UCHAMBUZI: Dosari hizi ziondolewe mapema EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliasisiwa na nchi tatu – Tanzania, Kenya na Uganda. Awali ilianzishwa mwaka 1967 na kufa miaka 10 baadaye yaani mwaka 1977.

Hata baada ya kufufuliwa nchi hizo tatu ndizo zilihusika katika mkataba wa wakuu wa nchi wa Novemba 30, 1999 na Julai 7, 2000 ilianza kazi rasmi ikiwa inajengwa katika nguzo nne.

Nguzo hizo ni ushirikiano katika masuala ya soko la pamoja, forodha, fedha na shirikisho la kisiasa.

Mbali na hayo, tangu kuanza kwa jumuiya iliyovunjika 1977, kulikuwapo na tofauti za kimtazamo baina ya viongozi, wananchi na wadau wengine.

Katika nchi hizi tofauti ziliibuka hata katika sera za nchi. Wakati Kenya ikijikita katika ubepari, Tanzania ilikuwa inajiimarisha katika ujamaa, lakini wakati huo kulikuwa na mgongano mkubwa wa masuala ya utawala bora nchini Uganda.

Hata hivyo kuanzia miaka ya 1990, marais wa Tanzania, Kenya na Uganda walianzisha mchakato wa kuifufua jumuiya hiyo.

Baadaye Rwanda na Burundi zilijiunga 2007 na Sudan Kusini ikajiunga 2016.

Viongozi hawa walifanikiwa kuifufua jumuiya hiyo na hakika hadi leo imekuwapo na imefanya mambo makubwa.

Miongoni mwa mafanikio ni kuanzishwa kwa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Mahakama ya Afrika Mashariki, soko la pamoja, umoja wa forodha na sasa mchakato unaendelea kuwa na sarafu moja pamoja na shirikisho la kisiasa.

Novemba 30, wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki walitarajiwa wote kukutana katika mkutano wao wa kawaida wa kila mwaka.

Hata hivyo, mkutano huo ulikwama kutokana na wajumbe kutoka Burundi yaani Rais Piere Nkurunzinza, mawaziri wake au watendaji wa Serikali ambao wangemwakilisha kushindwa kuhudhuria.

Kutohudhuria kwa Burundi kulisababisha kukwama kwa mkutano huo, licha ya kutumia mamilioni ya fedha katika maadalizi yake imeleta shida.

Pia taarifa zilizopatikana katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha zilieleza kuwa Burundi kabla ya kikao hicho iliandika barua kuomba mkutano uahirishwe, lakini iligonga mwamba.

Kutofika kwa Burundi na hivyo kukwamisha mkutano kunaleta tafakuri kubwa katika mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Miongoni mwa tafakuri hizo ni iwapo mkataba wa Afrika Mashariki unalazimisha kila nchi kufikia maridhiano katika maamuzi yote?

Je, EAC imejipanga vipi kukabiliana na changamoto ambazo zimeanza kujitokeza sasa? Walio wengi wanajua msuguano uliopo sasa baina ya Burundi na Rwanda na wengi wanaamini hata Burundi kususia mkutano huo kulitokana na ukweli kuwa Rwanda ilikuwa inakwenda kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

Lakini je, tujiulize nchi hizi zimejipanga kiasi gani kuhakikisha zinatatua mgogoro uliopo sasa baina ya Rwanda na Burundi?

Hivi hali itakuwaje ikiwa mkutano unaofuata itakosekana nchi nyingine mojawapo.

Pia tumeelezwa kuwa hata Bunge la Afrika Mashariki limeshindwa kukutana kutokana na ukata. Hivi hii mivutano haiwezi kusababisha nchi kushindwa kuchangia?

Wahenga walisema usipozipa ufa utajenga ukuta na hili la Burundi ni ufa ndani ya jumuiya ambapo sasa ni lazima dosari ambazo zimeanza kujitokeza ziondolewe.

Dosari hizo ni pamoja na mkataba wa Afrika Mashariki katika ibara ya 12 ambayo inaeleza kuwa mkutano wa wakuu wa nchi za EAC ni lazima uhudhuriwe na marais wa nchi zote au wawakilishi wao ndipo utakuwa halali.

Ibara hiyo pia inaeleza kuwa uamuzi wa marais wa jumuiya hiyo utafikiwa baada ya kufikia maridhiano baina ya marais wote sita au wawakilishi wao.

Katika mkutano uliokwama wakuu wa nchi; Paul Kagame (wa Rwanda) aliwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje, Richard Sezibera na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini aliwakilishwa na Waziri wa Biashara, Paul Malong lakini marais wa Tanzania, Kenya na Uganda walikuwapo. Hivyo itoshe kutoa wito kwa watendaji wa EAC kuzifanyia kazi changamoto zilizoanza kujitokeza katika jumuiya hii kabla ya haijasambaratika kwa sababu viashiria vya mgongano vimeanza kujitokeza na hivyo kuwapo kwa tishio kubwa la uhai wa jumuiya.

Tunajua hivi sasa kuna mkakati wa kuipokea Somalia ambayo ina changamoto nyingi, sasa je, kwa mkataba uliopo jumuiya itaweza kufanya kazi?

Hata hivyo naamini jumuiya ina uwezo wa kupambana na changamoto zake lakini ni muhimu kuzipatia ufumbuzi mapema zaidi.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi. 0754296503