MAONI: Bodi ya Ligi, TFF watupie macho mechi za Ligi Kuu Bara zilizosalia

Monday April 15 2019

Juzi, klabu bingwa ya Tanzania Simba ilitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa mabao 4-1 na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Pamoja na kutolewa, wawakilishi wetu hao wanastahili pongezi kwani waliweka rekodi ya kuingia katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa katika ngazi ya klabu barani Afrika.

Hiyo inamaanisha kwamba katika timu bora nane katika Bara la Afrika, Simba imo. Hii ni fahari kubwa kwa Simba na fahari kubwa kwa Tanzania na kwa sababu hiyo, tunaungana na wanamichezo wengine nchini kuipongeza timu hiyo kwa hatua iliyofikia.

Tunawataka wachezaji na viongozi kutokatishwa tamaa na matokeo hayo, bali wajipange na wawe na malengo makubwa zaidi katika msimu ujao.

Ushiriki wa Simba katika michuano hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa kwa Bodi ya Ligi na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika suala zima la upangaji wa ratiba.

Mechi nyingi ziliahirishwa kupisha Simba kushiriki mechi zake tangu hatua za awali hadi makundi hivyo kuifanya timu hiyo kuwa na michezo mingi ya viporo.

Kwa mujibu wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu hiyo ambayo inashika nafasi ya pili imecheza mechi 22 ikilinganishwa na mechi 31 hadi 33 ambazo timu nyingine shindani zimeshacheza.

Hiyo inaashiria kwamba baadhi ya timu zinaweza kumaliza ligi na kujua nafasi au msimamo katika ligi wakati Simba ikiwa na mechi nyingi mkononi jambo ambalo tunadhani litasababisha malalamiko lakini kikubwa zaidi litapunguza ladha na msisimko.

Kwanza tunadhani haikuwa busara kwa wahusika kuahirisha kwa kiwango kikubwa hivi mechi hizo lakini wakati tukiamini hivyo, tumebaki tukijiuliza sababu ya Bodi ya Ligi na TFF kuziruhusu baadhi ya timu kuingia katika mzunguko wa pili ilihali hazijacheza na kukamilisha baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza.

Mathalan, Simba haijacheza kabisa na Coastal Union ya Tanga wala Biashara United ya Mara mechi za awali huku baadhi ya timu zikiwa zimebakiza mechi tano kumaliza ligi.

Mbali na hizo, Yanga na Azam ambazo zimeshacheza mechi 31 na 30 hazijakutana hata mara moja katika ligi hiyo.

Tunadhani hii ni changamoto kubwa ambayo Bodi ya Ligi na TFF wanapaswa kuiangalia kwa umakini mkubwa.

Sifa ya mwanadamu ni kujifunza kila uchao. Wenzetu waliopiga hatua kubwa katika mchezo huu unaopendwa zaidi nchini na pengine sehemu kubwa ya ulimwengu, hawajawahi kuendesha ligi zao katika mazingira kama haya, wanashiriki ligi kama hizo na pengine kwa kiwango kikubwa zaidi cha timu katika ligi zao, tena hizo si za Ulaya pekee hata katika Bara la Afrika.

Tunaamini kasoro hii itakuwa ni funzo kwetu katika kufikia hatua nzuri na bora zaidi ya kiushindani kwenye ligi yetu ambayo msisimko wake umekuwa mkubwa ikilinganishwa na nyingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki.