Dodoma ya sasa sio ile ya kina Nyerere na Kikwete

Muktasari:

  • Pale barabara ya sita angekumbuka jengo zuri la CCM lililo katikati ya barabara hiyo na barabara kuu mahali alipokuwa akifanya vikao vya chama chake.

Ikiwa Mwalimu Julius Nyerere atafufuka leo kisha akaomba kutembelea mitaa mbalimbali katikati ya Dodoma, bila shaka atakumbuka mitaa ya barabara ya sita na ya saba.

Pale barabara ya sita angekumbuka jengo zuri la CCM lililo katikati ya barabara hiyo na barabara kuu mahali alipokuwa akifanya vikao vya chama chake.

Barabara ya saba angekumbuka mahali alipolala mara nyingi wakati wa harakati za Uhuru alipokuja Dodoma na hata baada ya Uhuru alikwenda kwa rafiki yake ambaye naye sasa ni marehemu.

Mbali na Nyerere, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete naye atashangaa ikiwa atazunguka mitaa hiyo na kwenda barabara ya nane alipokuwa anashona sare za chama chake wakati wa vikao kipindi alipokuwa mbunge na waziri. Atafika hapo akitumia barabara ya One way.

Ni One way hiyohiyo ambayo ilijizolea umaarufu kwa kila mtu huku wenyeji wakiita barabara ya Mang’ongo wakiwa na maana ya vigae vilivyojengwa chini yake. Ama kweli hadi sasa bado vinapendeza, lakini havionekani kutokana na utitiri wa bidhaa zilizomwagwa chini.

Uzuri wa One way haukuwa na mfano wake kwa kila mtaa kutokana na mpangilio wa maduka ulivyowekwa na kwa sehemu kubwa shughuli za biashara na uchumi wa barabara hiyo unatosha kuliingizia Taifa mapato mengi.

Hongera Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuendelea kuienzi barabara hii na kuifanyia ukarabati wa mara kwa mara ili isiweze kuchakaa licha ya kuwa haiwezekani kupanuliwa.

Hata hivyo, hii siyo One way ya enzi za kina Jakaya Kikwete wala Mwalimu Nyerere. Hii ni nyingine kabisa, ni eneo ambalo limegeuzwa kuwa sawa na dampo, hakuna mtu anayefurahi kupita mahali hapo labla kwa shida kubwa. Mpangilio wa bidhaa katika eneo hili ni usumbufu mtupu kwa waendao kwa miguu; hakuna ustaarabu, hakuna uhuru. Ni kelele zilizopitiliza.

Eneo hili kwa sasa limepoteza ubora wake lakini hakuna anayejali, siasa zimetamalaki na kuharibu kabisa mpango mzuri uliokuwa umewekwa na Manispaa kwa wakati huo sasa ni Jiji.

Huwezi kutazama ukaona maduka mazuri yaliyopangwa kwa mstari mnyoofu na badala yake macho yanaishia kwenye milima ya bidhaa zilizomwagwa chini barabarani, huku vipaza sauti vya kutangaza bei za bidhaa vikishindana kwa mvumo wa juu.

Umekuwa ni mtaa wa Machinga lakini wengi wakionekana kuwa na mitaji mikubwa iliyopitiliza hata kile kiwango kinachotajwa na Serikali kuwa ndiyo kiwango cha mfanyabiashara wa hali ya chini.

Ni kweli kuwa Serikali ilishapiga marufuku kwa wafanyabiashara wadogo kwamba wasisumbuliwe, lakini hii imekuwa zaidi kwamba hata huwezi kumshika mkono mtoto uwapo kwenye barabara hii, badala yake unatakiwa kwenda mstari mnyoofu na vita ni pale unapotaka kuingia dukani.

Kila kukicha barabara hii inazidi kupoteza ubora wake kwa kujaza watu wenye mali nyingi, hapaonekani mtu wa kukemea na hivyo kufanya uhuru wa watu kuwa kuzidi mipaka.

Wenye maduka wanalia bila kupata mtu wa kuwasemea, hawauzi licha ya kuwa wanazo leseni walizokatia hapo badala yake wanafanya kazi ya kudunduliza na kulipa kodi ya Majengo kwa wajanja waliowahi kujenga enzi hizo.

Hapa ndipo mahali ambapo vigogo walikuwa wakinunua vitambaa vya suti. Kimsingi, palionyesha sura halisi ya Dodoma na ndipo palipokuwa pakifanywa makutano ya watu wengi waliotoka maeneo ya mbali. Hii ndio One Way.

Mamlaka tupieni jicho eneo hili, isaidieni Dodoma katika jambo hili ili kumtendea haki Rais katika uamuzi wake wa kuufanya mkoa huu kuwa eneo la shughuli rasmi za kiserikali.

Ingawa zinatajwa biashara, lakini mahali hapa pangeweza kufanywa kama ilivyo eneo la Nyerere Square ambapo bidhaa zinafunguliwa mchana na kumwagwa barabarani kisha njia za magari zinafungwa lakini si wakati wote kama mtaa huu.

One way hii ikiachwa kama ilivyo itakuwa ni hatari, msongamano wa bidhaa ambazo sina uhakika kama zinalipiwa kodi, si mzuri hata kidogo, watu wanafunga maduka yao wanakuja kutandika chini ili kufuata wateja maana kule ndani hawawaoni tena.

Sina uhakika kama huu ndio utekelezaji wa kauli ya Rais John Magufuli kwamba wafanyabiashara wadogo wasibughuziwe.

Siasa ziachwe ili kusaidia eneo hili. Kama maeneo kama Nyerere Square, Independence, Jamatini, Sabasaba na bonanza huko kote kuna mpangilio wa wafanyabiashara, kwa nini hapa inashindikana?

Habel Chidawali ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Dodoma