UCHAMBUZI: Mashindano ya AFCON ni fursa, tunufaike

Saturday January 19 2019

 

Tanzania imepata bahati ya kuandaa fainali za Fainali za Afrika za Vijana (AFCON) zitakazofanyika Aprili 14 hadi 28 kwenye viwanja viwili; ule wa Taifa na wa Azam maarufu Chamazi Complex.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimthibitishia Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad utayari wa kuwa wenyeji wa mashindano hayo na maandalizi yanaendelea kwa kasi ili kuendana na muda uliopangwa.

Jambo zuri zaidi ni kuwa tayari timu ya wakaguzi kutoka CAF imekuja mara kadhaa na kuridhika na maandalizi, na kilichobaki ni matayarisho madogo madogo kama walivyoelekeza.

Timu zilizofuzu kucheza fainali hizo ni Angola, Cameroon, Guinea, Morocco, Nigeria, Uganda, Senegal na wenyeji Tanzania.

Droo kwa ajili ya mashindano hayo imefanyika ambapo wenyeji Tanzania wamepangwa na Nigeria, Angola na Uganda katika Kundi A.

Katika droo iliyofanyika Mlimani City mjini Dar es Salaam ,kundi B linazikutanisha timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Wakati w enyeji Tanzania tukiwakilishwa na timu ya vijana ya Serengeti Boys, itafungua dimba na bingwa mara mbili wa michuano hiyo Nigeria, Aprili 14, 2019 kabla ya kukutana na Angola Aprili 17 na kukamilisha mechi za kundi lake kwa kuonyeshana umwamba na Uganda Aprili 20.

Ukitizama kwa umakini Serengeti Boys imepangwa kundi gumu, hivyo inahitaji shangwe, kuungwa mkono na Watanzania wote kila mmoja kwa namna anavyoweza ili kuhakikisha inaingia fainali na kujihakikishia safari ya kucheza fainali za kombe la dunia nchini Peru kati ya Oktoba 5 na 27 mwaka huu.

Mbali yn kuiunga mkono timu hiyo, lakini Watanzania hususani vijana wana kila sababu ya kuona fursa katika michuano hii, kwa sababu itafungua mianya ya kuingiza mapato ikiwamo biashara na kutengeneza marafiki wapya kutoka katika nchi zinazoshiriki michuano hiyo na zitakazokuja kwa lengo la kuwekeza.

Kinachofurahisha ni kuwa kwa kipindi cha mwezi mzima ambao utakuwa kunafanyika mashindano hayo ofisi nzima ya CAF itahamia hapa nchini.

Hii ni bahati na fursa kubwa kwa vijana wa Kitanzania kufanya biashara na kupata ajira za muda.

Kuna baadhi ya hoteli ambazo viongozi hao watazibadili na kuwa ofisi tayari zimeanza kutoa ajira za muda kwa watakaozibadili mwonekano na kuziweka kiofisi.

Mbali ya fursa hiyo ipo pia fursa ya utalii wa nchi yetu, badala ya kuhangaika kwenda mbali kutangaza, sasa wageni kutoka nchi mbalimbali za ndani na nje ya Afrika watakuwa hapa nchini.

Vijana wachonga vinyago, wachoraji, wanamuziki, wabunifu wa mavazi na wenye vipaji mbalimbali kupitia michuano hii mtapata nafasi ya kujitangaza na kuanzisha uhusiano mpya.

Hivyo unapokwenda kiwanjani kuangalia mechi, unapohudhuria mikutano ya wazi inayohusisha michuano hiyo, matangazo hakikisha una kipeperushi cha bidhaa au huduma unayotoa kwa sababu ni rahisi kukutana na wageni ikiwamo wafanyabiashara, watangazaji, waandishi wa habari watakuwa wanazunguka maeneo hayo.

Kwa kifupi wakati huo utakuwa ni wakati wa fursa ya kupata fedha, kujifunza na kupanua wigo wa unachokifanya, mji utakuwa umefunguka.

Jambo la maana tunalopaswa kufanya kama vijana kuiunga mkono timu, kujitangaza, kufanya biashara kwa nidhamu ya hali ya juu.

Inawezekana kusiwe na faida kubwa kwa mashindano haya ya vijana kwa nchi na mtu mmoja mmoja, lakini kitakachofanyika sasa ndiyo kitafungua wigo kwa mashindano makubwa.

Hivyo tuwekeze sasa kwa ajili ya baadaye, tutumie fursa hii kuonyesha upendo wa Watanzania badala ya kufanya vurugu, kama unauza bidhaa au kutoa huduma hakikisha ina ubora wa hali ya juu, usilipue kwa sababu una uhakika wa wateja.

Vijana mnaouza chakula hakikisheni mnauza kilicho bora hususani kwenye maeneo watakapokuwa wanazunguka wageni, badala ya kuona wingi wao ni nafasi ya kuwauzia ndaza. Kufanya hivi ni kujiharibia kwa sababu CAF hawatatoa nafasi kwa nchi kuandaa mashindano makubwa.

Popote ulipo kumbuka Tanzania waandaaji wa AFCON 2019 umiza kichwa, fikiria utanufaika vipi na mashindano hayo na utasaidiaje taifa kuyaandaa mashindano makubwa zaidi ya hayo.

Kalunde Jamal ni mwandishi wa Mwananchi, anapatikana kwa simu namba; 0713856970