Alphonsina Kaduma Kutoka ufundi makenika hadi uuguzi

“Daktari hutibu, lakini muuguzi hutunza mgonjwa. Kazi ya kutunza mgonjwa inahitaji ukarimu, upole, upendo na uwezo mkubwa wa kumtia moyo hata yule aliyekata tamaa kwamba kifo kimeribia, lazima ajione anayo nafasi ya kupona.”

Hivi ndivyo muuguzi na mkunga wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi (Tanna) mkoani humo, Alphonsina Kaduma alivyoanza kuelezea kazi yake.

Kwa zaidi ya miaka 30 sasa, mwanamke huyo amekuwa akiwahudumia wagonjwa mbalimbali kupitia kazi yake ya uuguzi.

Wakati leo dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Kaduma anajivunia maadhimisho hayo kwa kudumu kwenye taaluma inayohusisha uokozi wa maisha ya watu hasa, kitengo cha mama na mtoto alichofanya kazi kwa zaidi ya miaka saba.

“Nafurahia kazi yangu na huwa nafurahi zaidi pale mgonjwa anapopata nafuu au kupona kabisa na kisha kuruhusiwa kutoka hospitali. Kazi yangu ni kuhakikisha anakuwa salama.”

Awali, Kaduma hakupenda kuwa muuguzi, hivyo aliamua kusomea ufundi makenika.

Alifanya kazi hiyo kwa miaka minne wilayani Ludewa Mkoa wa Iringa, lakini moyo wake haukuwa na furaha kwa sababu alitamani kufanya kazi ya kuwahudumia watu hasa wenye uhitaji.

“Nilishangaa kila napoenda kazini siifurahii sana kazi yangu japo nilikuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza magari yaliyoharibika, nilijivuta (alijilazimisha) hivyo hivyo kwa miaka miwili,” anasema Kaduma.

Muuguzi huyo anasema siku moja wakati akiendelea na kazi hiyo, alisikia tangazo kuwa wanahitajika vijana watakaosomea kazi ya uhudumu hospitalini.

“Zilitoka nafasi 60 niliomba, nikapata kisha nikapewa mtihani cha ajabu nilifaulu vizuri na nikawa wa kwanza kwa hiyo mwaka 1983 nikamaliza mafunzo ya uhudumu na kuwa muhudumu,” anasema.

Alianza kazi yake katika Hospitali ya Wilaya ya Ludewa kabla ya kwenda kusoma mafunzo mengine ya uhudumu kwa mwaka mmoja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Kaduma anasema alipomaliza alifanya kazi kidogo kabla ya kwenda tena kusomea uuguzi na ukunga kwa miaka minne.

“Nilipomaliza kusoma miaka minne katika Chuo cha Mkomaindo, mkoani Mtwara nilirudi kazini na baadaye nikaamua kusoma tena miaka miwili ili nibobee kabisa kwenye taaluma yangu,” anasema muuguzi huyo.

Uuguzi ni wito

Anasema kihalisia kazi ya uuguzi inahitaji wito. Siyo kazi ambayo mtu anaweza kusomea na kufanya kwa sababu hana kazi nyingine.

Japo zamani kazi hiyo ilionekana kama ya wanawake, anasema siku hizi hata wanaume wanaifanya kutokana na ukweli kwamba inahusu kuokoa misha ya mgonjwa.

Kaduma anasema kama mgonjwa yupo kwenye hali mbaya na wakati mwingine ameelezwa kuwa ugonjwa wake ni wa kudumu au huenda akapoteza uhai wake, kauli nzuri na zenye kutoa moyo zinaweza kumpa nguvu na akasahau ugonjwa wake.

“Ikiwa utakimbilia uuguzi kwa sababu hakuna hazi nyingine ya kufanya utapotea, kazi hii inahusisha maisha na uhai wa watu, ulivyo ndivyo mgonjwa anaweza kupata naafuu au lah,” anasema Kaduma.

Anasema kauli mbaya na kutojali wateja ni kati ya vitu vinavyoitia doa taaluma hiyo. Anawashauri wauguzi kuwa makini na kuwajali wagonjwa wakifuata misingi yote ya taaluma ya uuguzi hasa wakijifunza kwa mwanzilishi wa kazi hiyo duniani Florence Nightingale.

Kaduma ambaye pia ni katibu wa kamati za wanawake kupitia vyama vya wafanyakazi, anasema kinachoweza kumpatia heshima muuguzi ni kauli na huduma nzuri kwa wagonjwa.

“Kwa sasa nipo kitengo cha maboresho ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa; nikiwa makamu mwenyekiti nasaidia kusimamia shughuli mbalimbali nje ya utabibu ndani ya hospitali hii, hata hivyo jambo muhimu na kubwa kwa muugusi siyo elimu yake, ni utu wake kwa mgonjwa,” anasema.

Changamoto

Kaduma anasema katika miaka aliyofanya kazi hiyo zipo changamoto mbalimbali zinazowagusa wauguzi wengi sio yeye peke yake.

Anasema kihalisia daktari hukaa na mgonjwa chini ya saa moja kisha anamuacha muuguzi akiendelea kuhakikisha kuwa anahudumiwa na kutumia dawa au kupata tiba iliyoandikwa kwenye dozi.

Anaeleza kuwa wakati mwingine linaweza kutokea tatizo kwa mgonjwa au kutopata kile anachostahili na mzigo wote akabeba muuguzi wakati hakuwa msababishaji.

“Yaani kuna wakati tunabeba lawama au kusingiziwa jambo lililo nje ya uwezo wetu, lakini kwa sababu ni sisi tunaokaa na mgonjwa muda mrefu, mzigo wa jambo hilo hujikuta tunabeba.

“Kikubwa hapo ni kulinda maadili tu, wakati mwingine unaweza singiziwa jambo au umepewa rushwa kumbe hukupewa sasa mpaka uchunguzi ufanyike unakuwa umeumia. Ila kama ulitunza maadili ya kazi, ukweli huwa unabainisha,” anasema Kaduma.

Kitu anajivuniaMama Kaduma anasema ni shangwe kuzalisha mtoto mwenye afya tele anayekuwa na kufikia malengo yake kimaisha.

Anasema wapo baadhi ya wanawake aliowahi kuwazalisha miaka 22 iliyopita ambao watoto wao wapo vyuo vikuu, elimu nyingine za juu na wengine wapo kazini.

Kwake hayo ni mafanikio makubwa, huku akisema kama asingetunza maadili yake ya kazi huenda baadhi ya watoto wangeshindwa kufika hatua waliyopo kwa sababu upo baadhi ya ulemavu ambao huwa unaweza kutokea wakati wa kujifungua.

“Mfano, usiposimamia ipasavyo na ukamuacha mama ambane mtoto kichwa kutokana na uchungu, unaweza mpata mtoto mwenye mtindio wa ubongo, kwa hiyo kwangu mafanikio ni kuona watoto niliowazalisha wapo salama na wapo mbali kielimu.”

Anasema kuna wakati wauguzi hufanya kazi zaidi kutokana na sababu nyingi hasa upungufu wao kazini jambo linalochosha mwili na akili.

Kaduma anasema wauguzi wanapaswa kupumzika ili kutimiza wajibu wao wa kuwahudumia wagonjwa.