Ukitulia utakabili vikwazo na utafanikisha malengo yako

Kila mtu anayeishi kwenye dunia hii ana ndoto au alikuwa nayo alipokuwa mtoto.

Siyo jambo la ajabu kusikia mtoto anasema ninataka kuwa daktari, ninataka kuwa baba bora kabisa ninayejali familia, ninataka kuwa tajiri.

Pengine utasikia mtu anasema, nina ndoto ya kuwa msanii mkubwa, mfanyabiashara nguli au mwandishi maarufu.

Watoto ndiyo wanaongoza kwa kuwa na ndoto kubwa namna hii. Kwa asili, binadamu huwa tunapenda vitu vizuri.

Hakuna mtu ambaye hapendi kuishi kwenye nyumba nzuri au hapendi kuwa na fedha za kutosha. Kila mtu hutamani kuwa na uwezo wa kununua chochote atakacho.

Kabla sijaendelea, napenda kukwambia unastahili kupata vitu hivi, unastahili kuwa na afya njema, unastahili kuwa na maisha bora.

Vitu hivi ni haki ya msingi kabisa ya kuzaliwa. Ila tofauti kati ya haki hii na nyinginezo ni kwamba, unalazimika kuweka juhudi, kuwa na nidhamu na kuweka malengo makubwa ili kuipata.

Haki yako ya mafanikio hauipati kkwamba kwenda mahakamani na wala haki hii hailindwi na vyombo vya usalama wa raia kama polisi.

Haki hii unaipata kwa kuamua kutoa thamani kwa jamii, kutatua matatizo ya watu na kuishi ndani ya vipaji vyako.

Sasa kuna vikwazo ambavyo huwa vinawazuia watu kupata haki yao ya kufanikiwa. Na vikwazo hivi ndivyo napenda niviongelee kwa undani.

Kwanza ni kujilinganisha na wengine. Wewe ni mtu wa kipekee sana, wala hakuna unayeweza kujifananisha naye.

Tatizo kubwa ni kutaka kujilinganisha na wengine.

Ukianza kufananisha mafanikio yako na watu wengine ni chanzo cha kushindwa. Maana kila mtu ana njia yake anayopitia kufikia kilele cha mafanikio.

Cha ajabu zaidi ni pale unapoanza kujilinganisha na watu wengine kwa mambo ambayo huwezi kabisa kuyabadili.

Mfano eti unaanza kujiona wewe ni mfupi. Unaanza kutamani ungekuwa mrefu kama fulani. Huu ni upotezaji wa muda, maana kitu kama hiki huwezi kukibadili kamwe.

Ngoja nikwambie kitu, kuna sababu kubwa sana ya kwa nini umezaliwa katika familia fulani, katika mazingira fulani, ukasoma shule fulani.

Kuna sababu kubwa kwa nini una vipaji ulivyo navyo. Inawezekana kulikuwa na mpango kutoka kwa Mungu uliokutaka usome shule fulani ili ukutane na mtu fulani na hata ikija fursa basi uwe ushakutana na mzunguko wa watu unaowahitaji.

Kwa hiyo usianze kujilinganisha na mwingine, fursa zako ni za kipekee sana. Hakuna mwenye historia kama ya kwako. Hakuna mwenye ujuzi kama wa kwako. Ni wewe tu.

Kwa hiyo itumie fursa hii vizuri.Kaa chini na uandike vitu unavyojua unaweza kuvifanya kwa upekee sana.

Andika, hata kama ni vidogo. Kisha anza kuvifanyia kazi kuvikuza. Inawezekana unaweza kuwasiliana na watu kwa namna ya kipekee. Inawezekana pia una uwezo wa kuinadi biashara kwa namna ya kipekee.

Pia, unaweza kufanya kazi hata bila kusukumwa na mtu. Huu ndiyo upekee wako, huyu ndiye wewe. Jikubali kisha songa mbele.

Suala jingine unalotakiwa kulifanyia kazi ni kutaka kuishi kama wengine. Hili si jambo zuri kulifanya, usitake kuyafananisha maisha yako na ya wengine.

Kwanza kabisa nashukuru ukuaji wa teknolojia umerahisisha mambo mengi. Ila sasa umewapoteza watu na kuwafanya wasiishi kwa uhalisia.

Kwa sasa ukiangalia kwenye mitandao unaona kila anayeweka picha yupo maeneo mazuri ya starehe au watoto wa mjini wanaita kula bata kwenye hoteli kubwa au kwenye vivutio vizuri. Hakuna anayepiga picha akiwa kwenye nyumba ya nyasi hata kama ndiyo uhalisia wake.

Sasa wewe ukiiga vitu hivi na kuvitaka viwe sehemu ya maisha yako, utapoteza pesa, muda na nguvu ambayo ungetumia kutimiza ndoto zako.

Ukianza kufuatilia maisha ya mtu fulani anaishi na nani na uhusiano wao ukoje, ni upotezaji wa muda ambao ungeutumia kutimiza ndoto zako.

Kumbuka ndoto zako ni zako. Wala hakuna atayekuonea huruma katika kuzitimiza.

Unaweza kuwa unavyotaka kama utaamua. Ila kwa kufuatilia na kuiga maisha ya watu wengine, kiukweli utachelewa sana kutimiza ndoto zako.

Hata hivyo, hebu jiulize, unaiga maisha ya mtu una jua amefikaje hapo alipo? Kila mja ana njia zake za kufanikisha maisha hivyo nawe pambana.

Jikite kwenye eneo lako usimamie rasilimali ulizonazo kufanikisha ukitakacho. Usiige kwa wengine.

Mwandishi ni mdau wa maendeleo. Anapatikana kwa namba 0755 848 391