Mauaji ya bodaboda tishio Bukoba yadhibitiwe

Tuesday June 12 2018

 

By FREDRICK RUTECHURA

Usafiri wa pikipiki maarufu bodaboda ni usafiri ulioshika kasi hivi karibuni katika matumizi yake. Hata hivyo, kwa muda wote umeendelea kukabiliwa na changamoto lukuki kutokana na namna watekelezaji wake, kwa maana ya madereva na wasimamizi wa sheria wanavyofanya.

Usafiri huu ulianzia nchini Uganda na kuvuka mipaka kuingia Tanzania. Kwa wenzetu Waganda, matumizi ya bodaboda na changamoto zake yamezoweleka na kimsingi ni kwamba, hata yanayousibu huku kwetu kule kwao wameyazowea.

Kwa hapa nchini, kama ilivyo katika nchi nyingine zinazoutumia usafiri huu umeonekana kuwa msaada mkubwa kwa watu wenye kipato cha chini na cha kati kwa kuwarahisishia huduma ya usafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine katika maeneo ya mjini na vijijini.

Bahati mbaya hapa kwetu ni kuwa changamoto za matumizi ya bodaboda zimebaki kuwa mtihani mgumu kuufanya na hivyo unatoa jibu moja tu, kuwa usafiri wa bodaboda ni rahisi kumfikisha mtu kule aendako lakini usalama wake ni kudra za Mungu.

Si hilo tu, lakini kuna changamoto pia za abiria kuwa nao sehemu ya athari zinaoukwaza usafiri huu. Napenda kuwashirikisha wasomaji wa safu hii kuhusiana na tukio la kushangaza lililotokea hivi karibuni huku Bukoba.

Ilikuwa ni usiku wa saa sita kuamkia Jumapili ya Machi 13, 2018, dereva wa bodaboda aliuawa na watu wasiojulikana katika Kata ya Kashai jirani na Shule ya Msingi Kashai.

Dereva huyo kijana huyo ambaye ni mkazi wa Kahororo aliuawa kwa kukatwa na kisu na mtu anayedaiwa kuwa alikuwa amembeba kama mteja wake. Hili ni tukio mojawapo kati ya yale yanayofanywa na wahalifu dhidi ya madereva wa bodaboda.

Katika matukio mengi kama haya yametokea pia sehemu nyingine za mji wa Bukoba ikwemo Kisindi, Rwamishenye, Kashenye na Kasarani. Kwa sasa hofu imetanda kwa waendesha pikipiki hao kutokana na mfululizo wa matukio hayo.

Haya ni matukio yanayojitokeza kuanzia muda wa saa mbili za usiku wakati ambapo giza linakuwa limeingia.

Mpaka sasa hatujajua lengo la mauaji haya kwa kuwa wanaouawa hukutwa katika maeneo husika wakiwa na alama za visu pamoja na pikipiki zao.

Hali hii imejitokeza kwa karibu mwezi mmoja sasa huku ikizua taharuki kwa wakazi wa Kashai, Rwamishenye na Bakoba.

Katika mauaji hayo, imebainika kuwa wauaji hawachukui kitu chochote baada ya kutekeleza mpango huo jambo linalowaanishwa wananchi juu ya kuwapo kwa imani potofu za kishirikina.

Askari wa doria wanahitajika kujipanga kikamilifu ili kuthibiti uhalifu huo. Ni vyema kikosi cha upelelezi kiingie kazini kwa ajili ya kuwabaini wahusika ili kurejesha imani ya wananchi ambao kwa sasa wameanza kuonyesha kukata tamaa.

Pia nawaomba raia wema watoe ushirikiano kusaidia kutoa taarifa za kupatikana kwa wahalifu hao. Kikosi cha intelijensia kwa mfumo wa special task force kinaweza kusaidia kufanya upelelezi wa karibu ili kuutokomeza mtandao huu.

Katika hali kama hii madereva bodaboda nao wachukue tahadhari ya kuheshimu muda wa kazi kwa kutofanya kazi usiku wa manane na kuepuka maeneo hatari kama vichochoroni, mahali ambapo ni rahisi kuvamiwa na kutekwa.

Pia tahadhari ichukuliwe dhidi ya yeyote anayekodisha usafiri wa pikipiki. Hili litakuwa rahisi kama waendesha bodaboda watakuwa pia na vitambulisho maalumu pamoja na sare kama ilivyo kwa madereva na makondakta wa daladala.

Napenda kutoa wito kwa wadau na Serikali kwa ujumla kushirikiana kutatua suala hili. Ndiyo, nafahamu zipo changamoto wanazosababisha madereva bodaboda, lakini nao ni binadamu haki zao zilindwe.