UCHAMBUZI: Ni muda mwafaka kutumia Kiswahili kufundishia

Tuesday October 1 2019

 

By Emmanuel Mtengwa

Mijadala inaendelea kila kona, tafiti zinazidi kufanyika na mapendekezo yanatolewa, lakini bado ni kitendawili.

Ni kuhusu matumizi ya lugha ya kufundishia nchini. Mijadala imekuwa na mvutano baina ya wadau wa elimu huku wengine wakiona mfumo unaotumika sasa wa elimu umekuwa kikwazo wakishawishi kuwa Kiswahili ndio mwarobaini wa elimu yetu.

Mtazamo wao ni kwamba unapomwelekeza mtoto kitu kwa lugha anayoielewa, inakuwa rahisi kupata maudhui yanayolengwa. Naamini hakuna anayepingana na nadharia hii.

Nikiwa mdau wa Kiswahili ninaungana na wale wanaoamini kuwa kutumia Kiswahili kufundishia kutoka elimu ya awali hadi elimu ya juu, kunaweza kuleta manufaa kwa wahitimu, kwa kuwa ukimfundisha mwanafunzi kwa lugha anayoielewa kunampa fursa ya kuoainisha nadharia na maisha ya kawaida.

Hakuna atakayepingana nami kuwa Kiingereza kwa Tanzania ni kikwazo katika kumuunganisha mwalimu na mwanafunzi, lakini pia kati ya mzazi na mtoto.

Wazazi wengi wanazungumza Kiswahili wakiwa na watoto nyumbani lakini elimu shuleni inatolewa kwa Kiingereza. Hiki ni kikwazo hasa kwa mzazi kumsaidia mtoto kuoanisha yale aliyofundishwa shuleni na mazingira yanayomzunguka.

Advertisement

Kuna baadhi ya tafiti zinazobainisha kuwa tatizo la Kiingereza nchini si kwa wanafunzi pekee, hata baadhi ya walimu wanapata shida kuelekeza kwa kutumia Kiingereza.

Wakati mwingine walimu hulazimika kufundisha somo la Kiingereza kwa Kiswahili ili kumpa mwanafunzi nafasi ya kuelewa bila kujali kuwa anamuandaa mwanafunzi ambaye atajibu mtihani utakaotungwa kwa Kiingereza.

Ninachozungumzia ni maudhui yanayotakiwa kwa mwanafunzi, haimaanishi kuwa Kiingereza ndio elimu bora. Ifahamike kuwa Kiingereza ni lugha tu, si elimu.

Mfumo ulivyo sasa, mtoto anaanza shule ya awali hadi darasa la saba akifundishwa kwa Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza. Akianza sekondari anabadilisha anafundishwa kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili.

Naiona hali hii ikiendelea kuleta mkanganyiko hasa ukizingatia mwanafunzi anakutana na masomo mengi sekondari na matokeo yake inamlazimu mwanafunzi kukariri badala ya kuelewa.

Ninatamani kuona Kiswahili kinatumika kama lugha ya kufundishia kutoka elimu ya awali hadi elimu ya juu kama wadau wengine wanavyopendekeza, nikiamini kuwa lugha inayotumika sasa inawapa shida wanafunzi wengi kupokea maudhui wanayolishwa shuleni.

Nionavyo mimi, ili kupata matokeo chanya yenye ufanisi kwa vijana ni lazima wadau wa elimu na Serikali kuamua kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.

Unapotumia lugha ambayo ni changamoto kwa mpokeaji, mpokeaji atakosa maarifa, stadi na ujuzi unaostahili kutokana na kikwazo cha mawasiliano yasiyo fanisi baina ya mpokeaji na muwasilishaji.

Kiswahili kinafahamika vizuri kwa wanafunzi na walimu walio wengi kwa kuzungumza na kuandika na pia ndiyo lugha inayotumika kwa mawasiliano kati ya wanafunzi wenyewe na wazazi nyumbani. Ndio maana nawiwa kuhoji kwa nini kunakuwa na kigugumizi cha kuruhusu lugha moja kutumika katika elimu kutoka elimu awali hadi elimu ya juu?

Kuendelea kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, ni kuwafanya wanafunzi kuwa na ugumu wa kuelewa kutokana na ujuzi mdogo wa lugha inayotumiwa kufundishia.

Katika kongamano la elimu lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi hivi karibuni, baadhi ya wadau walipaza sauti zao wakiona lugha ya kufundishia imekuwa kikwazo katika maendeleo ya elimu.

Hawakusita kupendekeza kuwa na mfumo unaoruhusu lugha moja kufundishia badala ya matumizi ya lugha mbili kama ilivyo sasa.

Pamoja na wadau wengine wanaosisitiza matumizi ya Kiswahili, Rais wa Tanzania, John Magufuli naye hayuko nyuma, amekuwa akihamasisha na kusisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali.

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) katika mkutano wao wa 39 uliofanyika Agosti jijini Dar es Salaam, walipitisha Kiswahili kuwa lugha ya nne itakayotumika katika nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Hizi ni jitihada zinazoashiria kuwa Kiswahili kina nafasi kubwa katika ulimwengu wa sasa.

Emmanuel Mtengwa ni mdau wa Kiswahili : 0753590823