Dalili za saratani ambazo hutakiwi kuzifumbia macho

Februari 4 ilikuwa Siku ya Saratani Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ili kujikumbusha hatua na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Naishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuanzisha kampeni mbalimbali ili kuinua uelewa kuhusu magonjwa ya saratani.

Pia, nawashukuru wasomaji wangu kwa mirejesho ninayopokea kutoka kwenu kuonyesha mnaelimika na elimu tunayoitoa ya magonjwa na hasa magonjwa ya saratani.

Naendelea kuwakumbusha, tofauti na wengi wanavyodhani kuwa saratani haitibiki, la hasha! Hiyo ni dhana potofu! Saratani inatibika endapo tu utaiwahi kuitibu katika hatua zake za awali. Wagonjwa wengi wanakuja hospitali wakiwa tayari saratani zao zimeshakuwa hatuza za mbele na hapo ndipo ugumu wa matibabu unapoanza.

Hivyo, suluhisho pekee la kukabiliana na saratani ni kufanya vipimo mara kwa mara, kuwa makini na dalili zake na kuwahi matibabu, hapo utakuwa umeikabili saratani kwa asilimia 100 na ukapona.

Ndiyo maana leo, nakueleza dalili mbalimbali ambazo kwa kiasi fulani huashiria saratani na pindi unapoziona, hupaswi kuzifumbia macho, unatakiwa kupata vipimo haraka.

Mzunguko wa hedhi usio na mpangilio pamoja na maumivu ya kiuno ya mara kwa mara.

Ninatumaini neno saratani ya shingo ya kizazi siyo geni kwa walio wengi hasa nyakati hizi ambazo watumishi wa afya tumekuwa tukijitahidi sana kuinua uelewa wa magonjwa ya saratani na hasa saratani hii ya shingo ya uzazi.

Hii ni aina ya saratani ambayo huanza na kushambulia shingo ya uzazi kabla ya kusambaa sehemu nyinginezo za mwili.

Baadhi ya dalili kuu za aina hii ya saratani ni pamoja na maumivu ya kiuno yasiyokoma, kupata hedhi zisizo na mpangilio ambazo hazipo kwenye mzunguko bali zinatoka tu mara kwa mara, na wakati mwingine hata kutokwa na damu unaposhiriki tendo la ndoa au hata baada ya kumaliza.

Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ SUPER SPOECIALIZED POLYCLINIC.