Hili la UTI liziamshe mamlaka nchini

Saturday March 16 2019

By Mhariri

Matumizi holela ya dawa ni tatizo ambalo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara na wataalamu wa afya wakibainisha madhara ya tatizo hilo ikiwamo wa usugu kwa magonjwa.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amewahi kulizungumzia suala hilo akionya matumizi holela ya dawa za kutuliza maumivu yanavyoweza kumsababishia mtu maradhi ikiwamo ya figo.

Wakati tukiamini kauli ya waziri ina maana kubwa ya kutukumbusha Watanzania ili tuepukane na matumizi holela ya dawa, tumeshtushwa na taarifa kuhusu vipimo vinavyofanyika kwa kulipua kwa ugonjwa wa UTI.

Taarifa hizo ambazo zilichapishwa na gazeti hili jana, zilieleza kuwa baadhi ya zahanati na hata hospitali huwapa wagonjwa majibu yasiyo sahihi ya vipimo vya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo wagonjwa wengi wanaodhaniwa kuwa na UTI, baada ya kupimwa hupewa majibu baada ya saa moja au mbili wakati kiutaratibu wa vipimo majibu ili yawe ya uhakika yanatakiwa yapatikane ndani ya saa 48 hadi 72.

Jambo hili linashangaza na kuogopesha kwani kwa maana nyingine inadhihirisha kwamba, bado lipo tatizo katika sekta ya afya kuhusu suala la vipimo wanavyopatiwa wananchi katika hospitali.

Kwa hiyo yale matatizo ambayo naibu waziri aliyataja kuhusiana na suala la dawa kutumiwa bila kuzingatia taratibu, hayapishani na hili kwani yote yanamwangukia mwananchi yuleyule japokuwa kwa njia tofauti.

Kinachosikitisha zaidi ni kuwa Watanzania wanakwenda hospitali kwa wataalamu, lakini wataalamu haohao wanawapa majibu yasiyo ya uhakika, hivyo kuwarudisha kulekule kwenye matumizi holela ya dawa.

Kwa mujibu wa mganga mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi, vipimo vya UTI vinaanza kwa kupima mkojo na baada ya hapo ndipo mtalaamu hujiridhisha kama ni ugonjwa huo na katika hatua hiyo ni lazima bakteria waoteshwe kitaalamu, hatua ambayo inaitwa culturing bakteria.

Baada ya hapo majibu sahihi yatapatikana ambayo pia yatatoa mwelekeo wa dawa gani mgonjwa atumie, vinginevyo anaweza kupewa dawa isiyo sahihi na hivyo kutengeneza usugu na kumfanya asipone. Hatua yote hiyo ya vipimo inachukua si chini ya saa 48 hadi 72.

Hatutaki kuamini kwamba wataalamu wetu wa afya wanaowahisha vipimo vya UTI hawajui taratibu, badala yake tunadhani wanafanya wanachofanya kutokana na tamaa ya kufanya biashara ya dawa ili wapate pesa.

Dhamira ya kuuza dawa inawafanya wakiuke maadili yao ya kitabibu ambayo wametumia miaka kuyahifadhi akilini mwao, jambo ambalo si zuri na linapaswa kupigwa vita na kila mtu.

Hata hivyo, haitoshi kwa Watanzania kulipigia kelele jambo hili badala yake tunapenda kuona viongozi wa hospitali na vituo vyote vya afya wanahakikisha utaratibu unafuatwa ili kulinda afya za watu.

Pamoja na hilo, pia ili mafanikio yapatikane ni vyema mamlaka zinazohusika na usimamizi sekta ya afya ziamke na kusimama imara kuhakikisha utaratibu wa vipimo vya UTI na magonjwa mengine unafuatwa na kuzingatiwa na kila mtaalamu.

Tunayasema haya tukiamini kwamba, iwapo hao wanaofanya ‘mchezo’ huu unaohusiana na maisha ya watu wanadiriki kufanya hivi kwa vipimo vya UTI kinyume na utaratibu, hivi inakuwaje katika magonjwa mengine? Hapo ndipo tunapouona umuhimu wa mamlaka husika kufanya kazi yake na ikiwezekana tuone hatua za kinidhamu na kisheria zinachukuliwa dhidi ya wahusika kwa sababu wanacheza na maisha ya watu.