VIDEO: BMT ivimulike vyama vya michezo

Tuesday July 30 2019

Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ jana ilicheza mchezo wa kwanza kuwania kufuzu michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (Chan), dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ kwenye Uwanja wa Taifa na zitarudiana Agosti 4.

Taifa Stars na Kenya zilicheza mchezo huo zikiwa na kumbukumbu ya kukutana katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), zilizofanyika Misri. Zilipokutana, Kenya ilishinda mabao 3-2. Timu hizo zilikuwa Kundi C pamoja na timu za Algeria, Senegal kwenye fainali hizo za 32 zilizoshirikisha timu 24 ikiwa ni mara ya kwanza katika michuano hiyo yenye hadhi Afrika na Algeria ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Senegal mabao 2-1 katika mechi ya fainali.

Mbali na mchezo huo wa jana, Taifa Stars inajiandaa kwa mechi za kufuzu fainali kama hizo Oktoba ikipangwa Kundi J pamoja na Libya, Equtorial Guinea na Tunisia.

Wakati Taifa Stars ikiwa katika michuano hiyo, Ligi Kuu Tanzania Bara imepangwa kuanza Agosti 23. Klabu mbalimbali ziko katika mchakato wa usajili kabla ya dirisha kufungwa Julai 31.

Joto la usajili na mechi za Taifa Stars zimechukua nafasi kubwa kulinganisha na michezo mingine kama kikapu, ngumi, netiboli, mpira wa meza, vishale, vinyoya na mingine.

Mchezo wa soka umechukua nafasi kubwa kulinganisha na mingine ingawa yote hiyo nayo ina viongozi wake waliochaguliwa na wanachama wao kuongoza vyama husika.

Advertisement

Licha ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya michezo, lakini hatuoni shughuli zao zikifanyika kama ilivyo kwa mpira wa miguu ambao kalenda yake ya mwaka inaonyesha kuna matukio mengi yanafanyika.

Katika miaka ya 1980 na 1990, michezo mingine nje ya soka ilikuwa na hadhi kubwa na ilifikia hatua ya kutoa ushindani mkubwa kwa mpira wa miguu.

Kwa mfano, mpira wa kikapu ulitamba nchini kiasi cha kutoa baadhi ya wachezaji kwenda kucheza nje ya nchi. Timu kama Pazi na Vijana, zilikuwa zikijaza mashabiki kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Mbali na timu hizo, pia kulikuwa na idadi kubwa ya timu zilizokuwa zimesheheni wachezaji nyota waliotikisa Afrika Mashariki na Kati. Oilers, Savio/Don Bosco, ABC, ni baadhi ya timu zilizokuwa tishio.

Pia mchezo wa netiboli ulipata umaarufu mkubwa timu kama Bora, Benki Kuu, Bima, Bandari, Jeshi Stars, JKT zikijaza watazamaji kwenye Uwanja wa Relwe, Gerezani na Uwanja wa Ndani na kutoa fursa kwa wachezaji kupata umaarufu ndani na nje ya nchi.

Tanzania ilikuwa tishio katika michezo nje ya soka na mara kadhaa iliwawahi kutwaa ubingwa katika michuano ya Kanda ya Tano hasa katika ngumi. Viongozi wa vyama hivyo waliopo madarakani wanapaswa kujitathmi utendaji wao wakati michezo wanayosimamia ikiwa hoi.

Kilio cha viongozi wengi wa michezo hiyo ni udhamini. Inawezekana, lakini cha kujiuliza hapa ni kwamba kipi kinapaswa kuanza? Wadhamini kuona kwanza hamasa katika michezo husika ndipo washawishike au kinyume chake?

Huu ni wakati mwafaka wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuvimulika vyama ambavyo havijatekeleza kalenda yake kwa ufasaha na kuchukua hatua stahiki zitakazokuwa na tija kwa ustawi wa maendeleo ya michezo nchini.