Vitambulisho vya wamachinga ni zaidi ya kukusanya Sh20,000

Hakuna mikakati yoyote inayoweza kupangwa bila kuwa na takwimu sahihi na zinazokwenda na wakati.

Ili Serikali iweze kupanga namna bora ya kuwahudumia wananchi wake inahitaji kuwa na takwimu bora zinazoelezea watoto, vijana, wanawake, walemavu, wazee na makundi mengine.

Moja ya changamoto inayokabili nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea ni kutambua idadi halisi ya wananchi wanaojishughulisha na biashara nje ya mfumo rasmi na mchango wao katika kuendeleza nchi zao.

Ripoti ya Umoja wa Wanawake wasio na Ajira Rasmi Duniani (WIEGO) iliyochapishwa mwaka 2012 inataja sekta isiyo rasmi kuundwa na makundi mbalimbali ikiwamo mama/baba lishe, waendesha toroli/guta, vinyozi wa mtaani hawa wapo zaidi Afrika Kusini katika mji wa Durban, na wanaouza biashara mitaani au katika maeneo ya wazi.

Kundi jingine ni mafundi wanaojishughulisha na utengenezaji baiskeli, pikipiki, bajaji na hata magari.

Wapo pia, wanaojishulisha na ukusanyaji na uhifadhi wa chupa za vimiminika zilizotumika na vyuma chakavu.

Ripoti ilibainisha kundi jingine kuwa lile linalojishughulisha na utengenezaji wa samani ikiwamo viti, vitanda, meza, makabati na aina nyingine ya samani pamoja na mafundi wa nguo.

Sekta isiyo rasmi pia inajumuisha utengenezaji wa viatu vya kushona na kupaka rangi.

Pia, usafirishaji wa madini kwa njia ya kienyeji na uchuuzi wa nguo unatajwa kuwa katika kundi la sekta isiyo rasmi.

Wapo madereva wa abiria kwa vyombo vya baiskeli, pikipiki na bajaji.

Kundi jingine ni wale wanaojishughulisha na biashara za vibarua ikiwamo katika migahawa na hoteli.

Walinzi, vibarua wa ujenzi, kilimo na wasaidizi wengine wa ofisi wanatajwa kuwa katika sekta isiyo rasmi na makundi mengine ambayo kwa muktadha huu hayakutajwa.

Orodha hii inaonyesha ni kwa namna gani sekta isiyo rasmi ilivyo sheheni kundi kubwa la watu na kwa vyovyote linahitaji kutambuliwa. Katika makundi tajwa hapo juu ipo idadi kubwa ya watu wanaojishughulisha na shughuli hizo.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); hapa nchini kuna jumla ya pikipiki zilizosajiwa kwa ajili ya biashara milioni 1.2 kwa mwaka 2016.

Kwa tafsiri ya kawaida, vitambulisho vya awali 650,000 ambavyo Rais John Magufuli alivikabidhi kwa wakuu wa mikoa mwaka 2018 visingetosha kwa kundi hili la vijana wanaojishughulisha na biashara ya “bodaboda” pekee.

Utafiti uliofanywa mwaka 2008 kuhusu madhara ya utandawazi katika sekta isiyo rasmi na Umoja wa Mataifa chini ya Tume ya Uchumi Afrika (Uneca) ulionyesha, zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi ya Tanzania imejiajiri kwenye sekta isiyo rasmi.

Hii ni zaidi ya watu milioni tisa kwa kutumia takwimu za idadi ya vijana kuanzia miaka 15–35 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.

Hadi kufikia Januari mwaka huu, jumla ya vitambulisho vilivyotolewa na Rais John Magufuli kwa ‘wamachinga’ ni milioni 1.65.

Kwa takwimu za makadirio ya watu waliopo katika sekta isiyo rasmi, hii bado ni idadi ndogo sana kulinganisha na hali halisi iliyopo mtaani.

Hakuna Taifa lililoendelea au linaloendelea lenye uwezo wa kupuuza kundi linalojipatia kipato cha kuendesha maisha ya kila siku kupitia sekta isiyo rasmi.

Ili kuweza kukidhi mahitaji ya kundi hili ni lazima jitihada mahsusi zifanyike ikiwamo kuwatambua.

Kwa mtazamo wangu, vitambulisho hivi vimetolewa kwa lengo la kuhakikisha Taifa linakuwa na kanzidata ya idadi ya watu wote waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi.

Pili, baada ya kuwatambua ni kuwajengea miundombinu rafiki ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwamo kukopesheka.

Tatu, ni kuwajenga kimtazamo kujua wana wajibu wa kuchangia maendeleo ya Taifa lao.

Kwa mwaka mmoja wenye wiki 52, maana yake kila wiki ‘mmachinga’ anapaswa kuhifadhi kiwango kisichozidi Sh400 ambayo ni sawa na Sh55 kwa siku. Nia safi na dhamira njema inaelekeza kuwezekana kwa hili.

Ni wajibu wetu kushirikiana kwa pamoja na kuhakikisha tunalijenga Taifa lenye heshima na lenye kujitegemea; lengo la muda mrefu likiwa ni kuondoka katika utegemezi wa misaada kutoka nje na kuweza kujitegemea angalau kwa kutoa zile huduma za msingi kwa wananchi.

Mwandishi ni mtakwimu Wizara ya Tamisemi. Anapatikana kwa namba 0685 214 949.