Wenye ulemavu ni nguvu kazi iliyosahaulika

Thursday November 1 2018

Mlemavu wa miguu, Seneth Simon (37) ambaye ameacha kuwa ombaomba na kuwa mfanyabiashara baada ya kupata mtaji wa Sh200,000 ni kielelezo kwamba walemavu wakiwezeshwa ni nguzo ya maendeleo ya Taifa na familia zao.

Picha ya Simon ilichapishwa kwenye gazeti hili toleo la jana katika ukurasa wa kwanza, ikimuonyesha akijisukuma kwenye baiskeli yake ya magurudumu manne akipeleka bidhaa anazoziuza sokoni.

Ni picha iliyoleta hisia kwamba watu wenye ulemavu hasa wanaoombaomba mitaani wakiwezeshwa wanaweza kuacha tabia hiyo ya fedheha na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali zitakazochangia pato la Taifa.

Tunafahamu Serikali imekuwa na sera nzuri kuhusu watu wenye ulemavu, hasa ile inayozungumzia umuhimu wa kuanzisha mfuko utakaowawezesha kujijengea uwezo wa kushiriki shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya maendeleo yao.

Hatuna hakika kama sera hii imetekelezwa kwa kiwango gani, lakini muhimu ni kukumbushana kwamba kundi la watu wenye ulemavu ni nguvu kazi iliyosahauliwa na lina umuhimu katika maendeleo ya Taifa.

Mfano, mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu ambao Tanzania imeridhia unazungumzia umuhimu wa kuimarisha na kukuza fursa za kundi hilo kujiajiri, kuanzisha na kuendesha shughuli za ujasiriamali. Kila mmoja anafahamu kuwa wenye ulemavu ni miongoni mwa watu maskini katika jamii na maisha yao yanaambatana na vikwazo mbalimbali ikiwamo baadhi yao kutengwa.

Pia, ushiriki wao katika uzalishaji mali ni mdogo na wakati mwingine mikakati iliyopo ya kuondoa umaskini haijawashirikisha ipasavyo.

Mbali na hivyo, watu wenye ulemavu hawajahamasishwa vya kutosha kuweza kufaidika na mifuko ya kuendeleza makundi maalumu kama yale ya vijana na wanawake. Siku zote imekuwa ikielezwa na kuimbwa kwenye majukwaa ya kisiasa kwamba kuna fedha zinazopelekwa na Serikali kwenye halmashauri kuwakopesha mitaji vikundi vya vijana na wanawake, lakini haijawekwa wazi namna gani wenye ulemavu wananufaika na fedha hizo.

Ni ukweli kwamba watu wenye ulemavu ni nguvu kazi ambayo haijatumika ipasavyo, lakini kama watapewa fursa ya kupata na kutumia rasilimali kuwaletea maendeleo, wanaweza kuongeza ajira kwenye jamii na kuchangia pato la Taifa.

Serikali haina budi kuweka mazingira yatakayowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki, kupata na kutumia vyombo vinavyohusika na uzalishaji mali kwa lengo la kujiletea maendeleo.

Pia, Serikali inatakiwa kuwekwa utaratibu utakaohakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata nyenzo zitakazowawezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya uzalishaji mali. Tunashauri ianzishwe programu ya utambuzi na uendelezaji wa vipaji maalumu vya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

Wadau wa maendeleo kwa upande wao, tunashauri washirikiane na Serikali kuboresha mazingira na mafunzo ya stadi za kazi kwa watu wenye ulemavu.

Pamoja na yote hayo jamii yenyewe inapaswa kuonyesha mwamko kwa kuwapenda na kuwaendeleza kiuchumi watu wenye ulemavu, badala ya kuwageuza kitega uchumi.

Haitakuwa na maana kama Serikali kwa upande wake itatekeleza wajibu wake, lakini jamii ikawa na mtazamo hasi kuhusu kundi la watu wenye ulemavu.

Tunaamini kama jamii itashirikiana vizuri na Serikali, kundi la watu wenye ulemavu linaweza kuishi maisha mazuri na wakawa sehemu ya mchango katika maendeleo ya Taifa.