Yapo mazingira ya ATCL kukua, takwimu zinaonyesha

Mwaka 1943, Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt alisema, “usafiri wa anga si usafiri wa anasa na kifahari” akimaanisha huo ni sawa na usafiri mwingine wowote. Alisema hayo baada ya kuweka historia ya kuwa Rais wa kwanza duniani kusafiri kwa kutumia aina hiyo ya usafiri. Ripoti ya Air Transport Action Group (ATAG) inaonyesha usafiri wa anga umekuwa kichocheo cha kusisimua uchumi, kuongeza uzalishaji wa pato la Taifa (GDP) na fursa za ajira.

Aidha ripoti hiyo inataja kuwapo kwa ongezeko la mtandao wa biashara miongoni mwa mataifa na utalii.

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (Icao) ya 2004 inaonyesha kuwa zaidi ya abiria bilioni mbili duniani walisafiri kwa kutumia usafiri wa anga na asilimia 40 ya bidhaa zilisafirishwa kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa kutumia usafiri huo.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 40 ya watalii walisafiri kwa kutumia usafiri wa anga na kwa mwaka huo na kuzalisha zaidi ya ajira milioni 29 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Pia, sekta hiyo ilisafirisha zaidi ya tani milioni 38 za mizigo. Kiuchumi, usafiri wa anga ulichangia zaidi ya Dola2.96 trilioni za Kimarekani sawa na asilimia nane ya pato la dunia.

Mashirika 900 ya usafiri wa anga yenye ndege zaidi ya 22,000 yanayotumia zaidi ya viwanja 1,670 vya ndege yalifanyiwa utafiti mwaka 2004 na kuonyesha kuwa usafiri huo umechangia kwa kiasi kikubwa ajira na kukuza uchumi wa nchi kupitia kodi na tozo.

Zaidi ya asilimia 75 ya ripoti za kibiashara zilionyesha usafiri wa anga umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa biashara kwa wingi na wakati mmoja kulinganisha na aina nyingine ya usafiri.

Kwa upande wa matumizi ya mafuta ya ndege takwimu za mashirika ya ndege ya Airbus na Boeing zinataja ndege hizo kutumia wastani wa lita tatu kwa kila abiria 100 kwa kilomita. Haya yanatajwa kuwa matumizi bora ya rasilimali na miundombinu kulinganisha na aina nyingine ya usafiri.

Usafiri wa anga hauishii kuwa na faida kiuchumi tu, bali hata kijamii. Mtu yeyote kwa wakati aupendao anaweza kwenda maeneo mbalimbali kwa ajili ya mapumziko na kujiliwaza kwa gharama nafuu.

Kupitia utalii na biashara, hali ya maisha ya watu inaimarika na kupunguza umaskini kutokana na ajira na makusanyo ya kodi na tozo mbalimbali zinazokusanywa kutokana na huduma zinazotolewa.

Kwa upande wa utunzaji wa mazingira, usafiri wa anga unatajwa kupunguza kelele kwa zaidi ya asilimia 75 kulinganisha na aina nyingine ya usafiri. Taasisi zinazohusika na masuala ya usafiri wa anga Ulaya (Nasa) na Marekani (Acre) zinataja kiwango hicho kupungua kwa wastani wa zaidi ya asilimia 50 ifikapo 2020.

Kelele zinatajwa kuwapo wakati wa kuruka na kutua kwa ndege. Usafiri wa anga kwa tafsiri nyepesi umegawanyika katika maeneo makubwa mawili yaani huduma na matengenezo.

Upande wa huduma unajumusiha abiria, mizigo na tiketi. Pia inataja huduma za viwanja na watoa huduma.

Kwa upande wa matengenezo unajumuisha karakana, injini na vifaa vingine. Katika maeneo haya mawili makubwa kote kunazalisha fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Kwa takwimu hizi kuna kila sababu ya kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ili nalo liweze kuingia kwa nguvu kwenye biashara ya usafiri wa anga ambayo ina ushindani mkubwa duniani.

Takwimu zinaonyesha kuanza kuimarika kwa ATCL kutoka kuzalisha hasara miaka kadhaa nyuma hadi kuanza kujiendesha na hatimaye kuzalisha faida. Takwimu za ATCL zinaonyesha mwaka 2016 lilikuwa na deni la Sh14.2 biloni ambalo Serikali imelilipa na kubaki Sh4.3 bilioni hadi mwaka 2017.

Kwa upande wa faida, shirika hilo limeendelea kutengeneza faida kutoka wastani wa Sh700 milioni kwa mwezi 2016 hadi kufikia wastani wa 4.5 bilioni kwa mwezi mwaka 2017.

Moja ya sababu ya kuimarika kwa shirika hilo ni nia na dhamira njema ya Rais John Magufuli juu ya biashara ya usafiri wa anga itakayosaidia kukuza sekta nyingine za uchumi.

Serikali imenunua ndege mpya na kuweka menejimenti mpya kuratibu na kusimamia rasilimali za shirika.

Endapo menejimenti hii itatekeleza majukumu yake kwa ufasaha na umakini, mazingira ya shirika hilo kushamiri zaidi na kulinufaisha Taifa ni makubwa.

Mwandishi ni mtumishi wa Serikali na mtakwimu. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa namba: 0685-214949