UCHAMBUZI: Tunaweza kuyaepuka magonjwa haya kwa urahisi

Saturday June 15 2019

 

By MUHIMGO MWENEZI

Siku hizi kumekuwa na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (NCD’s), huku baadhi wakiwa hawajui kama wanayo na wanaendelea na mitindo yao ya maisha ambayo wanapaswa kuibadili.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wamekuwa wakitueleza mara kwa mara nanma ya kuyaepuka magonjwa hayo kwa usalama wa afya zetu.

Ni lazima tuzitunze afya zetu kwa kuwa ndiyo kitu cha kwanza muhimu katika maisha ya binadamu yeyote yule.

Mtu anapokuwa na afya njema, atakuwa na nguvu za kumuwezesha kufanya kazi za uzalishaji mali na kuongeza pato la Taifa na familia kwa jumla.

Baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na shinikizo la damu, saratani na kisukari.

Magonjwa haya humuathiri mtu kwa kipindi kirefu na kadri siku zinavyoendelea na ugonjwa huendelea kukua mwilini taratibu.

Advertisement

Wakati mwingine magonjwa haya yasiyoambukiza husababisha vifo mapema yaani tangu mtu anapogundulika kuugua kwa sababu anakuwa amechelewa kupata tiba.

Makundi ambayo yako hatarini kupata magonjwa haya ni pamoja na vijana, watoto na watu wazima.

Watoto wapo hatarini kutokana na kupewa vyakula visivyokuwa na virutubisho pamoja na kutozingatia mlo sahihi.

Vijana na watu wazima nao mlo wao hauzingatii taratibu za lishe bora, pia ni wavivu wa kufanya mazoezi hivyo kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa hayo.

Hata wataalamu wa afya wamekuwa wakieleza kuwa mitindo ya maisha tuliyonayo ya kutofanya mazoezi pamoja na aina za vyakula tunavyokuwa vyenye mafuta na wanga ndiyo sababu kuu ya magonjwa hayo.

Ni kawaida kumkuta mtu anakula chakula kimesheni wanga na protini tu, kwa maana ya ugali na nyama choma huku pembeni kukiwa na soda.

Katika sahani hiyo hakuna mboga za majani wala matunda au juisi halisi pembeni.

Mbali na vyakula na mazoezi, taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2002, inaeleza kuwa matumizi ya sigara, unywaji wa pombe na uzito mkubwa huchangia magonjwa hayo.

Kuna presha ya asili ambayo chanzo chake hakifahamiki, lakini tatizo la kimazingira kama chakula, mazoezi zina nafasi kubwa katika mwili wa mgonjwa.

Aina ya pili ya presha ni ile inayosababishwa na tatizo kwenye mwili kwa mfano kupungua unene wa mishipa fulani ya damu, matatizo ya tezi, matatizo ya figo, matumizi ya dawa, madawa ya kulevya au kemikali.

Hivi sasa idadi kubwa ya Watanzania wanaofika hospitalini wameonekana kuwa na magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu pamoja na kuwa na uzito mkubwa huku wataalamu wa afya wakionya kuwa kama watu hawatabadilisha tabia za mwenendo wa maisha yao kuna hatari ya wengi kuugua.

Ni jukumu la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kuendelea kufanya utafiti wa magonjwa yasiyoambukiza kwa sababu watu wengi wanaugua magonjwa hayo kwa sasa.

Daktari wa magonjwa yasiyoambukiza katika Hospitali ya Wilaya Kibondo mkoani Kigoma, anasema ulaji wa vyakula usiozingatia mtiririko mzuri ni chanzo cha magonjwa ya kisukari na presha.

‘‘Watu wengi hawafanyi mazoezi ya mwili, wanakula vyakula hovyo, tena vile vya kusindikwa badala ya kutumia vyakula vya asili, mtu anaona akinunua vyakula vya asili atafikiriwa katika jamii kuwa kaishiwa, kwa hiyo mpangilio wa vyakula usiozingatia lishe bora ni changamoto.”

Hayo yote yametokea kwa sababu Watanzania tunapenda kuiga, badala ya kula vyakula vyenye lishe tunatilia mkazo kwenye nyama choma, chipsi mayai na soda ambazo pia zina kiwango kikubwa cha sukari.

Ni vyema tukajijengea utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili tuweze kupata ushauri kwa wataalamu pindi tunapogundulika tuna tatizo lolote katika miili yetu.

Pia, hata gharama za matibabu huwa ndogo na hata kuweza kudhibiti aina ya ugonjwa usiendelee kuliko kukaa hadi ugonjwa ujitokeze wenyewe matokeo yake tatizo linakuwa kubwa.

Ni wachache sana wenye tabia ya kwenda kwa daktari kupima afya zao hata kama hawahisi chochote katika miili yao; na hivyo ndivyo inavyotakiwa.

Upimaji wa afya mara kwa mara ni muhimu kwa kila mtu, haijalishi tajiri wala masikini.

Mwandishi wa uchambuzi huu anapatikana kwa namba 0756906770 au 0683848097