Wazazi tuwape watoto nafasi za kusoma

Wilaya ya Nyang’wale ni miongoni mwa wilaya tano zilizopo mkoani Geita yenye shule 10 za sekondari na wanafunzi 6,756.

Kati ya wanafunzi hao, 3,365 ni wavulana na wasichana ni 3,391.

Shule hizo zilizopo Nyang’wale, nane zina hosteli kwa ajili ya wanafunzi huku mbili zikiwa kwenye mkakati wa ujenzi wa mabweni kwa wanafunzi hasa wa kike ili kuwaondolea kero ya kutembea umbali mrefu na kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuchangia kupata ujauzito.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wanafunzi 160 waliacha shule wilayani humo kwa kupata ujauzito.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia mimba kwa wanafunzi ni kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda na kurudi shule na wengine hutembea umbali mrefu zaidi.

Baadhi hulazimika kutumia usafiri wa baiskeli huku wengine wakitembea kwa miguu.

Umbali mrefu umesababisha wanafunzi wawe wanaomba lifti barabarani huku wanaume wasiowatakia mema kuwarubuni na kuwapa ujauzito unaokatisha ndoto zao.

Serikali kwa kuliona hilo ikaamua kuhamasisha wazazi na wananchi kujenga mabweni ili kunusuru watoto wakike wanaopata mimba na kukatisha ndoto zao.

Mwitikio wa wazazi ukawa mkubwa wakajenga mabweni katika shule nane kati ya 10 zilizopo, lakini jambo la kushangaza mabweni hayo hayana wanafunzi zaidi ya 1,000 na wanafunzi bado wanatembea umbali mrefu.

Wahenga walisema penye miti hapana wajenzi, wakati maeneo mengine nchini wakilia wajengewe mabweni ili kuwasaidia watoto wao kusoma karibu na kuepuka vishawishi, wazazi hawa wa Nyang’hwale licha ya kujenga mabweni hawataki watoto wao wakae shuleni.

Ni kama maajabu ndivyo unavyoweza kusema kwa haraka, wazazi walikubali kushirikiana na Serikali kujenga mabweni ili watoto wa kike wasitembee umbali mrefu na watumie muda mwingi kusoma, lakini wazazi hao hao wamegeuka na hawataki watoto wakae shuleni. Sababu inayoelezwa ndiyo inazidisha maajabu hayo, wanawategemea watoto wawasaidie kazi za nyumbani kila wanapokwenda na kurudi shuleni na umuhimu wa elimu kwao siyo kipaumbele.

Kutokana na wazazi kuzuia watoto wao wasikae bwenini, wazazi wa wilaya na mikoa jirani wamechangamkia fursa na sasa unaweza sema, “kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi.”

Kitendo hiki cha wanafunzi hasa wa kike kutembea umbali mrefu licha ya kuchoka njiani bado wakirudi nyumbani hukutana na kazi za jikoni zikiwasubiri na ni dhahiri muda wao wa kujisomea nyumbani ni mdogo na wengine hushindwa kabisa kusoma.

Mbali na wazazi kukataa watoto wao wasome wakiwa bwenini kwa madai ya kupoteza nguvu kazi, wapo wengine hawapo tayari kuchangia chakula shuleni.

Uamuzi huo licha ya kumuumiza mtoto, mzazi kwake siyo tatizo na anauona ni msimamo wa busara.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyang’hwale yenye bweni, John Mabere anasema wapo wanafunzi wanaotembea zaidi ya kilomita 14 kwenda na kurudi kutokana na wazazi wao kukataa kuchangia chakula watoto wasome.

Gharama za chakula zinazomshinda mzazi kulipa hadi aamue mwanae atembee kilomita zaidi ya 20 kila siku za shule, mahindi debe tatu, mchele kilo 25 na maharage kilo 25 kwa mwaka.

Kwa wazazi wa wilaya hiyo ni wazi kuwa hawashindwi kumudu gharama hizo kwakuwa ni wakulima wazuri wa zao la mpunga,mahindi na maharage hivyo mzazi akiamua anaweza kabisa kumsaidia mwanae asome vizuri kwa manufaa ya baadaye.

Uelewa mdogo wa umuhimu wa elimu kwa wazazi ni moja ya sababu inayowafanya wawazuie watoto wao kusoma bwenini,wazazi wengi huamini mtoto kuwa bwenini ni sawa na kupoteza muda wa kazi.

Wazazi wanaamini mwanafunzi kuwa mtoro shuleni na kwenda kuchunga mifugo au kushiriki shughuli za kilimo ni jambo jema zaidi kuliko kutumia muda huo kujisomea au kuishi bweni ambako kutamsaidia kuepuka vishawishi.

Uongozi wa halmashauri umeliona hilo na tayari mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Mariam Chaurembo amewataka wakuu wa shule kutopokea watoto wanaohamia kutoka wilaya na mikoa jirani hadi pale watakapokaa na wazazi kuona namna ya kuwasaidia watoto wa kike waweze kupata elimu.

Hakuna sababu ya wazazi kujenga mabweni huku wakiwa hawapo tayari watoto wao wakae bwenini.

Wazazi tuamke tumpe nafasi mtoto asome kwa manufaa yake na taifa kwa ujumla.

Rehema Matowo ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Geita, anapatikana kwa namba 0756 - 919 691