika mwisho wa mwaka zitaendelea tena kuwa bima kwake.

Ili kufidia mfuko wa bima usifilisike, msimamizi wa bima hizo huruhusiwa kuwekeza fedha hizo ambazo huwa ni nyingi sana na faida itakayopatikana kila mwana bima ya hupata gawio.

Tayari baadhi ya wadau wamejipanga kuanzisha kampuni za kutoa huduma ya bima ya Takaful.

Kuna tofauti kadhaa katika utoaji wa huduma ya takaful ukilinganisha na bima za kawaida. Katika bima hii inayofuata misingi ya dini ya Kiislamu, mwanachama ana haki ya kupata gawio kwa kiasi ambacho kinabaki kutokana na fedha zilizokusanywa kwa mwaka, jambo ambalo halipo katika bima za kawaida.

Bima ya Takaful hairuhusu mtu mmoja au taasisi kunufaika peke yake. Wanachama wanaochangia katika mfuko ndiyo wanufaika wakubwa.

Katika Takaful, mwanachama akipata tatizo atalipwa kulingana na tatizo lake, lakini mwisho wa mwaka waendeshaji watapiga mahesabu na kama kuna kiasi ambacho kimebaki ni mali ya wanachama.

Kuhusu suala la uendeshaji, taasisi ya bima ya Kiislamu itaendeshwa zaidi kupitia ada zitakazolipwa na wanachama wake.

Faida nyingine ya bima ya Takaful ni kuepusha watu dhidi ya riba. Inajulikana wazi kuwa, baadhi ya watu hawapendi kujihusisha na shughuli za kiuchumi zenye riba ndani yake, lakini Tanzania kwa sasa hakuna mbadala wa taasisi ya bima isiyojihusisha na riba.

Malengo makuu ya uwepo wa bima ya aina yeyote ni kumnusuru yule aliyekata bima asipate hasara na kuyumba pindi anapopata matatizo ama majanga yasiyotarajiwa kumtokea.

Aidha, bima ni kinga muhimu inayomuacha mwenye kuikata akiwa na amani ya moyo kwa kuweza kuwa huru kufanya shughuli zake bila kuhofia majanga yanayoweza kutokea mbele. Baadhi ya wataalamu wameita bima, akiba isiyooza ambayo itatumika katika kipindi ambacho unahitaji msaada wa haraka wa kukuvusha kutoka sehemu moja kwenda nyingine baada ya mkwamo usiotarajiwa katika maisha yako ya kila siku.

Serikali yetu iko katika kujenga uchumi wa viwanda. Moja ya vipengele muhimu katika uchumi huo ni upatikanaji mpana wa huduma za kifeha na bima kwa wananchi wengi.

Suala la uanzishwaji wa bima ya Takaful nchini linakuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu tayari kuna benki na taasisi za kifedha kama vile Saccos zinatoa huduma za kifedha za Kiislamu ambazo huenda sambamba na bima ya Takaful.

Kuanzishwa kwa Takaful kutachochea ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuvutia wawekezaji wanaohitaji uwepo wa huduma hizo, kuingiza fedha serikalini kupitia ukataji wa leseni za Takaful, kupanuka kwa huduma za bima na hivyo kukuza uchumi.

Katika uchumi wa viwanda, kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia huduma za kibenki na bima ni jambo muhimu sana kwa sababu itahakikisha fedha inaingia katika mzunguko rasmi na haibakii mikononi mwa watu.

Ni vema basi Serikali yetu Ikaharakisha mchakato wa kuanzishwa huduma za bima ya Takaful nchini ili kuwahudumia wananchi wake wanaohitaji huduma hizo.

Mwandishi anapatikana kwa barua pepe: [email protected]