UCHAMBUZI: Dodoma sasa imekuwa makao makuu

Tuesday July 9 2019

 

By Habel Chidawali

Usemi kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, umetimia kwa Watanzania baada ya kushuhudia namna ambavyo Dodoma imebadili sura yake kutokana na hatua ya Serikali kuhamia hapa rasmi.

Kila kilichokuwa kikipatikana Dar es Salaam sasa kinapatikana Dodoma na kila lililopangwa kufanyika huko linaweza kufanyika mkoani hapa pasi na shaka yoyote.

Safari hii ilichukua zaidi ya miaka 40 tangu ilipotangazwa rasmi na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1973.

Kwa hali ilivyokuwa, wengi hawakuamini kama mji huu ungeweza kubadilika, mitazamo hasi ilikuwa mingi kuliko chanya na waliokata tamaa walikuwa wengi kuliko walioamini ipo siku itawezekana.

Hata hivyo, imewezekana na itawezekana zaidi pale Rais John Magufuli atakapohamia rasmi mkoani hapa ukizingatia hata ile Ikulu ya Chamwino wameshaiingiza ndani ya ramani ya jiji.

Kwa waliokuja mwaka jana, wanaona tofauti lakini waliokuja mwaka juzi wanaona tofauti kubwa zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya jiji. Hii ndiyo Dodoma walioingoja.

Advertisement

Kwa wakazi wa mji huu watakubali kuwa mabadiliko ni makubwa katika kila mtaa, licha ya ukweli kuwa bado kuna mapengo kidogo ya majengo ya zamani ambayo yanaonyesha sura ya zamani.

Mwendo wa Dodoma sasa ni mchakamchaka kwani ukitembea unaachwa, watu wanakimbia, wengine wanaruka ilimradi kila mmoja anachangamkia fursa zinazokuja na zilizopo.

Jiji limepanuka, majengo yamejengwa katika mpangilio mzuri wenye sura ya kuvutia hata kwa wageni. Pia, barabara zake zimesambaa katika mtandao mpana unaokwenda sanjari la usambazaji wa kasi wa huduma za maji na umeme.

Hakuna ubishi kuwa sura ya makao makuu imetimia, kinachosubiriwa ni kuona moshi mweupe wa mkuu wa nchi kuingia katika kaya yake kwa ajili ya kuanza maisha na kwa dalili zilivyo, huenda hatokawia.

Safari ya kuja Dodoma ilihitaji uamuzi mgumu kwani miaka 43 bado ilikuwa katika mtazamo na kauli za mdomoni ingawa uamuzi wa ‘Hapa Kazi Tu’ umesaidia kusukuma viongozi na watu waliokuwa wamejichimbia mizizi katika jiji kubwa la Dar es Salaam nao wakajikuta wamekuja wenyewe bila shuruti.

Ule usemi wa mgeni njoo ili mwenyeji apone, unasadifu yanayoendelea kwa katika jiji hili kwa sasa; biashara zimepanuka, huduma za usafiri zimeongezeka, uboreshaji wa majengo umefanyika na majengo mapya yanasimama kila uchao.

Mtandao mpana wa barabara za lami umefanya jiji hili kushika nafasi ya pili kwa urefu wa barabara hizo ikiwa ni nyuma kidogo ya barabara za Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Huduma za afya zimeboreshwa, hospitali ya rufaa ya mkoa kwa sasa inapokea wagonjwa wengi ikijivunia kuhudumia viongozi wa Serikali.

Pia hospitali kubwa na ya kisasa ya Benjamin Mkapa na zile za taasisi za dini kama Ntyuka na St Gemma ni kielelezo tosha kuwa wamejipanga kuhakikisha kwamba afya za watu zinaimarika wanapokuwa makao makuu ya nchi.

Kwa upande wa usafi, bila shaka mashindano yatakapokuja jiji hili litakuwa miongoni mwa miji itakayofanya vizuri, licha ya kuwa usafi wa mtu mmojammoja bado ni changamoto inayotakiwa kufanyiwa kazi ili kuondokana na msukumo.

Dampo la kisasa la Chidaya ni ushahidi tosha kwamba jiji limedhamiria kufanya kazi kidigitali, huku magari ya kisasa yakiendelea kuzunguka katikati ya jiji kwa ajili ya kuona kila takataka inakusanywa.

Kwa baraza la madiwani na mkurugenzi mtendaji wanastahili pongezi, kwa Serikali kuu iliyofanya uamuzi huo inastahili sifa njema na wananchi wanapaswa kutiwa moyo zaidi kwa mchamchaka wa maendeleo unaofanyika.

Jambo la kuangalia hapa ni namna gani Serikali inavyoweza kuwasaidia wakazi wa Dodoma na wageni katika baadhi ya maeneo ambayo yanaleta picha mbaya ikiwamo kina dada wanaoshinda na kulala hapa Uhindini katika Mtaa wa CDA Hall.

Juhudi zimefanyika kuwaondoa lakini huenda Serikali haijaweka msukumo na kulisaidia Jeshi la Polisi ipasavyo. Wanakamatwa na wanatangazwa na kuonyeshwa picha zao, lakini siku inayofuata wanarudi. Hili bado ni doa.

Ukiachilia hayo, mnada wa Msalato nao ni vyema ukatazamwa katika eneo la machinjio na kuboreshwa. Ujengewe uzio ili kuwe na faragha kwa wanyama wanaochinjwa.

Vinginevyo, Dodoma imekuwa ni kimbilio, mahali salama kwa uwekezaji, sura ya kupendeza na mji wenye kuigwa.

Habel Chidawali ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Dodoma. Anapatikana kwa simu 0657861733