Serikali iwasaidie wasafirishaji wa wanyama nje

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla

Uamuzi wa Serikali wa kupiga marufuku usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi, umewaathiri wananchi wengi waliokuwa wakifanya biashara hiyo.

Wakati wa kikao cha Bunge lililopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ndiye aliyepigilia msumari wa mwisho kwa kutangaza uamuzi wa kupiga marufuku biashara hiyo.

Dk Kigwangalla alitoa tangazo hilo wakati wafanyabiashara hao wakisubiri utaratibu mpya baada ya wizara hiyo kusimamisha usafirishaji wa viumbe pori hai nje ya nchi kwa miaka mitatu iliyokuwa inaishia Mei, mwaka huu.

Serikali ilifikia uamuzi huo kwa ajili ya kutoa muda kwa idara ya wanyamapori kupanga namna ya kufanya biashara hiyo kwa usalama, uhakika na kwa kufuata sheria. Maelezo mengine yaliyotolewa ni kwamba wanyama wa Tanzania wamekuwa wakikamatwa katika bandari na viwanja vya ndege vya nje ya nchi wakiwa hawajafuata taratibu za usafirishaji.

Uamuzi wa kuzia biashara hiyo ulichukuliwa wakati wafanyabiashara wengine wakiwa tayari wamelipia gharama zote wizarani ikiwamo vibali.

Tunafahamu biashara ya kusafirisha wanyama hai nje ya nchi inahitaji mtaji mkubwa, hivyo kusimamisha ghafla kunaleta maumivu ya kiuchumi kwa wahusika ikiwamo hatari ya kufilisika.

Lakini, kuna wale ambao wamechukua mikopo benki na taasisi zingine za fedha, ka hiyo kabla ya Serikali kuchukua uamuzi huo ilipaswa kuwaandalia mazingira mazuri wananchi hawa japo kwa kuwapa muda wa kuuza walichokuwa nacho.

Tunaamini uamuzi wa Serikali hauna lengo baya kwa wananchi wake, ila tunachokiona umefanyika kwa ghafla mno wakati wafanyabiashara wengine wakiwa kwenye hatua za mwisho kusafirisha viumbe hao.

Ni vyema Serikali ikawafikiria hata hao waliokuwa wameingia gharama za usafirishaji, ikiwamo kulipa vibali, lakini pia na wale ambao wana mikopo iliyotokana na kufanya biashara hiyo.

Tunaona wafanyabiashara hawa wanastahiki kulipwa kwa kuwa uamuzi wa awali ulikuwa ni kusubiri utaratibu wa idara ya wanyamapori kuhusu namna bora ya usafirishaji wa wanyama hao, lakini baada ya kusubiri kwa muda wote huo Serikali ikaja na uamuzi mwingine wa kupiga marufuku.

Wananchi walikuwa wakinufaika na biashara hiyo, pia Serikali ilinufaika kwa kupata kodi na mapato mengine.

Kwa mfano, wafugaji 156 wa vipepeo katika hifadhi ya asili ya Amani iliyopo Tanga, kabla ya zuio hilo walikuwa wakisafirisha nje ya nchi vipepeo vyenye thamani ya dola za Marekani 90,000 huku wakijipatia Sh500 milioni kwa mwaka.

Amani kulikuwa na vijiji sita vinavyofuga vipepeo aina 31 wanaouzwa katika nchi za Ulaya na Marekani, hivyo ni wazi uchumi uliokuwa ukiimarika kwenye vijiji hivyo kutokana na biashara hiyo sasa haupo.

Ushauri wetu kwa Serikali iangalie namna bora ya kuweza kuwafidia wananchi hao waliowekeza katika biashara ya usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Tunafahamu Serikali ni sikivu inayopenda kusaidia wananchi wanyonge, hivyo kwa wafanyabiashara hawa ni vyema wakaangaliwa kwa namna ya pekee.

Kwanza kwa uvumilivu wao wa kusubiri kwa muda mrefu wakiwa na matumaini ya kuendelea na biashara yao, hasara wanayoipata na wale wenye mikopo benki wafikiriwe namna ya kuwanusuru na hatari ya kufilisiwa.