Ushirika una nafasi kubwa kupunguza umaskini nchini

Ushirika ni moja kati ya nyenzo muhimu za kupambana na kupunguza umaskini kwa watu wa kipato cha chini. Ushirika unaruhusu umiliki wa rasilimali ambazo zinafanyiwa uamuzi wa pamoja na kunufaisha wengi. Hili linawezekana kuanzia kwenye kilimo, masoko, fedha hata mambo mengi mengine yanayohusu ujasiriamali.

Kutokana na malengo yanayowekwa na Serikali hata yale ya Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu (SDG), nfasi ya ushirika inaonekana dhahiri.

Endapo vijana, wanawake na wajasiriamali wataungana kupitia vyama vya ushirika wakihamasishana kufanyakazi kwa juhudi huku wakipeana fursa za masoko na elimu ya uzalishaji wa bidhaa za aina mbalimbali, wengi watapenda kujiunga.

Lakini, kama zilivyo sekta nyingine, kuna umuhimu wa kuangalia baadhi ya maeneo ili kutengeneza msingi mzuri wa biashara kwa ushirika kujiendesha kitaasisi na kuwashawishi wanachama kuwa ushirika ni biashara nzuri.

Matumizi mazuri ya fedha ni moja kati ya eneo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa na malalamiko yanayoleta sintofahamu miongoni mwa wanachama wa ushirika.

Matumizi mabovu ya fedha yamekuwa yakiathiri vyama vya ushirika vya mazao na vile vya kuweka na kukopa. Matumizi haya yamekuwa yakitokana na uamuzi wa viongozi na watendaji wa vyama ambao wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa manufaa binafsi.

Kwa kiasi kikubwa, matumizi hayo, yanatafuna misingi ya ushirika kujiendesha kibiashara kutokana na kupoteza mtaji hasa fedha za uendeshaji.

Ili kukabiliana na baadhi ya changamoto, inapendekezwa kutumia wataalamu wa ushirika kusimamia taasisi hizo. Kutokana na ukweli kwamba ushirika ni eneo la aina yake na linahitaji wataalamu wake ni muhimu kuwa nao katika ngazi za utendaji wa chama.

Kwa mfano, Saccos zinahitaji wataalamu wa sekta ndogo za fedha hivyo ni muhimu kuwatumia wale wenye elimu ya taasisi ndogo za fedha ili kufanya chama kuwa eneo la ubunifu, ushindani wa kibiashara na kuwarithisha wateja wake kwa viwango vinavyotakiwa.

Ukiacha watalaamu, taasisi za fedha sasa hivi zimeanzisha akaunti maalumu kwa ajili ya vikundi vya wajasiriamali ambazo kila muamala unaofanyika kila mmoja anapata taarifa. Kwa kutumia akaunti hizi, itaongeza urahisi wa kusimamia fedha za ushirika kutumika bila ridhaa ya wengi.

Kuwekeza kwenye utafiti ili kujiwekea mazingira mazuri ya kutambua njia za ubunifu, ushindani kutoka kwenye taasisi kubwa za fedha kwa upande wa saccos kama zilivyokuwa sekta nyingine.

Utafiti unasaidia kufanikisha mambo mengi ya kitaasisi hivyo ni vema kuwekeza zaidi kwenye eneo hili ili kuja na bidhaa na huduma zenye nguvu ya kushindana na taasisi kubwa za fedha.ikumbukwe, utafiti ni nguzo kwenye mipango na maamuzi ya kibiashara ya ushirika.

Uongozi mzuri, unaoanzia kwenye bodi za vyama vya ushirika, kamati na watendaji wake unahitajika kufanikisha malengo ya kibiashara ya ushirika. Viongozi wenye maarifa, maono, wanaofahamu majukumu yao na uwezo wa kusukuma ushirika kwa kuwajibika na uadilifu wa hali ya juu wanahitajika sana.

Tukiwapata watu wa aina hii itakuwa ni moja ya hatua nzuri za kutengeneza msingi imara wa kibaishara kwa vyama vya ushirika nchini.

Kutoingiliwa na siasa. Wengi tunafahamu siasa zinapenya mpaka kwenye vyama vya ushirika lakini ni vema watendaji, wanachama na viongozi wakaepuka kuonyesha maslahi yao ya kisiasa kwenye ushirika.

Ushirika ni biashara hivyo inatakiwa iheshimiwa kama taasisi nyingine na kuachwa kutekeleza maamuzi, utendaji na mipango yake ya maendeleo kwa mujibu wa sheria.

Kutengeneza mtandao mzuri ambao utakuwa unaweka nafasi ya vyama vya ushirika kusadiana ni jambo muhimu kwa mushakabali wa wanachama. Ili kutengeneza uwezo wa kuwafaidisha kibiashara ni vizuri ukawepo mtandao wenye uwezo wa kupatia taarifa za masoko, elimu na mafanikio ili kujifunza.

Kutengeneza wanachama hai wanaotumia huduma na kutambua kwamba ushirika ni mali yao hivyo ni vyema kuwa na ubunifu wa bidhaa na huduma utakaofanya wanachama kukubali na kuendelea kubakia.

Msingi wa ushirika mawazo chanya yenye ubunifu unaoruhusu kujitathimini na kuwekeza kwenye maeneo yenye tija ili kupiga hatua ya kweli ya kibiashara.

Mwandishi ni mtaalamu wa sekta ndogo ya fedha. Kwa maoni anapatikana kwa namba 0657 157 122