Elimu kwa mtoto wa kike chachu ya maendeleo

Naikumbuka Siku ya Mtoto wa Kike ambayo mwaka huu ilikuwa na kauli mbiu isemayo: “GirlForce: Unscriptured and Unstoppable”.

Ni siku inayoadhimishwa duniani kote kila ifikapo Oktoba 11 ya kila mwaka.

Kauli mbiu hii pia inasadifu mafanikio yaliyofikiwa, kwa wasichana tangu kupitishwa kwa Azimio la Beijing na Jukwaa la kuchukua hatua.

Kusudi lake kuu likiwa ni kuwawezesha wasichana na kuwasaidia kupata haki zao, ili waweze kukabiliana na changamoto ulimwenguni kote na kukidhi mahitaji yao.

Nasi Watanzania tunaungana nao kwa msemo wetu wa Kiafrika unaosema “ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii.”

Ni muhimu sana kuadhimisha siku hii ya mtoto wa kike duniani hasa ukizingatia changamoto anazopitia mtoto wa kike hadi sasa.

Kwa mfano, kuboresha viwango na ubora wa elimu ni muhimu kuwawezesha vijana hasa watoto wa kike kutimiza malengo yao kwa ufanisi na kwa uwezo wao wote.

Katika nchi ambazo kuna upungufu wa kijinsia, fursa za kujitegemea, ujuzi binafsi, mawazo dhamiri, nia/nguvu thabiti hususan fursa za kujikwamua kiuchumi huwa ni ndogo kwa upande wa wasichana.

Ni kwa sababu hii wengi huona hakuna haja ya kuendelea na masomo huku wengine wakiozwa.

Pengo la kijinsia ni kubwa licha ya ongezeko ya watoto wa kike waliopata elimu, ukilinganisha na watoto wa kiume kwenye vipaumbele vya kupata elimu au hata fursa nyingine za kimaisha.

Kuna sababu zinazozuia ushiriki mdogo wa wanawake katika majukwaa ya fursa. Hii ni pamoja na mtazamo wa mtu binafsi kwa masuala yanayohusiana na ufanisi wa kujitegemea, uwepo wa msaada kwenye mitandao ya kijamii, mifumo, sheria, kanuni, maadili na kanuni zinazofafanua umuhimu wa kumpa kipaumbele mtoto wa kike.

Licha ya kupiga hatua nzuri, tafiti zinaonyesha wavulana bado ni wengi zaidi kuliko wasichana shuleni na yawezekana wasichana milioni 16 hawatokwenda shuleni maisha yao yote. Hii ni kwa mujibu wa kituo cha takwimu cha Unesco.

Ingawa ni kweli kwamba idadi ya wasichana wengi wenye umri mdogo, kwa sasa wanahudhuria shule kuliko hapo awali, lakini wingi wa vikwazo wanavyokumbana navyo bado ni vingi sana hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Vikwazo vinavyowakumba watoto wa kike ni kama vile mila na tamaduni potofu za kijamii, ukatili wa kijinsia, umaskini, ndoa za mapema na za kulazimishwa.

Nyingine ni mimba zisizotarajiwa, ubaguzi wa kijinsia na fikra nyingine potofu ambazo ni sababu kubwa ya ukosefu wa elimu kwa watoto wa kike duniani.

Ni wazi kuwa kuna mengi ya kufanya kuboresha uwakilishi wa watoto wa kike katika maendeleo.

Ni muhimu kuwawezesha watoto wa kike wawe na ujuzi na kuimarisha ujasiri wao kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo na shughuli ambazo zinaweza kuwa na faida kubwa.

Hatua za kupunguza utofauti wa jinsia ni pamoja na kuunganisha mtalaa wa ubunifu

Huu ni mtalaa unaohusisha wanafunzi hasa watoto wa kike katika elimu ambayo inahamasisha mawazo ya ubunifu.

Pia, kuwashirikisha wavulana/watoto wa kiume katika kukuza dhamira nzuri na mabadiliko ili kujenga na kuimarisha uthubutu wa wasichana.

Tuwahamasishe walimu shuleni, viongozi mbalimbali kuwasaidia watoto wa kike kwa kuweka mazingira salama ya kijinsia yaliyo rafiki, ili waweze kujiamini.

Habari njema ni kwamba mbali na elimu ya darasani, programu na fursa mbalimbali za ubunifu zimeanzishwa ili kumsaidia mtoto wa kike kufanya vitu anavyovipenda na huenda vikampa kipato hapo baadaye na uhuru wa uchumi kwa jumla

Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali bado kuna nafasi ya kuboresha! Tafiti zinaonyesha pia kuwa uwekezaji wa elimu kwa mtoto wa kike, husababisha ukuaji wa uchumi kwa kasi zaidi kutoka ngazi ya familia hadi ngazi ya taifa.

Phelisters Wegesa ni mwanafunzi anayesoma nchini China