Dalili za saratani ambazo hutakiwi kuzifumbia macho-2

Wiki iliyopita nilisema kutokwa na ute mchafu ukeni mara kwa mara au hata aina nyinginezo za uchafu ni dalili mbaya.

Ieleweke kuwa dalili hizi zinaweza pia kuashiria tatizo lingine kwenye mfumo wa uzazi mbali na saratani na kama zikiwa zinajirudia, basi hutakiwi kufumbia macho.

Mabadiliko kwenye matiti; siyo kila mabadiliko yanayotokea kwenye matiti yanaashiria saratani.

Pia, bado ni muhimu kuwasiliana na daktari kuhusu mabadiliko yanayojitokeza kwenye matiti ili yafanyiwe uchunguzi. Mjulishe daktari kuhusu uvimbe wa aina yoyote, mabadiliko katika chuchu ikiwamo kuziba kwa chuchu, uwapo wa rangi nyekundu, kuhisi ugumu au maumivu kwenye matiti kwa ujumla.

Daktari atakufanyia kipimo cha x-ray kwenye titi. Kipimo hiki kwa kitaalamu kinaitwa ‘Mammogram.’

Kipimo hiki kinatumika kuchunguza saratani ya matiti kwa wanawake ambao hawana dalili za saratani ya matiti.

Tunapozungumzia matatizo ya saratani. Basi wanaume hawapo nyuma baada ya tafiti za kiafya za hivi karibuni zinazothibitisha kuwa wanaume wengi wapo hatarini kuugua baadhi ya aina za saratani ikiwamo ile ya tezi dume. Hii ni aina ya saratani ambayo hutokea wakati tezi dume zinapanuka na kuongezeka ukubwa unaochochea uwapo wa zile seli zinazosababisha saratani.

Saratani ya tezi dume huwapata wanaume ambao kiumri kuanzia miaka 40 na kuendelea na hasa wale ambao historia zao za kifamilia zinahusiana na magonjwa ya saratani yaani kupitia vinasaba

Saratani ya tezi dume ina dalili nyingi, lakini baadhi ya dalili zake kuu ni pamoja na kupata haja ndogo mfululizo kupita kiasi, lakini kwa baadhi ya watu hujisikia kwenda haja ndogo lakini mkojo unashindwa kutoka na kuhisi kama umejibana sehemu kwa ndani kukiambatana na maumivu.

Dalili nyingine ni mkojo kuchanganyika na damu na kuanza kupoteza uwezo wa kushiriki tendo la ndoa. Mwanaume unapoona dalili hizi hasa kama umri wako tayari umeshafikia miaka 40 na kuendelea, ni bora uwaone wataalamu wa afya. Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ SUPER SPOECIALIZED POLY-CLINIC.