Fao, Koica kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar waboresha sekta ya ufugaji viumbe bahari

Wednesday January 22 2020

 

Ufugaji wa viumbe bahari Zanzibar umepiga hatua kubwa kufuatia mafanikio ya kuanzishwa kwa kituo cha kisasa cha uzalishaji wa vifaranga wa viumbe bahari kilichofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (koica) kupitia ushauri wa kitaalam wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (Fao).

Kituo hiki cha urafiki baina ya Korea na Zanzibar hivi karibuni kilikabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kukidhi uhitaji unaoongezeka wa uzalishaji wa vifaranga vya viumbe bahari ndani na nje ya kisiwani humo.

Mradi huu wa maendeleo ya sekta ya ufugaji viumbe bahari Zanzibar ulijumuisha ujengwaji wa uwezo katika sekta hii ya ufugaji wa viumbe bahari, ujenzi na uendeshaji wa kituo cha uzalishaji vifaranga vya samaki, uunganishaji wa wakulima kwenye mashamba ya mfano, mnyororo wa thamani wa mazao ya viumbe bahari, na ubia wa pamoja kati ya sekta binafsi na ile ya umma.

a.  Kituo cha uzalishaji vifaranga vya viumbe bahari chajengwa, chaanza kufanya kazi

Ujenzi wa kituo cha kisasa cha uzalishaji wa aina mbali mbali za vifaranga wa viumbe bahari umekamilika na tayari kimeshaanza kufanya kazi. Mwanzo kilijikita katika uzalishaji wa aina tatu za viumbe bahari yaani jongoo bahari, samaki aina ya mwatiko na kaa koko.

Lakini hivi karibuni, aina nyingine mpya ya viumbe bahari imeongezwa yaani samaki aina ya perege ambapo uzalishaji wake utaanza rasmi mwaka 2020 baada ya majaribio ya kwanza kuonesha matokeo mazuri.

Advertisement

Jongoo Bahari

Jumla ya mizunguko kumi na mbili ya uzalishaji wa jongoo bahari ilifanyika. Ilizalisha jumla ya vifaranga elfu thelathini na sita na mia tatu ambavyo vilisambazwa kwa wakulima waliopo Pemba na Unguja.

Mwatiko  

Pamoja na kwamba kituo hakina samaki wazazi wa kuzalisha mayai ya mwatiko, mradi ulikamata vifaranga vikubwa themanini na moja (81) ambavyo vinalelewa katika mabwawa ya kituo hiki ili kuja kutumika kwa ajili ya uzalishaji wa mayai kama samaki wazazi kuanzia mwaka 2020.

Kwa ajili ya kuziba pengo la mahitaji ya vifaranga kwenye soko, Mradi uliagiza vimelea laki mbili (200,000) vya mwatiko ili kuchochea uzalishaji wa kibiashara wa viumbe bahari Zanzibar. Hivi vilitumika kuzalisha vifaranga elfu ishirini (20,000) ambavyo vilisambazwa kwenye mashamba ya mafunzo na wafugaji binafsi huko Pemba na Unguja. 

Kaa Koko

Majaribio kadhaa ya kutagisha na uzalishaji wa vimelea na vifaranga vya kaa koko yamefanyika kati ya Desemba 2017 na Septemba 2019.

Jumla ya vimelea milioni kumi na moja, laki tano, sabini na tano elfu (11,575,000) vilizalishwa katika majaribio haya na kufanikiwa kufikia hatua ya tano (5) katika uzalishaji.

Uzalishaji wa chakula hai cha viumbe bahari

Kituo kinaendesha uzalishaji wa chakula hai kwa ajili ya viumbe bahari ambapo aina kuu saba za za majani maalum yanazalishwa, miongoni mwa vingine.

Kina uwezo wa kuzalisha (bila kujumuisha matangi ya nje) lita elfu nane na mia mbili (8,200) ambayo ni sawa na uzalishaji wa zaidi ya lita elfu moja mia nane (1,800). Uwezo huu wa uzalishaji unaweza kuongezeka.

  1. Uwezo wa wakulima, maofisa wa serikali, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wa kituo umeendelezwa na kuimarishwa

Mradi umeendeleza na kuimarisha uwezo wa wakulima, maofisa wa Serikali, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyakazi wa kituo juu ya hatua sahihi za ufugaji wa viumbe bahari katika muktadha wa kibiashara, na juu ya uendeshaji wa mashamba darasa yaliyopo Pemba na Unguja kote.

Wafanyakazi wa kituo

Mradi umejenga uwezo wa wataalam kumi na mbili (12) wa kituo ambao wanajumuisha wengine kutoka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi (Zanzibar) kuhusu uzalishaji wa aina mbalimbali ya viumbe bahari pamoja na vyakula vyao kama vile kaa koko, jongoo bahari, perege na kadhalika.

Hii ni hatua endelevu inayofanikishwa kupitia mafunzo yanayofanywa na wataalam wazawa na wale wa kimataifa. Mradi pia ulifanikisha ushiriki wa wataalam wa kituo katika mafunzo ambayo yalifanyika ndani na nje ya nchi.

Wakulima na maafisa wa serikali

Zaidi ya wakulima mia tatu (300), wavuvi na maafisa wa Serikali kutoka Pemba na Unguja walipata mafunzo juu ya ufugaji wa kibiashara wa viumbe bahari pamoja na masuala mbalimbali muhimu kuhusu shughuli hiyo. Mafunzo haya yalijumuisha mafunzo ya vitendo kwenye mashamba darasa na pia kuwatambulisha kwenye mambo mengine mapya kama vile uchanganyaji wa ufugaji wa viumbe bahari kama vile kaa koko na kilimo cha mwani.

Wanafunzi na wafanyakazi wa vyuo vikuu

Mradi umejenga mahusiano ya karibu na vyuo vikuu ikijumuisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Taasisi ya Sayansi ya viumbe bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Zanzibar na Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo umetoa fursa za kujifunza na kufanya tafiti mbali mbali kwa wanafunzi na wafanyakazi wao.

Kufikia Desemba 2019, zaidi ya wanafunzi arobaini (40) ikijumuisha wale waliokuwa wakifanya masomo kwa ngazi ya shahada ya uzamivu, umahiri na zile za kwanza walifanya tafiti zao katika kituo hiki.

  1. Mashamba ya ufugaji samaki kibiashara yaanzishwa, yaanza uzalishaji

Ili kuhakikisha uendelevu wa mashamba ya kibiashara ya ufugaji wa viumbe bahari kote Unguja na Pemba, mradi ulisaidia uendelezwaji na uboreshwaji wa mashamba ya mifano saba (7) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi (Zanzibar).

 

Ili kuhakikisha mafanikio ya mradi yanakuwa endelevu, Fao, Koica na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wengine waliandaa mkakati maalum wa mwisho wa ufadhili wa mradi.

Utafiti ulifanyika ili kuweza kuivutia sekta binafsi katika uwekezaji wa kituo hiki kupitia Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi. Kampuni kadhaa za binafsi kutoka Tanzania Bara, Kenya na Msumbiji zimeonesha nia ya kushiriki katika shughuli za mradi huku nyingine zikiwa tayari zimewasilisha rasmi mahitaji yao kwa ajili ya kupata vifaranga.

Ushuhuda wa wanufaika

Ufugaji jongoo bahari wakuza vipato vya wavuvi, wakulima wa mwani huko Pemba

Wavuvi na wakulima wa mwani katika kijiji cha Kukuu Wilaya ya Mkoani, Pemba Kaskazini Zanzibar wamejawa na furaha kufuatia mafanikio ya mradi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ushauri wa kitaalam wa Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao) ambao umewaongezea shughuli nyingine ya kuzalisha kipato.

Ukiwa unafadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (Koica), mradi huu wa Maendeleo ya Sekta ya Ufugaji Viumbe Bahari Zanzibar, umewawezesha wavuvi na wakulima hawa kufuga aina mbalimbali ya viumbe bahari ikijumuisha jongoo bahari, mwatiko na kaa koko kama sehemu ya juhudi za kuboresha vipato vyao, uhakika wa chakula na lishe.

“Tulikuwa tunategemea shughuli mbili tu – uvuvi na kilimo cha mwani,” anasema Salum Mohamed Juma mmoja wa wanakijiji wa Kukuu ambaye pia ni mwenyekiti wa kikundi cha wafugaji wa jongoo bahari kinachojumuisha matawi mawili yaani wavuvi na wakulima wa mwani.

Kwa mujibu wake, uvuvi ulikuwa hautabiriki kutokana na kupungua kwa idadi ya samaki baharini jinsi muda unavyokwenda. “Mradi huu umekuja katika wakati muafaka. Kwa sasa tumeanza kuchanganya uvuvi na kilimo cha mwani pamoja na ufugaji wa majongoo bahari kwa pamoja,” anafafanua.

 “Tuna furaha kwani hatutegemei tena uvuvi na kilimo cha mwani pekee. Tunatumaini kuona kijiji chetu kikistawi katika muda mfupi ujao na mpaka sasa majongoo bahari tunayofuga yanaendelea vyema,” Juma anahitimisha.

Kwa upande wake, Tabia Mohamed Omar mwanakijiji mwingine anasema kuwa mafunzo waliyopata kuboresha kilimo cha mwani na namna ya kuchanganya na ufugaji wa majongoo bahari ni mchango mkubwa wa kuboresha maisha yao.

“Hii ni habari njema kwetu sisi wanawake. Mwani ndio shughuli yetu kuu ya kiuchumi. Tunalisha familia zetu, tunalipa ada za shule na gharama za huduma za afya kupitia kilimo cha mwani,” anasema. Ali Rashid Hamad ni Afisa Mipango na Utawala wa Kitengo cha Maendeleo ya Uvuvi katika Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa Ofisi ya Pemba. Ni mmoja wa wataalam ambao wanafanya kazi na Fao katika kutoa mafunzo na kushirikiana na wakulima katika kuanzisha na kuendesha mashamba darasa.

 “Kama sehemu ya mradi, tulianza na kutoa mafunzo kwa wakulima na kufuatiwa na uanzishwaji wa mashamba darasa kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima wengine, na kwa hapa Pemba kijiji cha Kukuu kilipata bahati ya kuwa sehemu ya mradi huu. Kwa kuanzia, waliingia katika ufugaji wa jongoo bahari. Eneo hili lina mazingira yote muhimu kwa ajili ya ufugaji wa jongoo bahari,” anasema.

Hamad anahitimisha kwa kuwataka wadau wote ikiwemo sekta binafsi kuja na kuwekeza huko kwao ili kukuza uzalishaji wa jongoo bahari kwa kuwapa wakulima vitendea kazi vya muhimu kwa ajili ya uzalisaji mkubwa ili kuweza kufikia kiwango kikubwa kinachohitajika katika soko.

Ujengaji uwezo wa wataalam wa ndani

Yusuph Salum Yusuph ni mwanafunzi anayemalizia masomo yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Taasisi ya Sayansi za Baharini Zanzibar ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Masomo yake yamejikita katika suala zima la uzalishaji wa jongoo bahari pamoja na namna ya kuwakuza kufikia ukubwa ambao wanaweza kugawiwa kwa wanavijiji kwa ajili ya ufugaji.

Yusuph anasema alianza masomo yake mwanzoni mwa mwaka 2016 wakati huo Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Ufugaji Viumbe Bahari Zanzibar haujaanza. “Mwishoni mwa mwaka 2016 ndipo ujenzi ulipoanza na wakati ukiendelea tulianza kufanya kazi pamoja na Fao katika kiatamizi kidogo ambacho kilikuwa kinapatikana ndani ya kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar pale Beit el Ras, Zanzibar,” anabainisha.

Kwa sasa Yusuph yupo katika hatua za mwisho za kumaliza masomo yake ambapo anajiandaa kuwasilisha ripoti ya utafiti wake kuhusu majongoo bahari.

“Kusema ukweli ujenzi wa kiatamizi hiki kupitia huu mradi kwa hapa Zanzibar umenisaidia kwa kiasi kikubwa kwa kuniwezesha kukamilisha masomo yangu,” anakumbuka.

Maoni yake kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa uwekezaji huu mkubwa kupitia mradi huu unakuwa endelevu ili kuhakikisha wakulima na wafugaji wanendelea kufaidika. Kwa upande wa wale waliopata bahati ya kupata mafunzo kupitia mradi huu hususan wale walioajiriwa kuendesha kituo hiki, Yusuph anawashauri watumie elimu na maarifa yao ili kuweza kuisadia serikali katika kuendeleza huu mradi ili matunda yake yaonekane.

“Isiwe mradi ukiisha basi kila kitu kinakufa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kwa sababu tukiweza kuendeleza kile ambacho kimeanzishwa, huu mradi utatatua matatizo mbalimbali yanayohusu upungufu wa rasilimali za baharini,” alishauri.

Kwa upande wake Omar Haji Omar anayesomea shahada ya umahiri katika Chuo Kikuu cha Bremen, nchini Ujerumani kwenye masomo ya Shahada ya Kimataifa ya umahiri katika Sayansi ya Ekolojia ya maeneo ya ufugaji viumbe bahari yaliyopo katika Tropiki anasema mradi wa kituo hiki umekuwa msaada mkubwa sana kwake.

“Kituo hiki cha uzalishaji wa vifaranga wa viumbe bahari kinanisaidia sana katika masomo yangu. Hivi sasa nafanya utafiti wangu kuhusiana na majani bahari ambayo pia ni chakula cha viumbe bahari mbalimbali ambapo nitakusanya taarifa kwa ajili ya kuandika andiko la kuhitimu masomo yangu juu ya hili,” anasema. 

Omar alisoma shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisomea fani ya BSc. in Aquatic Environmental Sciences and Conservation na kuhitimu mwaka 2014.

Anasema amefaidika sana na kituo hiki kwani miundombinu yake ipo vizuri kwa ajili ya kuendesha utafiti wake.  “Kama kituo hiki kisingekuwepo ningefanya utafiti wangu sehemu nyingine lakini gharama zake zingekuwa kubwa. Pia hakuna eneo lingine kwa sasa kwa hapa Zanzibar lenye miundombinu ya kisasa kama hili,” anasema.

Naye Said Juma Shaaban ni mmoja wa wataalam wanaofanya kazi katika kituo hiki. Yeye ni mtaalam wa uzalishaji wa vifaranga vya samaki, jongoo bahari na kaa koko. Amekuwa akifanya kazi hapa tangu Juni mwaka 2017. Kabla ya hapa alikuwa akifanya kazi katika kiatamizi cha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

“Kupitia kituo hiki nimejifunza mengi ambayo sikuyajua kabla kama uzalishaji wa vifaranga samaki, uzalishaji wa jongoo bahari na uzalishaji wa kaa koko. Nimepata mafunzo ya ufugaji na ujengaji wa mashamba ya ukuzaji wa jongoo bahari na utengenezaji wa nyumba za kukuzia kaa koko,” anasema.

Said anasema pia kuwa alipata fursa ya kupata mafunzo ya uzalishaji wa samaki nje ya nchi yaliyofanyika nchini Ufilipino mwaka 2019. Said anasema kuwa ndoto yake ni kujiendeleza zaidi kielimu katika fani hii ili aje kuwa mtaalamu aliyebobea na mzalishaji bingwa wa kimataifa wa vifaranga vya vuimbe bahari.

Mradi huu umetuhakikishia upatikanaji wa vifaranga vya jongoo bahari

“Tumeanza ufugaji samaki tangu mwaka 1998. Lakini miaka hii yote tulikuwa tunafuga kienyeji tu,” anasema Inspekta Badru Ali Makungu Kaimu Kamanda wa Idara ya Magereza Bumbwini, Kaskazini Unguja.

Kwa mujibu wa Kamanda Badru, walikuwa hawana vyanzo vya uhakika vya kupata vifaranga vya samaki na pia hata mabwawa waliyokuwa wanayatumia yalikuwa ya kawaida tu. 

“Mradi huu umetusaidia kuboresha ufugaji wetu. Sasa tunafuga kisasa. Tuna uhakika wa vifaranga na pia tumeboresha mabwawa yetu. Tulikuwa na changamoto sana ya kupata vifaranga. Mradi huu umekuwa mkombozi mkubwa. Mafunzo tuliyopata yametupa maarifa makubwa sio kwetu tu bali hata kwa wafugaji na wavuvi wa vijiji vya jirani,” anasema.

Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Ufugaji Viumbe Bahari Zanzibar umewapatia vifaranga vya samaki 4,500 ambapo wameviweka katika mabwawa mawili makubwa.

Akielezea kuhusu hali ya masoko, alisema kuwa wao kama Idara ya Magereza hawana tatizo la soko kwani samaki wote wanaowazalisha hutumika kulisha wafungwa na serikali kulipa. Maelezo haya pia yanaendana na yale ya Mohammed Khamis Ali kutoka Kisiwa cha Uzi, Kusini Mashariki mwa Unguja. Yeye mbali tu ya kuwa mmoja wa wafugaji wa majongoo bahari, pia ni afisa wa kitengo cha mazao ya baharini kwa Wilaya ya Kati, Zanzibar.

“Zamani tulikuwa tunayaokota tu majongoo bahari huko baharini. Uvunaji haukuwa endelevu na ikafika kipindi yakapungua na sehemu nyingine yalitoweka kabisa. Bei zake zikapanda kutokana na kuadimika,” anasema.

Kwa Bi. Mtumwa Hamis Haji wa kikundi cha Rabi Tuokoe cha kijiji cha Mafufuni mradi huu umeleta fursa ya kuongeza uzalishaji ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko hususan kwa samaki aina ya mwatiko ambao wanaonekana wa masoko zuri. “Tulianza kufuga kidogo na tukagundua kuwa bwawa lilikuwa dogo. Tukaamua kuuza samaki wote na kisha kulipanua. Tayari tumepata vifaranga. Mwatiko wana soko kubwa. Na hata sisi wenyewe tunakula. Watamu mno. Sokoni wanauzika vyema,” anasema.

Kwa upande wake Mahadhi Jumbe Haji wa Kikundi cha Mungu Tupe Baraka cha Kijiji cha Mafufuni, Bumbwini anasema walianza ufugaji wa samaki aina ya mwatiko mwaka 2018. “Baada ya mafunzo tuliingiwa na hamu. Tukaanza wenyewe,” anasema. Mradi huu umewapa vifaranga vya samaki 500. Wachache walikufa na wakawaongeza wengine kutoka baharini.

“Tunataka kuifanya hii kazi iwe endelevu. Tumejifunza ufugaji wa kisasa. Tunajua sasa wakifikia muda gani wanakuwa tayari kuliwa. Mwatiko wanakua kwa haraka sana,” anasema.