Bajeti ithibitishe nia ya kuendeleza kilimo

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga

Muktasari:

  • Kilimo kikiwa uti wa mgongo wa Taifa letu, kinaelezwa kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wote. Ni kutokana na umuhimu huo, kisipopata fedha za kutosha kitaendelea kuchechemea na kuathiri vibaya uchumi wetu.

Jana Wizara ya Kilimo iliwasilisha bajeti yake ya mwaka 2019/20 ya Sh253.85 bilioni yenye ongezeko la Sh83.65 bilioni ikilinganishwa na Sh170.2 bilioni zilizotengwa katika mwaka 2018/19.

Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema kati ya Sh253.85 bilioni, wizara ya kilimo imetengewa Sh208.04 bilioni, kati yake Sh143.57 bilioni ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ukilinganisha na Sh98.1 bilioni zilizotengwa kwa ajili hiyo mwaka jana.

Pia katika bajeti hiyo, zimetengwa Sh37.48 bilioni za Tume ya Umwagiliaji ambayo kati yake Sh32.5 bilioni ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hii ni hatua nzuri inayofaa kupongezwa, kwamba walau umeonekana umuhimu wa kuongeza bajeti ya kilimo, hasa ile ya shughuli za maendeleo ili kuendesha miradi ya kilimo itakayokiwezesha kukua na kuleta tija.

Kilimo kikiwa uti wa mgongo wa Taifa letu, kinaelezwa kuajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wote. Ni kutokana na umuhimu huo, kisipopata fedha za kutosha kitaendelea kuchechemea na kuathiri vibaya uchumi wetu.

Tunaipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya kusikia kilio cha wabunge katika mijadala yao ya Bajeti ya mwaka jana. Wabunge wengi walilia na bajeti kupungua kwa asilimia 23 kutoka Sh221 bilioni mwaka 2017/18 hadi Sh170.2 bilioni za mwaka 2018/19.

Mbali na kilio hicho, suala jingine lililojitokeza katika bajeti ya mwaka jana yalikuwa madai kuwa hata fedha zilizotengwa katika baadhi ya maeneo hazikufika katika baadhi ya maeneo.

Ingawa jana Waziri hakugusia utekelezaji huo, mwezi uliopita akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche alisema kilimo kinachoajiri asilimia 70 ya Watanzania na kutoa chakula kwa Watanzania kwa asilimia 100 na malighafi za viwandani kwa asilimia 80 mwaka jana kilitengewa Sh98.1 bilioni lakini zilizotolewa ni Sh42 bilioni.

Ni imani yetu kwamba kwa kuwa kilio cha bajeti kupungua kimesikika, hata kile cha fedha kutopelekwa kadri zilivyotengwa kitaendelea kusikika na hatimaye fedha zote kutumika kama zilivyopangwa.

Itakuwa haina maana ikiwa fedha zinatangazwa tu bungeni lakini inapofika katika utekelezaji hali inakuwa tofauti.

Ni matarajio yetu kwamba ikiwa Sh143.57 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika bajeti ya mwaka huu zitapitishwa na kupelekwa huko, upo uwezekano mkubwa wa kilimo chetu kupata tija zaidi na kulinufaisha taifa.

Hii inatiwa chachu na kuanzishwa kwa Tume ya Umwagiliaji ambayo imetengewa zaidi ya Sh37 bilioni, kati ya hizo Sh32 bilioni zikiwa za miradi ya maendeleo. Ikiwa fedha hizo zitatumika kwa umwagiliaji ni dhahiri kuwa tutakuwa na miradi mingi ya umwagiliaji.

Tumezungumza mara nyingi kwamba kilimo cha jembe la mkono na cha kutegemea mvua hakiwezi kumkomboa Mtanzania, badala yake kilimo kitakachotukomboa ni cha umwagiliaji ambacho bila shaka kinakwenda kufanyiwa kazi.

Ni maombi yetu kwamba Serikali kama imedhamiria kupanga bajeti hiyo ya kuinua kilimo ifanye hivyo kwa moyo wa dhati ili ifikapo mwaka hadithi iwe nyingine badala ya mvua kuchelewa au kukosekana na mazao kunyauka.

Vilevile tungependa kuunga mkono kauli ya Waziri Hasunga kuhusu mchakato wa bima ya mazao ili kuepukana na changamoto nyingine za kilimo zinazoleta hasara kama ukame, mafuriko, magonjwa na wadudu waharibifu wanaoharibu mazao.