Serengeti Boys yapata mualiko Uturuki

Wednesday December 19 2018

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ wamepata mualiko mwingine wa kushiriki katika mashindano maalumu ya maandalizi ya Afcon U17 yatakayofanyika nchini Uturuki kuanzia Februari 22, hadi Machi 2, 2019.
Serengeti Boys imepata mwaliko huo ikiwa ni siku chache baada ya kutwaa ubingwa wa kombe la COSAFA kwa kuifunga Angola kwa mikwaju 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1 nchini Botswana.
Wakiwa wamerejea nchini na furaha baada ya kupata ushindi huo, Serengeti imepata mualiko mwingine wa kushiriki katika mashindano maalumu ya maandalizi ya Afcon U17 yatakayofanyika nchini Uturuki mwezi Februari 2019.
Mashindano hayo yameandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).
Mashindano hayo yataanza Februari 22, 2019 mpaka Machi 2, na kushirikisha jumla ya timu 12 kutoka Afrika na Ulaya.
Mashindano hayo yatakuwa ni sehemu ya maandalizi ya Serengeti Boys katika kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika U-17 yatakayofanyika Aprili mwakani jijini Dar es Salaam.