Madaktari wasema asiyevuta sigara ‘Hupokea’ moshi wenye sumu zaidi

Friday January 11 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Wakati takwimu zikionyesha asilimia 16 ya Watanzania wanatumia tumbaku, Shirika la Afya Duniani (Who) limebainisha kuwa waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 54.2.

Who inaeleza kuwa vifo vingi vitokanavyo na matumizi hayo vitatokea miaka ijayo.

Kwa mujibu wa Who, njia sahihi zisipotumika kuzuia matangazo ya tumbaku na kutoa elimu zaidi, hali itakuwa mbaya kwa kuwa ukuaji wa magonjwa yasioambukiza unachangiwa zaidi na tumbaku.

Mratibu Programu ya Usalama Barabarani kutoka Shirika la Afya Duniani, Merry Kessi anasema vifo milioni 7.2 kote duniani kila mwaka husababishwa na matumizi ya tumbaku.

“Kati ya vifo hivyo, wanaoathirika ni wale wanaopokea moshi utokanao na tumbaku ambao ni wanawake na watoto wengi hufariki kwa saratani mbalimbali,” anasema Kessi.

Mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dk Maghuha Stephano anasema kemikali inayotoka kwa mtu anayevuta huwa sumu mbaya zaidi ikipokewa na mtu mwingine.

“Ile kemikali iliyopo kwenye sigara mtu anapokuwa anavuta, ule moshi unaotoka nje ndiyo una sumu nyingi zaidi kuliko ule unaoingia kwa mvutaji,” anasema Dk Maghuha.

Pia, anasema madhara yanayoweza kumpata mtu anayepokea moshi wa sigara kutoka kwa mvutaji, anaweza kupata matatizo ya kawaida kwenye njia za hewa kama kupaliwa na hata magonjwa ya mfumo huo.

“Baada ya muda mrefu ndiyo anaweza kupata madhara kama ya magonjwa ya saratani za mapafu, koo za kichwa na koo, lakini pia zile za ini na aina nyingine ikiwamo saratani ya shingo ya kizazi,” anasema.

Anafafanua zaidi kuwa iwapo saratani ya shingo ya kizazi asilimia 99 hutokana na virusi vya HPV, mwanamke anayevuta sigara au anayepokea moshi wa sigara huwa hatarini zaidi kukumbwa na ugonjwa huo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Ocean Road, Crispin Kahesa anasema kwa kawaida mtu huvuta hewa safi na ikifika ndani huchujwa na taka sumu hutoka, hivyo mvutaji anapouvuta moshi wa tumbaku ule utokao hutoka na sumu nyingi zaidi.

“Tumbaku ndiyo chanzo cha aina zote za saratani, japokuwa kuna zile ambazo athari ni kubwa zaidi kama saratani za mfumo wa hewa ikiwamo mapafu, njia ya chakula, lakini hata ikifika sehemu nyingine inaleta madhara,” anasema.

Dk Kahesa anasema waathirika wakubwa wa matumizi ya tumbaku ni wanawake na watoto kwa kuwa ikiwa baba anatumia tumbaku, atavuta mbele yao na hawawezi kuwa na namna au mamlaka ya kujitetea.

“Ukiwa mwanamume hakuna mtu atakukemea na vivyo hivyo tukija kwenye madhara tunaona wanaopokea moshi wa sigara ndiyo wanaoathirika zaidi na hapo ndipo tunapowaweka watoto na wanawake kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani.” Hata hivyo, Dk Kahesa anasema waathirika wakubwa ni watoto wachanga na wale ambao bado wangali tumboni.

Anasisitiza kuwa tumbaku ni kisababishi cha saratani karibu za aina zote ukiachilia mbali magonjwa ya moyo na kisukari.

Kokulinda Kagaruki kutoka Chama cha kudhibiti matumizi ya tumbaku Tanzania anasema, tumbaku ni kisababishi kinachogusa magonjwa yote yasiyoambukiza.

Anasema lengo la tatu la malengo endelevu, limetambua mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku kama mkakati ambao ukitekelezwa una uwezo wa kupunguza vifo vya magonjwa yasiyoambukiwa kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.

“Tanzania iliridhia mkataba huu mwaka 2007; lakini mpaka leo hatuna sheria madhubuti inayoendana na mkataba na ndani ya Afrika Mashariki, tumebaki peke yetu, namuomba Waziri wa Afya atutie moyo atuambie ni lini tutaipata sheria hii,” anasema Kukulinda.

Wakati tumbaku ikitajwa kuwa kichocheo kikuu cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu anatoa msimamo wa Serikali.

Anasema Tanzania ni mwanachama wa Who na imesaini mkataba na kupunguza matumizi ya tumbaku (Tobacco Control) duniani tangu mwaka 2007.

“Sheria hii imepitwa na wakati, kuna maeneo hayajawa vizuri, katika masuala ya utekelezaji wa sheria kuna maeneo tumefanikiwa hasa katika ya viwanja vya ndege, sasa hivi unakuta kuna onyo usivute sigara na hazivutwi, tumeenda mbali zaidi kama mtu anataka kuvuta watenge vyumba na kwa sasa hayo hayafanyiki.”